Korea Kaskazini: Mazungumzo na Rais Trump 'hayawezekani'
10 Agosti 2017Umoja wa Ulaya umepanua orodha ya watu na mashirika ambayo yamejumuishwa kwenye vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini. Haya yanajiri wakati vita vikali vya maneno kati ya Washington na Pyongyang vikizidi kuzusha taharuki, huku Korea Kaskazini ikisema hakuna haja ya kuzungumza na Rais Trump.
Siku moja tu baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutishia Pyongyang kuwa itakumbwa na moto na ghadhabu kubwa ambayo dunia haijawahi kushuhudia, kufuatia mipango yake ya makombora, Korea Kaskazini imejibu kwa kusema hakuna haja ya mazungumzo na Rais Donald Trump.
Korea Kaskazini: 'Mazungumzo hayawezekani'
Korea Kaskazini imeelezea mipango yake kabambe ya kushambulia kisiwa cha Marekani cha Guam kilichoko bahari Pasifiki katika siku chache zijazo. Kauli hiyo ya mkuu wa mikakati jeshini, Kamanda Kim Rak Gyom, ilitangazwa na runinga inayomilikiwa na serikali ya nchi hiyo na ilisema: "Mazungumzo muafaka hayawezekani na mtu kama huyo asiyefikiria na kutumia nguvu dhidi yake ndiyo itamfaa. Huo ndio uamuzi wa maafisa wa mkakati wa jeshi ya KPA"
Kisiwa hicho kina kambi ya jeshi la Marekani yenye ndege za kivita na wanajeshi 7000. Athari ya taharuki ambayo imesababishwa na vita vya maneno na vitisho vya kushambuliana kati ya Marekani na Korea Kaskazini zimesababisha kuporomoka kwa baadhi ya masoko ya fedha yakiwemo ya Ulaya na Marekani.
Vikwazo zaidi kwa baadhi ya Wakorea kaskazini
Wakati hayo yakijiri, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zimesema kupitia taarifa rasmi kuwa zinaongeza watu 9 pamoja na mashirika 4 kwenye orodha ya waliowekewa vikwazo kutoka Korea Kaskazini likiwemo benki linalomilikiwa na Korea Kaskazini FTB. Uamuzi unaofikisha idadi jumla ya waliowekewa vikwazo nchini humo kufikia 103 na mashirika 57.
Kuongezwa kwa orodha hiyo kunajiri wiki moja baada ya UMoja wa Mataifa kuongeza vikwazo vikali vya kiuchumi dhidi ya Korea Kaskazini. Vikwazo vilivyofuatia hatua ya Korea Kaskazini kufanya jaribio la kombora la masafa marefu linaloweza kufika Marekani.
Umoja Wa Ulaya wenye nchi wanachama 28 za bara la Ulaya zimeweka vikwazo vya usafiri na vikwazo dhidi ya mali ya Korea Kaskazini, kufuatia hatua yake ya ukiukwaji wa mara kwa mara wa maafikiano ya Umoja wa Mataifa kuhusu mipango yake ya makombora.
Baraza la Umoja wa Ulaya limesema litafanya juhudi kutekeleza maafikiano ya Umoja wa Mataifa ikiwemo juhudi za kudhibiti mapato ambayo raia wa Korea Kaskazini wanaofanya kazi ughaibuni hutuma katika nchi yao.
Mwandishi: John Juma/AFPE/DPAE
Mhariri: Iddi Ssessanga