Korea Kaskazini yatakiwa kuachana na mpango wa nyuklia
5 Januari 2011Marekani na Korea Kusini zimekubaliana kuwa Korea Kaskazini lazima ichukue hatua madhubuti kuelekea kuachana na mpango wake wa kinyuklia kabla mazungumzo ya kimataifa ya pande sita kuhusu mpango huo hayajaanza tena.
Hayo yameelezwa mjini Seoul, Korea Kusini katika vyombo vya habari vya taifa na afisa wa ngazi ya juu wa Korea Kusini, baada ya mjumbe wa Marekani huko Korea Kaskazini, Stephen Bosworth kukutana na mjumbe wa masuala ya kinyuklia wa Korea Kusini, Wi Sung Lac. Akinukuliwa na shirika la habari la Yonhap, afisa huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema kuwa wanadiplomasia hao wawili walikubaliana zaidi ya kitu chochote kile kuwa Korea Kaskazini lazima ionyeshe kwa dhati kuhusu kuachana na mpango wake wa kinyuklia.
Mazungumzo hayo ya pande sita ya kuhusu mpango wa kinyuklia wa Korea Kaskazini yamekwama tangu mwaka 2008. Hata hivyo, nchi hiyo sasa imeonyesha nia ya kurejea katika meza ya mazungumzo, ingawa haijachukua hatua zozote zile kuhusu kutekeleza yale inayoyaahidi. Marekani na Korea Kusini pia zimeitaka jumuiya ya kimataifa kulizungumzia suala hilo kwa ukali zaidi, kutokana na Korea Kaskazini hivi karibuni kuimarisha zaidi urutubishaji wa madini yake ya uranium na kwamba mpango huo umekiuka mfululizo wa maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Wasiwasi umeongezeka zaidi katika wiki za hivi karibuni huku kukiwa na mivutano zaidi kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini, ikiwemo pia suala la kugundulika kwa kinu cha zamani cha kurutubisha madini ya uranium ambacho kilikuwa hakijulikani katika eneo la kinyuklia la Yongbyon, Korea Kaskazini. Afisa huyo amesema kuwa Bosworth na Wi leo pia wamekubaliana kuwa uhusiano kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini lazima uimarishwe kabla mazungumzo hayo hayajaanza tena.
Katika ujumbe wake wa mwaka mpya, Jumamosi iliyopita Korea Kaskazini ilisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wake na jirani yake hatua inayoonyesha nia ya Korea Kaskazini kurejea katika mazungumzo ya pande sita yanayozijumuisha Korea zote mbili, Marekani, China, Japan na Urusi. Aidha, baadae leo, Bwana Bosworth alitarajiwa kwenda China na kisha Japan hapo kesho. China ambayo ni mshirika mkubwa pekee wa Korea Kaskazini, imetaka mazungumzo hayo ya pande sita yaanze tena, lakini hadi sasa nchi hiyo imekataa shinikizo la kimataifa la kuikemea na kuishawishi Korea Kaskazini kuachana na tabia yake ya uchokozi.
Aidha, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani wiki iliyopita ilitangaza kuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates atasafiri kwenda Asia Mashariki tarehe 9 ya mwezi huu wa Januari na kuzuru China, Japan na Korea Kusini. Rais Barack Obama wa Marekani, anatarajiwa kukutana na mwenzake wa China, Hu Jintao tarehe 19 ya mwezi huu wa Januari, mjini Washington na ajenda kubwa ya mkutano huo inatarajiwa kuwa hali jumla katika rasi ya Korea.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE)
Mhariri:Josephat Charo