Korea Kaskazini yakubali mpango wake wa nyuklia ukaguliwe
1 Machi 2012Tangazo la makubaliano hayo, lililotolewa kwa wakati mmoja, siku ya Jumatano mjini Pyongyang na Washington na kufuatiwa na ahadi za msaada wa chakula kutoka Marekani, lilipokelewa kwa matumaini madogo na wachambuzi na wanadiplomasia wakibainisha kuwa jitihada za kumaliza mvutano katika eneo la Korea zimeshuhudia vikwazo vingi.
Lakini Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton, alisema hii ni hatua nzuri ya kwanza katika mwelekeo sahihi na kuongeza kuwa, nchi yake inaendelea kuguswa na shughuli nyingi zinazoendelea Korea Kaskazini.
Majaribio ya nyuklia kuahirishwa
Korea Kaskazini imesema itaahirisha majaribio ya nyuklia, makombora ya masafa marefu pamoja na kurutubisha madini ya uranium katika kituo cha Yongbyon, na pia imeahidi kuruhusu wakaguzi wa kimataifa wa shirika na kimataifa la nguvu za atomiki kukagua vituo vyake.
Lakini haikuweka wazi ni kwa umbali gani wakaguzi wataruhusiwa kufika na wala kama nchi hii itasitisha mpango wake wote. Hatua hiyo inakuja miezi miwili baada ya Kim Jong-un, kurithi uongozi wa taifa hilo kufuatia kufariki kwa baba yake mwishoni mwa mwaka jana.
China, ambayo ilikuwa mwenyeji wa mazungumzo yaliyofikia makubaliano hayo kati ya Marekani na Korea Kaskazini, imeeleza kufurahishwa kwake na hatua hii iliyofikiwa na kuahidi kuharakisha uanzishwaji wa majadiliano ya pande sita juu ya usitishaji wa mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.
Mlango mpya wa mazungumzo
Bruce Klingner, Afisa wa shirika la ujasusi la Marekani, CIA, na mataalamu wa masuala ya Korea kaskazini, amesema hatua iliyofikiwa na Marekani na Korea kaskazini inafungua milango kwa ajili ya mazungumzo ya muda mrefu.
"Siyo kwamba mazungumzo ya pande sita yataanza kesho, ila makubaliano haya ya mwanzo yanafungua milango kwa mazungumzo zaidi kati ya Marekani na Korea kaskazini kujaribu kufikia ajenda ya pamoja ambayo itawezesha kuanza upya kwa mazungumzo ya pande sita," alisema Klingner.
Mazungumzo hayo, ambayo yalivunjika kwa mara ya mwisho mwaka 2008, yanahusisha Korea Kaskazini, Korea Kusini, Marekani, China, Japan na Urusi. Korea Kaskazini iliwafukuza wakaguzi wa Umoja wa mataifa mwaka 2009.
Wachambuzi wamesema kuwa, huenda kifo cha Kiongozi wa taifa hilo, Kim Jong-il, kimechangia kubadilisha msimamo mkali wa utawala wa Pyongyang, ambao ulikataa makubaliao yaliyokuwa yamefikiwa huko nyuma.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/RTRE
Mhariri: Josephat Charo.