1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Koome awashtumu "wanasiasa" kwa kulichafua jina la polisi

8 Agosti 2023

Inspekta Jenerali wa polisi nchini Kenya Japhet Koome amedai kuwa baadhi ya watu walikodisha maiti kutoka vyumba vya kuhifadhia maiti ili kutumika kama wahanga wa ukatili wa polisi wakati wa maandamano ya hivi karibuni.

Kenia | Protest Steuererhöhung
Afisa wa polisi akikabiliana na waandamanaji mjini NairobiPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Inspekta Jenerali wa polisi nchini Kenya Japhet Koome amedai kuwa baadhi ya watu walikodisha maiti kutoka vyumba vya kuhifadhia maiti ili kutumika kama wahanga wa ukatili wa polisi wakati wa maandamano ya hivi karibuni ya kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha, ambayo mashirika ya haki yanasema mamia ya waandamanaji waliuawawa.

Inspekta Jenerali wa polisi Japhet Koome amewaambia waandishi wa habari leo kuwa baadhi ya watu walikula njama na wahudumu wa vyumba vya kuhifadhia maiti ili kukodisha maiti na picha zao kuchapishwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwa nia ya kulipaka tope jina la polisi.

Soma pia: Ruto: Niko tayari kukutana na Odinga wakati wowote

Bwana Koome hata hivyo hakutoa ushahidi wala maelezo zaidi kuunga mkono madai hayo, na badala yake amesisitiza kuwa polisi walitekeleza majukumu yao kama waliyoagizwa na katiba.

Mashirika ya haki za binadamu yamesema polisi waliua watu wakati wa mfululizo wa maandamano ya mwezi Julai yaliyoongozwa na muungano wa upinzani ambao unamshinikiza Rais William Ruto kufutilia mbali sheria ya fedha ya mwaka 2023 iliyopandisha ushuru wa bidhaa muhimu na hivyo kuongeza gharama ya maisha.

Upinzani watishia kuwasilisha kesi katika mahakama ya ICC

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Upinzani umeelezea dhamira yao ya kuwasilisha kesi dhidi ya maafisa wa polisi waliohusika na mauaji hayo katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC, hatua ambayo Koome ameilezea kama "vitisho.”

Inspekta Jenerali huyo wa polisi amesema hawatayumbishwa na vitisho vya kuwafungulia kesi katika mahakama ya ICC na kwamba wataendelea kupambana na waandamanaji kwa nguvu licha ya wasiwasi kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binadamu. 

"Tuna wajibu wa kuhakikisha nchi hii ni salama, hilo ni agizo tutakalolitekeleza bila uwoga wala upendeleo. Propaganda haitotuvunja moyo. Wacha waendelee kututisha kwamba fulani na fulani watapelekwa ICC. Hilo haliathiri lolote kuhusu kujiolea kwetu."

Amnesty International Kenya, pamoja na vyama vya madaktari na wanasheria nchini humo vimesema takriban watu 11 waliuawa katika maandamano hayo, wengi wao wakipigwa risasi wakati wakiwakimbia polisi au wanapojaribu kujisalimisha.

Nalo shirika lengine la kutetea haki za binadamu la IMLU limesema kiasi watu 35 waliuawa na polisi kote nchini Kenya katika maandamano ya mwezi Julai. Upinzani nao umeeleza kuwa watu 50 waliuawa wakati wa maandamano hayo, na ulitoa video kama ushahidi kuonyesha wahanga wa ukatili wa polisi.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi