1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yafanyia majaribio makombora manane

5 Juni 2022

Jeshi la Korea Kusini limesema Korea Kaskazini leo Jumapili imefyatua makombora manane ya masafa mafupi kuelekea pwani yake ya mashariki.

Raketensystem M270
Picha: South Korean Defense Ministry/Getty Images

Korea Kaskazini inafanya jaribio hilo siku moja baada ya Korea Kusini na Marekani kukamilisha luteka ya pamoja ya kwanza ya kijeshi iliyohusisha ndege za kijeshi za Marekani katika kipindi cha zaidi ya miaka minne.

Muungano wa wakuu wa utumishi wa jeshi nchini Korea Kusini umesema jeshi lao limegundua makombora manane yaliyofyatuliwa kutoka eneo la Sunan nchini Korea Kaskazini kuelekea Bahari ya Mashariki. Kulingana na taarifa yao, zoezi hilo limefanyika kwa dakika 30 mapema leo Jumapili.

Korea Kaskazini inafanya jaribio hili baada ya Marekani na Korea Kusini kukamilisha luteka kubwa ya kijeshi iliyodumu kwa siku tatu. Luteka hii ya pamoja ilikuwa ni ya kwanza tangu rais mpya wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol aingie mamlakani mwezi uliopita na ya kwanza inayohusisha ndege za kijeshi tangu Novemba 2017.

Soma Zaidi: Marekani na Korea Kusini zatafakari kutanua Luteka za Kijeshi

Pyongyang ambayo imeendelea kuimarisha mara dufu hatua zake za kuimarisha mipango ya silaha licha ya kukabiliwa na vikwazo vikali vya kiuchumi, kwa muda mrefu imekuwa ikipinga luteka hizo za pamoja za kijeshi ikiziita kuwa ni mazoezi ya uvamizi.

Rais wa Korea Kusini Yoon Suku-yeol alipokutana na rais Joe Biden wa Marekani mwezi Mei.Picha: Song Kyung-Seok/REUTERS

Go Myong-hyuy, mtafiti kutoka taasisi ya masomo ya sera ya Asan ameliambia shirika la habari la AFP kwamba  jaribio hilo la Korea Kaskazini huenda ni jibu kwa luteka hiyo ya kijeshi.

Waziri wa ulinzi wa Japan Nobuo Kishi amesema hatua hiyo ya kufyatua makombora haitakiwi kuvumiliwa.

Mwezi uliopita, wakati wa mkutano wa kilele na rais Yoon wa Korea Kusini, rais Joe Biden wa Marekani aliahidi kupeleka "vifaa vya kimkakati" iwapo kutakuwa na umuhimu wa kufanya hivyo ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ulinzi.

Soma Zaidi: Kim Jong Un aombwa kuzungumza na mrithi wake Suk Yeol

Marekani na Korea Kusini kwa wiki kadhaa sasa wamekuwa wakionya kuhusu nia ya Korea Kaskazini kufanya jaribio la kombora la nyuklia la masafa marefu ambalo ni la saba.

Licha ya kuelemewa na mlipuko wa maambukizi ya virusi vya UVIKO-19 Korea Kaskazini imerejea kwenye ujenzi wa kinu cha nyuklia ambao ulisimama kwa muda mrefu, hii ikiwa ni kulingana na picha mpya za satelaiti.

Mashirika: RTRE/AFPE