Korea Kaskazini kuondowa wafanyakazi wake Kaesong
8 Aprili 2013Kim Yang-Gon afisa mwandamizi wa chama tawala nchini Korea Kaskazini amekaririwa akisema katika taarifa kwamba Korea Kaskazini itawaondowa wafanyakzi wake wote katika kanda hiyo na wakati huo huo kusitisha kwa muda shuguli zinazofanyika hapo na kuangalia iwapo iruhusu kuwepo kwa kituo hicho au ikifungilie mbali.Kim ambaye alitembelea kituo hicho cha viwanda cha Kaesong leo asubuhi amesema wamelazimika kuchukuwa hatua hiyo kutokana na uchochezi wa kivita unaotaka kuifanya Kaesong kuwa mahala pa malumbano kutokana na kuongezeka kwa hali ya wasi wasi wa kijeshi katika Rasi ya Korea.Ameongeza kusema kwamba hali itakavyokuwa huko mbele itategemea mwenendo wa serikali ya Korea Kusini.
Wafanyakazi wa Korea Kusini wapigwa marufuku
Korea Kaskazini imewapiga marufuku mameneja wa Korea Kusini na wafanyakazi wake kuvuka mpaka na kuingia katika kituo hicho cha viwanda kilioko kilomita 10 ndani ya ardhi ya Korea Kaskazini tokea Jumatano.Hadi sasa makampuni 13 kati ya 123 yenye kuendesha shughuli zake katika eneo hilo yamelazimika kusitisha uzalishaji kutokana na uhaba wa mafuta na mali ghafi. Zaidi ya wafanyakazi 300 wa Korea Kusini ambao walikuwa wakifanya kazi katika kituo hicho cha viwanda cha Kaesong wakati marufuku hiyo ilipotangazwa wamerudi Korea Kusini lakini zaidi ya 500 wameendelea kubakia katika kituo hicho.
Jaribio la nuklea haliko wazi
Wakati hayo yakijiri Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini imekanusha dokezo kwamba jaribio la silaha za nuklea linalotaka kufanywa na Korea Kaskazini ni jambo lililo wazi na kwamba nyendo zilizorepotiwa kuwepo kwenye mtambo wa nuklea wa nchi hiyo zilikuwa ni za kawaida. Taarifa hii inapingana na kauli zilizotolewa awali na serikali ya nchi hiyo.Tetesi zimekuwa zikiongezeka kwamba Korea Kaskazini itachukuwa hatua fulani ya uchokozi hivi karibuni kwa kufanya jaribio la silaha za nuklea au kufyetuwa kombora kufuatia wiki kadhaa za vitisho vya shari dhidi ya Korea Kusini na Marekani.Awali akizungumzia repoti za vyombo vya habari Waziri wa Korea Kusini anayehusika na masuala ya muungano na Korea Kaskazini Ryoo Kihi-jae ameiambia kamati ya bunge kwamba nyendo zilioko katika mtambo wao wa nuklea zimeonyesha kwamba nchi hiyo inataka kufanya jaribio la silaha za nuklea lakini alikataa kutowa ufafanuzi zaidi.
Ban aongezea sauti yake
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo ametowa wito wa dharura kwa Korea Kaskazini kujiepusha na uchokozi zaidi kufuatia repoti kwamba inajiandaa kufyetuwa kombora jipya.Ban amesema mjini The Hague Uholanzi kwamba Jamhuri ya Kidemokrasi ya Watu Korea haiwezi kuendelea kufanya namna inavyofanya kulumbana na kupinga mamlaka ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Kimataifa kwa jumla. Akizungunmza na waandishi wa habari Ban amesema hilo ni "ombi la dharura na la uadilifu kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na kutoka kwake binafsi."
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/Reuters/
Mhariri: Mohammed Khelef