Korea kaskazini yabanwa na vikwazo vikali zaidi
6 Agosti 2017Hatua hizo ni za kwanza za aina hiyo zilizowekwa dhidi ya Korea kaskazini tangu rais Donald Trump kuingia madarakani na kuonesha kuwapo tayari kwa China kuiadhibu nchi hiyo ambayo ni mshirika wake.
Azimio hilo linaweka marufuku kamili katika mauzo ya makaa ya mawe, chuma na mchanga wa chuma, risasi pamoja na samaki na vyakula vinavyotokana na bahari katika taifa hilo lenye matatizo makubwa ya fedha za kigeni, na kuinyima korea kaskazini theluthi ya mapato yake ya nje yanayokadiriwa kufikia dola bilioni 3 kwa mwaka.
Balozi wa Marekani Nikki Haley amesema hatua hizo ngumu zimeleta athabu hiyo iliyowekwa dhidi ya Korea kaskazini kutokana na majaribio yake ya makombora, "katika kiwango kipya kabisa " na kwamba baraza limemuweka kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong-Un katika uangalizi.
"Hizi ni hatua kali kabisa za vikwazo dhidi ya nchi yoyote ile katika kizazi kimoja," haley ameliambia baraza la Usalama baada ya kura hiyo.
"Vikwazo hivi vitaingia kwa kina na kwa kufanya hivyo, vitatoa kwa uongozi wa Korea kaskazini ladha ya kujidhalilisha waliochagua kuwaletea wananchi wa Korea kaskazini."
Azimio hilo pia linaizuia Korea kaskazini kuongeza idadi ya wafanyakazi inaotuma nje ya nchi ambao kipato chao ni chanzo kingine cha mapato ya utawala huo wa Kim.
Uwekezaji utaathirika
Pia linazuia njia zote mpya za pamoja na Korea kaskazini , na kupiga marufuku uwekezaji mpya katika makampuni ya pamoja na kuongeza maafisa tisa wa Korea kaskazini pamoja na mashirika manne ikiwa ni pamoja na benki kuu ya fedha za kigeni ya Korea kaskazini katika orodha ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa.
iwapo hatua hizo zitatekelezwa kikamilifu , zitakaza kitanzi cha uchumi wa Korea kaskazini wakati nchi hiyo ikijaribu kuendeleza mipango yake ya makombora na nyuklia.
Trump amesifu kura hiyo kwa kauli moja katika baraza la usalama la Umoja wa mataifa, akisema vikwazo hivyo vitakuwa na "athari kubwa ya kiuchumi!"
Ni "vikwazo vikubwa vya uchumi dhidi ya Korea kaskazini. Zaidi ya bilioni moja ya dola katika gharama kwa Korea ," kiongozi huyo wa Marekani ameandika katika ukurasa wa twita.
Marekani imeingia katika majadiliano na China mwezi mmoja uliopita kuhusiana na azimio hilo jipya baada ya Pyongyang kufanya majaribio yake ya kwanza ya makombora yanayoweza kuvuka mabara Julai 4 ambayo yalifuatiwa na jaribio la pili Julai 28.
Lakini hatua hiyo haitoi nafasi ya kupunguzwa upelekaji wa mafuta kwa Korea kaskazini kama ilivyopendekezwa hapo kabla na Marekani , hatua ambayo ingetoa pigo kubwa kwa uchumi wa nchi hiyo.
Hatua hizo mpya za ni kundi la saba la vikwazo vya Umoja wa Mataifa vilivyowekewa Korea kaskazini tangu ilipoanza kufanya majaribio ya kinyuklia mwaka 2006.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Sudi Mnette