Korea Kaskazini yafanya majaribio ya makombora ya kimkakati
13 Machi 2023
Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini KCNA limeripoti mapema leo Jumatatu kuwa manowari hiyo ilifyatua makombora hayo siku ya Jumapili karibu na mji wa pwani ya mashariki wa Sinpo na kwamba majaribio hayo yamefanikiwa, kwani makombora hayo yalipiga sehemu zilizokusudiwa ambazo hazikubainishwa katika pwani ya mashariki ya rasi ya Korea.
Shirika la habari la Yonhap limesema jeshi la Korea Kusini limebaini kitendo cha kurushwa kwa kombora moja ambalo halijafahamika vyema, bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.
Majaribio hayo ya Korea Kaskazini yanajiri saa chache kabla ya Korea Kusini na Marekani kuanza luteka kubwa zaidi ya kijeshi katika kipindi cha miaka mitano. Pyongyang ambayo inamiliki silaha za nyuklia imekuwa ikionya kwamba mazoezi kama hayo yanaweza kuchukuliwa kama "tangazo la wazi la vita".
Ripoti ya KCNA imebaini kuwa jaribio hilo linadhihirisha "msimamo thabiti" wa Korea Kaskazini wa kukabiliana na azma ya wale iliyowaita "mabeberu wa Marekani na vibaraka wa Korea Kusini."
Soma pia:Marekani na Korea Kusini kufanya luteka
Wizara ya mambo ya nje ya Korea Kaskazini imesema katika taarifa nyingine kuwa Marekani "inaanda njama" ya kuitisha mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu katika taifa hilo la kikomunisti lililojitenga, ili kwenda sambamba na luteka hiyo ya pamoja. Hata hivyo Korea Kaskazini inasema huo ni ulaghai na unadhihirisha sera ya chuki ya Marekani dhidi yake.
Baadhi ya raia nchini Korea Kusini waliandamana siku ya Jumamosi karibu na Ofisi ya Rais mjini Seoul ili kupinga luteka hiyo. Mmoja wa waandamanaji hao alisema:
"Nadhani kwamba kuendelea kufanya mazoezi ya kijeshi kunaweza kuwa kitendo cha uchochezi kwa upande mwingine. Hii inaweza hatimaye kugeuka kuwa mzozo."
Uhusiano ulioimarika kati ya washirika hao wawili
Washington na Seoul zimeongeza ushirikiano wa kijeshi katika masuala ya ulinzi ili kukabiliana na vitisho vya nyuklia vinavyoongezeka kutoka Korea Kaskazini, ambayo katika miezi ya hivi karibuni, imekuwa ikifanya majaribio zaidi ya silaha ziliyopigwa marufuku.
Katika hali isiyo ya kawaida, jeshi la Seoul mwezi huu lilibaini kuwa, kwa ushirikiano na vikosi maalum vya Washington vilikuwa vikifanya mazoezi ya kijeshi yaliyopewa jina "Teak Knife", ambayo yanahusisha kufanya majaribio ya mashambulizi yenye usahihi kwenye vituo muhimu nchini Korea Kaskazini.
Soma pia: Kim aamuru uimarishwaji wa mazoezi ya kijeshi
Mazoezi kama hayo yameikasirisha Pyongyang ambayo inayachukulia kama mazoezi ya uvamizi, na kusisitiza kuwa mipango yake ya silaha za nyuklia na makombora ni ya kujilinda.
Mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Marekani na Korea Kusini, yanayoitwa "Ngao ya Uhuru", yamepangwa kufanyika kwa angalau siku 10 kuanzia leo Jumatatu na yatazingatia kile kinachoitwa "kubadilika kwa mazingira ya usalama" kutokana na uchokozi unaoongezeka wa Korea Kaskazini.