Korea Kaskazini yarusha kombora bahari ya Japan
5 Aprili 2017Wizara ya Usalama ya Korea Kusini imesema kombora hilo limerushwa kutoka umbali wa kilomita 60. Korea Kusini imesema, tukio hilo linatishia amani na utulivu duniani kote. Naye Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe amelaani vikali tukio hilo na kusema kuwa ni uchokozi mkubwa kutoka Korea Kaskazini.
"Ni uchokozi mbaya sana kwa usalama wetu wa nchi, na ni wazi kuwa unakiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hili haliwezi kustahmilika. Nitaitisha mkutano na Baraza la Usalama la Taifa mara moja," amesema Shinzo Abe.
Katika taarifa yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson amesema Marekani imeshasema vya kutosha juu ya Korea Kaskazini. Na sasa haina maneno tena.
Kufyatuliwa kwa kombora la masafa ya wastani la aina ya KN-15 kutachochea wasi wasi duniani kote kuhusu mpango wa silaha wa Korea Kaskazini.
Taifa hilo lina mpango wa kuunda kombora la masafa marefu lenye kichwa cha kinyuklia na ambalo litaweza kuruka hadi katika ardhi ya Marekani. Korea Kaskazini tayari imeshafanya majaribio matano ya silaha za kinyuklia, mawili kati yao yalifanywa mwaka jana.
Kombora lililorushwa hivi karibuni, limekuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutishia kuwa Marekani imejitayarisha peke yake bila ya msaada wa China kuizuia Korea Kaskazini kuendelea na mpango wake wa kinyuklia.
Trump na Xi kuijadili Korea Kaskazini
Victor Cha, Mshauri Mwandamizi na Mwenyekiti wa Korea, katika Kituo cha Mkakati na Mafunzo ya Kimataifa amesema kitisho cha Korea Kaskazini kitakuwa ni mada kuu katika mazungumzo kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Xi Jinping wa China, unaofanyika siku moja baada ya tukio hilo.
"Nadhani hali ni mbaya sana. Nadhani ni wazi kabisa kuwa Korea Kaskazini haipo tayari kurudi nyuma katika suala la kujaribu kuonyesha uwezo wake wa makombora ya masafa marefu, na kwamba inaweza kuifikia Marekani. Hii ni aina mpya ya kitisho kwa Marekani kutoka Korea Kaskazini, kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 50 au 60, tangu mwisho wa Vita vya Korea," amesema Victor Cha.
Mpango wa kinyuklia unaoshika kasi wa Korea Kaskazini unatarajiwa kuwa mada kuu katika mkutano wa viongozi hao wawili.
Trump atakuwa mwenyeji wa Xi katika mkutano huo utakao fanyika katika jimbo la Florida, ukiwa ni mkutano wao wa kwanza wa uso kwa uso. Utawala wa Trump umekuwa ukisisitiza kuwa China ndiyo inayoshika ufunguo wa kuizuia Korea Kaskazini na kwamba haifanji jitihada za kutosha kumdhibiti jirani yake.
Mwandishi: Yusra Buwayhid
Mhariri: Iddi Ssessanga