Korea kaskazini yaendeleza vitisho
3 Aprili 2013Wasiwasi huo unakuja baada ya Korea Kaskazini kufunga mipaka yake ya kijeshi iliyopo umbali wa kilomita 11 upande wa Kaskazini, na kuzuia zaidi ya Wafanyakazi 861 wa Korea Kusini na wafanyakazi 53,000 wa Korea Kaskazini waliokuwa wanafanya kazi katika eneo la viwanda la Kaesong.
Kufuatia hali hiyo waziri wa ulinzi wa Korea Kusini, ametishia kuwa serikali yake itafanya kila liwezekanalo hata kama ni kutumia jeshi ili kulinda usalama wa raia wa Korea Kusini waliokuwa wakifanya kazi katika eneo hilo ambalo linatumiwa na Korea mbili.
Meneja wa moja ya viwanda katika eneo hilo, Lee Jae-Young, akiongea na Shirika la habari la AFP amesema, hatua hiyo imeathiri mzunguko wa biashara na uzalishaji baada ya malighafi nyingi za viwanda hivyo zinazosafirishwa kwa meli kwenda eneo la Kaesong kwa ajili ya uzalishaji, kukwama.
Jamii ya Kimataifa yatoa maoni
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amezitaka pande mbili kuacha uchokozi na kukaa pamoja huku Westerwelle akiikosoa vibaya Korea Kaskazini kwa kutangaza pia kuendelea kutengeneza silaha za nyuklia, na kuwataka wasafiri Korea Kusini kutoingia Korea Kaskazini kwa sasa.
Kwa upande wake naibu Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Igor Morgulov, amesema kuwa kuna haja ya kuchukua tahadhari kwani kosa dogo la kibinadamu, linaweza kusababisha vita ambavyo havitaweza kusimamishwa, na kuwa hatua ya Korea Kaskazini si tu itatia dosari uhusiano wa kidiplomasia kati ya Korea mbili, bali utachafua sura ya Korea Kaskazini katika jamii ya kimataifa.
Ufaransa nayo pia imeitaka China ambayo ina nguvu ya kuishawishi Korea Kaskazini, iingilie kati mgogoro wa kijeshi unaotokota katika rasi ya Korea.
China ambayo imekuwa na misimamo ya kindumakuwili ambayo ilikuwa rafiki wa karibu wa Korea Kaskazini kwa miongo kadhaa na mshirika wa kibiashara, imefungua kinywa na kuitaka Korea Kaskazini kumaliza mgogoro uliopo Rasi ya Korea.
Uchokozi huo ulianza kushuhudiwa katika rasi ya Korea tokea Korea Kaskazini ilipofanya jaribio lake la mwanzo mwezi Desemba mwaka jana la kurusha kombora la masafa marefu na kufanya jaribio lake la tatu la Nyuklia mwezi Februari mwaka huu, matukio ambayo yalisababisha iwekewe vikwazo na Umoja wa mataifa.
Mwandisahi: Hashim Gulana/AP/AFP/DPAA
Mhariri: Josephat Charo