1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yajitayarisha kurusha kombora la masafa marefu

Josephat Nyiro Charo26 Machi 2009

Marekani Imetoa onyo kali kwa Pyong Yang ikisema hatua yake ya kurusha kombora la masafa marefu, itaangaliwa kama ni ya uchokozi.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, hillary Clinton akionya Korea Kaskazini dhidi ya kufyatua kombora la masafa marefu.Picha: picture alliance / landov


Marekani tayari imepeleka manowari mbili za kivita, katika pwani ya Japan, kujiweka tayari kwa lolote huku Korea Kaskazini ikijitayarisha kurusha kombora lake la masafa marefu katika kipindi cha siku tano zijaazo.

Hatua ya Pyong Yang ya kurusha kombora la masafa marefu, inakuwa changamoto na kero la kwanza kubwa kwa utawala mchanga wa Rais Barack Obama. Ingawa PyongYang ilitangaza inanuia kutupa satelite ya mawasiliano kati ya Aprili 4 na 8, Marekani na washirika wake wa bara Asia wanasema ishara zote zinaashiria utawala wa Kim jong IL unakusudia kutupa kombora la masafa marefu litakalofika katika jimbo la Alaska, lililoko Kaskazini mwa Marekani.

Mataifa washirika wakuu wa Marekani, bara Asia wamesema Korea Kaskazini, inahatarisha usalama wa eneo zima la kaskazini mwa bara la Asia.


Ari ya Korea Kaskazini kujenga zana za kinuklia daima ndio imekuwa chanzo cha mgogoro kati yake na Washington. Mapema jana maafisa wa Marekani walisema wamethibitisha kuwa Pyong Yang tayari imeshaweka kombora lake katika jukwa tayari kufyatua.


Mwanadiplomasia mkuu wa Marekani, waziri wa mambo ya nje Hillary Clinton aliye ziarani Mexico, alitoa onyo kali kwa Pyong Yang akisema hatua yake itasambaratisha mazungumzo yanayojumuisha nchi sita kujaribu kuishawishi Pyong Yang kuachana na mpango wake wa kinuklia.


'' hatua hii ni ya uchokozi......na hatutakaa kimya tutachukua hatua zipasavyo.'' alisema Clinton akirejelea onyo lake la awali kuwa watawasilisha swala hili mbele ya baraza la usalama la umoja wa mataifa, ili Pyong Yang ichukuliwe hatua zaidi.


Marekani haikuachia hapo. Tayari jeshi lake la majini, limetuma manawari mbili za kijeshi pwani ya Japan kujitayarisha kwa lolote. Televisheni moja mjini Seoul, ilitangaza Korea kusini pia huenda ikatuma meli za kivita, pwani ya Japan ingawa bado maafisa wa serikali hawajathibitisha taarifa hizi. Seoul kupitia wizara yake ya ulinzi ilitoa taarifa ikionya Korea Kaskazini isithubutu kufyatua kombora, kwani watakuwa wanakiuka kanuni za baraza la usalama wa umoja wa mataifa, na kuhatarisha usalama wa eneo zima la Korea.


Japan nayo pia haijakaa kimya, baraza la usalama la nchi hiyo litakutana wiki hii kujitayarisha kuangusha roketi yeyote itakayohatarisha nchi yake. Mwaka wa 1998 Tokyo ilishtushwa sana pale kombora la Korea Káskazini lilipopita katika anga yake.


Mbali na swala la usalama hatua hii ya Pyong Yang, ni kero pia kwa juhudi za kufufua uchumi katika eneo la Korea, hasa sasa wakati kuna mgogoro wa kiuchumi duniani.


Iwapo Pyong Yang itafaulu kufyatua kombora lake, huu utakuwa ushindi mkubwa kwa rais Kim Jong Il, katika siasa za Korea Kaskazini. Kim aliugua sana mwaka jana, hali yake ya kiafya ilieneza uvumi kote kuwa udhibiti wake madarakani ulikuwa unayumbayumba.



Munira Muhammad/ REUTERS

Mwandishi Saumu Mwasimba

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW