1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yasherehekea miaka 70 tangu kuasisiwa

Caro Robi
9 Septemba 2018

Korea Kaskazini imeadhimisha miaka 70 ya kumbukumbu ya kuasisiwa kwa taifa hilo, tofauti na ilivyo kawaida, safari hii kukiwa hakuna maonyesho ya makombora ya masafa marefu kwenye gwaride la kijeshi.

Nordkorea Militärparade zum 70. Jahrestag der Staatsgründung
Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Cheung

Watazamaji wengi walishuhudia gwaride wakati makumi kwa maelfu ya wanajeshi walioambatana na vifaru walipopita na kutoa heshima mbele ya jukwaa, alilokuwa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.

Tofauti na miaka iliyopita, hakukua na  majaribio ya nyuklia kuadhimisha siku hiyo, kama ilivyofanyika kila mwaka katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Hatua hiyo, inaashiria azma ya Kim aliyoielezea awali ya kuondoa silaha za nyuklia kwenye rasi ya Korea, pamoja na mikutano yake ya hivi karibuni na Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in mkutano wa kilele na rais Donald Trump wa Marekani pamoja na Rais wa China Xi Jinping.

Korea Kaskazini yachagua maua badala ya makombora

Kim alionekana akicheka na kushikana mikono na mjumbe maalumu wa China alipohudhuria sherehe hizo za miaka 70 tangu kuundwa kwa taifa la Korea Kaskazini yaliyofanyika katika uwanja wa Kim II Sung. Kiongozi huyo aliwapungia mkono umma kabla ya kuondoka bila ya kuwahutubia.

Umati wa Umma ukipeperusha maua na bendera katika sherehe za miaka 70Picha: Getty Images/AFP/E. Jones

Korea Kaskazini imewaalika wanahabari wengi wa kigeni kuangazia sherehe hizo na hafla nyingine zitakazofuata za kusherehekea miaka 70 ya taifa hilo.

Umati wa watu waliohudhuria sherehe hizo walipeperusha bendera na kubeba maua. Sherehe hizo zimempa fursa Kim kuonesha ufanisi wa kijeshi, maendeleo ya kitaifa na ushirikiano na jumuiya ya kimataifa licha ya kuongezka mashaka kuhusu kujitolea kwake kuachana kabisa na mpango wa kutengeza silaha za nyuklia.

Kauli mbiu ya sherehe za mwaka huu ni maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha umoja na ushirikiano katika rasi ya Korea ambayo imegawika tangu kumalizika vita vya pili vikuu vya dunia.

Kim Jong Un na Rais wa Korea Kusini Moon Jae In watakutana Pyongyang kati ya tarehe 18 hadi 20 mwezi huu, hiyo ikiwa mara ya tatu kwa viongozi hao wa Korea mbili kukutana mwaka huu kujadili hatua zitakazochukuliwa kuhakikisha silaha za kinyuklia zinaangamizwa katika rasi ya Korea.

Kulingana na maafisa wa Korea Kusini, licha ya kuwa hakuna hatua zilizopigwa baada ya mazungumzo kati ya Kim na Trump, lakini kiongozi wa Korea Kaskazini ana nia ya kuondoa kabisa silaha za nyuklia katika kipindi cha muhula wa kwanza wa Rais Trump madarakani.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/AP

Mhariri: Lilian Mtono

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW