Korea Kaskazini iko tayari kwa mkutano wa tatu na Marekani
13 Aprili 2019Kim ameyasema hayo katika hotuba yake ya Bunge la Korea Kaskazini siku ya Ijumaa. Hotuba hiyo ameitoa saa kadhaa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kukutana na kiongozi wa Korea Kusini Moon Jae-in mjini Washington Marekani na kujadili umuhimu wa mazungumzo na Korea Kaskazini, kuhusu silaha za nyuklia.
Katika mkutano wao huo wa Alhamisi mjini Washington, Trump alimwambia Moon kwamba yuko tayari kwa mkutano wa kilele wa tatu na Kim, lakini Marekani itaendelea kuiwekea Korea Kaskazini vikwazo vya kiuchumi.
Vikwazo vitaendelea
Kim alirejea tena matamshi yake ya awali kwamba katika hotuba yake bungeni na kusema uchumi ulioporomoka wa Korea Kaskazini utaendelea kujikongoja licha ya vikwazo vikali vya kimataifa ilivyowekewa kutokana na mpango wake wa silaha za kinyuklia na kwamba hatoshikilia kufanya mikutano na Marekani kwa lengo la kutaka kuondolewa vikwazo.
Kim aliwahimiza Wakorea kujijengea uwezo wa kujitegemea ili waweze kupambana na kile alichokieleza kuwa "nguvu ya maadui" wanaoamini Korea Kaskazini inaweza kusambaratishwa kwa kutumia vikwazo.
"Sisi hakika tunaunga mkono suala la kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo na majadiliano. Lakini mtindo wa Marekani wa mazungumzo wa kulazimisha kwa masharti hautufai sisi, wala hatuna haja nao," amesema Kim wakati wa hutuba yake hiyo.
Kulingana na Shirika Kuu la Habari la Korea, KCNA, Kim alisema kusambaratika kwa mkutano wa kilele ulitakiwa kufanyika Febuari kulitokana na kile alichokieleza kama masharti ya Marekani ya upande mmoja, ambayo alisema yalimpa wasiwasi iwapo Marekani ina nia ya kweli ya kuimarisha mahusiano kati yao. Lakini Kim pia aliongeza kwamba uhusiano wake binafsi na Trump ni mzuri na wanaweza kutumiana barua wakati wowote.
Trump na Kim walikutana mara mbili. Mara ya kwanza ilikuwa Hanoi mji mkuu wa Vietnam mnamo mwezi Febuari na mara ya pili ilikuwa Singapore mwezi Juni. Mara zote mbili walishindwa kufikia makubaliano ya mkataba wa Marekani kuondolea vikwazo vya kiuchumi Korea Kaskazini ili nchi hiyo nayo kwa upande wake iachane na mpango wake wa kutengeneza silaha za kinyuklia pamoja na makombora.
Mkutano wa Hanoi uliibua suali zito la iwapo tuko sahihi katika kuchukua hatua ya uamuzi wa kimkakati na ujasiri na kama Marekani kweli ina nia ya kuimarisha uhusiano na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea," alieleza Kim.
Mjini Hanoi, Marekani ilikuja katika mazungumzo huku ikijikuna kichwa kutafuta njia ambazo haziwezekani kabisa, haikuwa tayari kukaa nasi kwa majadiliano ya ana kwa ana kutatua tatizo lililoko," aliongeza Kim.
"Tutangoja kwa subira uamuzi wa kijasiri wa Marekani hadi mwisho wa mwaka huu lakini nadhani itakuwa vigumu kupata fursa nzuri kama ya mkutano wa kilele uliopita," alimalizia Kim.
Matamshi ya Kim yanaashiria kwamba hatokwama kwenye mjadala na Marekani daima, amesema Kim Dong-yup wa Taasisi ya Chuo Kikuu cha Mafunzo ya Mashariki ya Mbali nchini Korea Kusini.
"Hilo huenda likamaanisha kwamba Korea Kaskazini ina mipango ya kuimarisha mahusiano yake ya kidiplomasia na nchi nyingine," alisema Kim Dong-yup.
Korea Kusini kama mpatanishi
Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in, amechukua nafasi ya mpatanishi kati ya Kim na Trump. Lakini wakati wa ziara yake mjini Washington Alhamisi, alishindwa kupiga hatua zozote zile za angalau kusonga mbele kidogo katika suala la kuondoa kabisa silaha za nyuklia kwenye rasi ya Korea.
Hata hivyo, Moon anatarajiwa kukutana tena na Kim na kujaribu kutafuta makubaliano ya aina fulani.