Korea kaskazini yaharibu mtambo katika kinu cha Nuklia
27 Juni 2008Korea Kaskazini inaripotiwa kuharibu mtambo mmoja ulioko katika kinu cha Nuklia kama ishara ya nia yake ya kukomesha mchakato wa kutengeneza silaha za Atomik.
Mtambo ambao umeteketezwa ni dohani ya kupoza ilioko katika kinu cha Nuklia cha Yongbyon.Dohani hiyo ambayo ni mfano wa kinu kilichopinduka,ina urefu wa mita 20.
Shughuli za kuiteketeza dohani hiyo kwa kuilipua, zimefanyika Ijumaa mbele ya waandishi habari wa kimataifa, na taarifa hizo zimeripotiwa na kituo kimoja cha Televisheni cha Korea Kusini cha MDC.
Uteketezaji huo ni ishara ya kuwa utawala wa Korea Kaskazini umepania kuteketeza mpango wake wa silaha za nuklia.Alhamisi Pyongyang ilikabidhi nyaraka za mpango wake wa Nuklia kwa China.
Kufutia hatua hiyo rais George W Bush wa Marekani ameahidi kuiondolea vikwazo vya kiuchumi nchi hiyo na pia kuifuta kutoka orodha ya mataifa Marekani inayosema kuwa yanayosaidia ugaidi.
Kutokana na hilo Korea Kaskazini ikaamua kuteketeza dohani hiyo mbele ya kamera za kimataifa kama ishara yake ya nia njema.
Ulipuaji wa mtambo huo umekuja baada ya miezi 20 tu ambapo Pyongyang iliushtua ulimwengu kwa kufanya majaribio ya kulilipua bomu la Nuklia.Shughuli hiyo ilifanyika chini ya ardhi.
Mbali na rais Bush kukaribisha hatua ya Korea Kaskazini kutoa mpango wake wa Nuklia,mataifa mengine pia yaliikaribisha hatua hiyo.
Mawaziri wa mashauri ya kigeni kutoka mataifa tajiri duniani yanayoitwa kama G8, nayo pia yalikaribisha hatua hiyo.Hata hivyo wameonya kuwa ni baado mapema kwa Korea Kaskazini kujiunga tena na jamii ya kimataifa.
Aidha wametilia mkazo azma yao ya kupata mafanikio katika juhudi zao za kuona kama rasi ya Korea haina silaha za Nukila.
Wameihimiza Korea ya kaskazini kuteketeza silaha zake za Nuklia na pia kuachana na mipango yake ya sasa ya Nuklia mkiwemo na makombora ya masafa marefu.
Mbali na kusema kuwa hatua ya Pyongyang ya kutoa makaratasi ya mpango wake kuhusu Nuklia ni hatua moja muhimu,lakini pia wamesisitiza kuwa ni muhimu kuchunguza kwa kina mpango huo.
Aidha wameihimiza Korea hiyo kuchukua hatua madhubuti kushughulikia masuala kama vile usalama,haki za binadamu na pia masuala ya mengine ya kibinadamu mkiwemo ufumbuzi wa suala la utekaji.
Na ingawa Rais Bush amefurahishwa na hatua ya sasa ya Korea kaskazini ,na kuahidi kufanya alivyoahidi lakini pia ameionya kuwa ni lazima Pyongyang ifichue na iachane na mipango yake yote ya Nuklia la sivyo itakabiliwa na hatua mpya.
Hatua ya jana ya Korea ya Kaskazini ya kutoa makaratasi ya mpango wake wa Nuklia kwa China,imechelewa.Ilikuwa ifanye hivyo miezi sita iliopita.