1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Korea Kaskazini yarusha kombora la kisasa zaidi la nyuklia

31 Oktoba 2024

Korea Kaskazini imesema kuwa imejaribisha moja ya makombora yake mapya zaidi yanayokusudiwa kuimarisha vizuwizi vyake vya nyuklia, likiwa jaribio la kwanza tangu taifa hilo lilipotuhumiwa kupeleka wanajeshi nchini Urusi.

Jaribio la kombora Korea Kaskazini
Watu wanatazama skrini ya televisheni inayoonyesha matangazo ya habari yenye picha za jaribio la kombora la Korea Kaskazini, katika kituo cha treni huko Seoul tarehe 31 Oktoba 2024.Picha: JUNG YEON-JE/AFP

Seoul ilitoa onyo siku moja kabla kwamba Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia ilikuwa inajiandaa kufanya jaribio la kombora jingine la masafa marefu (ICBM) au hata kufanya jaribio la nyuklia kabla ya uchaguzi wa Marekani wiki ijayo.

Jaribio hilo lilifanyika saa chache tu baada ya mawaziri wa ulinzi wa Marekani na Korea Kusini kuitaka Pyongyang kuondoa wanajeshi wake kutoka Urusi, wakionya kuwa wanajeshi wa Korea Kaskazini wakiwa katika sare za Urusi wanapelekwa kwa ajili ya hatua dhidi ya Ukraine.

Ukraine imeliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa zaidi ya maafisa 500 wa Korea Kaskazini, wakiwemo majenerali watatu, wametumwa kuiunga mkono Urusi katika vita vyake Ukraine, wakitarajiwa kuunganishwa na vikosi vya Urusi ili kuficha uwepo wao.

"Uamuzi wa awali hadi sasa ni kwamba (Pyongyang) huenda ilifanya jaribio la kombora jipya la masafa marefu linalotumia roketi thabiti," jeshi la Seoul limesema, likiongeza kuwa kombora hilo liliruka takriban kilomita 1,000 (maili 621) baada ya kurushwa kwa njia ya mwinuko - ikimaanisha juu, sio mbali.

Soma pia: Korea Kaskazini yajiandaa kufanya jaribio la nyuklia

Utengenezaji wa makombora ya kisasa yanayotumia roketi thabiti - ambayo yanaweza kuzinduliwa haraka na ni vigumu kuyagundua na kuyaharibu mapema - limekuwa lengo la muda mrefu kwa Kim.

Korea Kaskazini ilitetea jaribio hilo lililokiuka vikwazo, ikiliita "hatua sahihi ya kijeshi inayokidhi kikamilifu lengo la kuwajulisha wapinzani... kuhusu nia yetu ya kukabiliana nao," shirika rasmi la Habari la Korea Kaskazini lilimnukuu Kim akisema.

Ukraine yataja majenerali walioko na wanajeshi wa Korea Kaskazini nchini Urusi

Serikali ya Ukraine imetaja majenerali watatu wa Korea Kaskazini ambao inasema wanaandamana na maelfu ya wanajeshi wa Jeshi la Watu wa Korea waliopelekwa Urusi kusaidia vita vya Moscow dhidi ya Ukraine.

Katika taarifa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano, ujumbe wa Ukraine ulisema majenerali hao watatu ni miongoni mwa maafisa angalau 500 wa Korea Kaskazini waliotumwa Urusi.

Miongoni mwa Majenerali waliotaijwa ni Luteni Jenerali Kim Yong Bok, kiongozi wa vikosi maalum vya Korea Kaskazini, vinavyojumuisha Kikosi cha XI (Storm Corps), ambacho kimepelekwa Urusi kwa mujibu wa taarifa za kijasusi za Korea Kusini.

Rais Putin na Kim Jong Un walisaini makubaliano ya ushirikiano mnamo Juni 2024.Picha: Vladimir Smirnov/POOL/TASS/dpa/picture alliance

Kim ameonekana mara saba na kiongozi Kim Jong Un mwaka huu, ikiwemo wakati wa mazoezi ya vikosi maalum, hali inayoonseha umuhimu wa nafasi yake katika mkakati wa kijeshi wa Korea Kaskazini.

Maafisa wengine wakuu waliotambuliwa na Ukraine ni Luteni Jenerali Ri Chang Ho, Naibu Mnadhimu Mkuu wa Jeshi na mkuu wa Shirika la Ujasusi la Korea Kaskazini, pamoja na Meja Jenerali Sin Kum Cheol, Mkuu wa Kurugenzi ya Kazi za Kijeshi.

Wachambuzi wasema jaribio la kombora ni kufunika utumaji wanjeshi Urusi

Yang Moo-jin, rais wa Chuo cha Masomo ya Korea Kaskazini mjini Seoul, amesema jaribio la kombora la Korea Kaskazini linaonekana kuwa na kusudio la kuondoa nadharia kwenye ukosoaji wa kimataifa kuhusu hatua yake ya kutuma wanajeshi nchini Urusi.

Seoul imekuwa ikidai kwa muda mrefu kwamba Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia inatuma silaha kuisaidia Moscow katika vita vyake dhidi ya Kyiv, na inaeleza kuwa Pyongyang imeanza kupeleka wanajeshi kwa wingi kufuatia mkataba wa ushirikiano wa ulinzi uliosainiwa na Kim Jong Un na Rais wa Urusi Vladimir Putin mwezi Juni.

Soma pia: Korea Kaskazini yaikosoa Marekani kwa uchochezi Asia Pasifiki

Jaribio hilo lilifanyika saa cheche tu baada ya wakuu wa majeshi ya Marekani na Korea Kusini kuitaka Pyongyang kuondoa wanajeshi wake Urusi, na kuonya kuwa wanajeshi wa Korea Kaskazini katika sare za Urusi walikuwa wanapelekwa yumkini kushiriki vita dhidi ya Ukraine.

''Licha ya maonyo yetu ya mara kwa mara ya kijeshi, Korea Kaskazini inaendelea na uchokozi wake kinyume cha sheria. Tunarudia onyo letu kali kwamba Korea Kaskazini itabeba jukumu kamili kwa madhara yoyote yatakayojitokeza, alisema Meja Jenerali Ahn Chan Myong, Mkurugenzi wa Operesheni wa Jeshi la Korea Kusini.

Korea Kusini imeonya kuwa Urusi huenda inatoa teknolojia mpya kwa Korea Kaskazini kama malipo ya silaha na wanajeshi kusaidia vita dhidi ya Ukraine.

Nchini hiyo ambayo ni muuzaji mkubwa wa silaha, imesema inachunguza uwezekano wa kutuma silaha moja kwa moja kwa Ukraine, hatua ambayo awali iliiepuka kutokana na sera yake ya ndani inayozuia kutuma silaha kwenye maeneo yenye migogoro.

Pyongyang imezuiwa kufanya majaribio ya kutumia teknolojia ya masafa marefu kupitia vikwazo kadhaa vya Umoja wa Mataifa, lakini kiongozi wake Kim ameongeza majaribio ya makombora mwaka huu, huku wataalam wakionya kuwa huenda anajaribu silaha kabla ya kuipatia Urusi.

Gwaride la kijeshi la Korea Kaskazini mjini PyongyangPicha: picture-alliance/Newscom

Urusi: Ikiwa Magharibi wanasaidia Ukraine, kwanini Korea Kaskazini isiweze kutusaidia?

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Balozi wa Urusi Vassily Nebenzia, alihoji kwa nini washirika wake kama Korea Kaskazini hawawezi kuisaidia Moscow katika vita vyake dhidi ya Ukraine, wakati kuna madai yaliotapakaa ya mataifa ya Magharibi kuisaidia Ukraine!

Nebenzia alikabiliwa na hoja kali katika mkutano wa Baraza la Usalama kutoka kwa Marekani, Uingereza, Korea Kusini, Ukraine na wengine, ambao wote waliishutumu Urusi kwa kukiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa na Katiba ya Umoja wa Mataifa kwa kupeleka wanajeshi wa Korea Kaskazini (DPRK) kusaidia Moscow.

"Kusaidia kitendo cha uchokozi, ambacho kinakiuka kabisa misingi ya Katiba ya Umoja wa Mataifa, ni kinyume cha sheria," Balozi wa Korea Kusini katika Umoja wa Mataifa Joonkook Hwang alisema. "Shughuli zozote zinazohusiana na utumaji wa wanajeshi wa DPRK kwenda Urusi ni ukiukaji wazi wa maazimio kadhaa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa."

Soma pia: NATO: Wanajeshi wa Korea Kaskazini tayari wako Urusi

Nebenzia alisema kuwa ushirikiano wa kijeshi wa Urusi na Korea Kaskazini haukiuki sheria za kimataifa. Urusi haijakanusha ushiriki wa wanajeshi wa Korea Kaskazini katika vita inavyoendesha nchini Ukraine tangu Februari 2022.

"Nebenzia alisema, 'Hata kama kila kitu kinachosemwa kuhusu ushirikiano kati ya Urusi na Korea Kaskazini na wenzetu wa Magharibi ni kweli, kwa nini Marekani na washirika wake wanajaribu kulazimisha kila mtu kukubali mantiki potofu kwamba wao wana haki ya kusaidia utawala wa Zelenskiy ... lakini washirika wa Urusi hawana haki ya kufanya jambo kama hilo."

Ukraine na washirika wazikabili Urusi na Korea Kaskazini

Balozi wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa, Sergiy Kyslytsya, alijibu: "Hakuna nchi inayotoa msaada kwa Ukraine ambayo ipo chini ya vikwazo vya Baraza la Usalama."

"Kupokea msaada kutoka Korea Kaskazini iliyo chini ya vikwazo kamili ni ukiukaji wa wazi wa Katiba ya Umoja wa Mataifa," aliongeza. "Kutuma wanajeshi wa DPRK kuunga mkono vita vya uchokozi vya Urusi dhidi ya Ukraine ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa."

Korea Kaskazini imekuwa chini ya vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tangu 2006, na vikwazo hivyo vimeimarishwa hatua kwa hatua kwa miaka ili kukomesha uendelezaji wa silaha za nyuklia na makombora ya masafa marefu ya Pyongyang.

Maswahiba, Kim Jong Un na Vladmir PutinPicha: Yonhap/picture alliance

Korea Kaskazini haijakiri kupeleka wanajeshi Urusi, lakini ilisema kuwa hatua yoyote kama hiyo ingekuwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Balozi wa Korea Kaskazini katika Umoja wa Mataifa, Song Kim, aliliambia Baraza: "Ikiwa uhuru na maslahi ya usalama ya Urusi yatakuwa hatarini kutokana na majaribio hatari ya Marekani na Magharibi, na ikiamuliwa kuwa tunapaswa kujibu kwa hatua fulani, tutafanya uamuzi unaohitajika."

"Pyongyang na Moscow zinaendelea kuwa na mawasiliano ya karibu kuhusu usalama wa pamoja na maendeleo ya hali ilivyo," alisema.

Hata hivyo, Naibu Balozi wa Marekani Robert Wood alimwonya kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un: "Iwapo wanajeshi wa DPRK wataingia Ukraine kuisaidia Urusi, hakika watarudi kwenye mifuko ya kuhifadhia maiti. Kwa hivyo, ningemshauri Mwenyekiti Kim kufikiria mara mbili kabla ya kujiingiza katika tabia kama hiyo isiyo ya busara na hatari."

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW