Korea kaskazini yafyatua makombora mawili
13 Machi 2023Korea Kaskazini imefanya majaribio ya makombora mawili ya kimkakati yaliyorushwa jana Jumapili kutoka kwenye manowari yake na kuelekea katika mji wa pwani ya mashariki wa Sinpo.
Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini KCNA limeripoti mapema leo kuwa majaribio hayo yamefanikiwa, kwani makombora hayo yalipiga sehemu zilizokusudiwa na ambazo hazikubainishwa katika pwani ya mashariki ya rasi ya Korea.
Jeshi la Korea Kusini limebaini kitendo cha kurushwa kwa kombora moja ambalo halijafahamika vyema, bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.
Majaribio hayo ya Korea Kaskazini yanajiri saa chache kabla ya Korea Kusini na Marekani kuanza luteka kubwa zaidi ya kijeshi katika kipindi cha miaka mitano. Pyongyang ambayo inamiliki silaha za nyuklia imekuwa ikionya kwamba mazoezi kama hayo yanaweza kuchukuliwa kama "tangazo la wazi la vita".