1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yatakiwa kuzingatia makubaliano

Angela Mdungu
14 Juni 2020

Korea Kusini imefanya mkutano wa dharura wa usalama leo 14.06.2020 na kuihimiza Korea Kaskazini kuzingatia makubaliano saa kadhaa baada ya Korea Kaskazini kutishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Korea Kusini.

Kim Jong Un und Schwester Kim Yo Jong
Picha: picture-alliance/dpa/Korea Summit Press Pool/Kyodo

Wito huo umetolewa na Korea Kusini huku kukiwa na wasiwasi kuwa huenda Korea ya Kaskazini ikaanza kutumia njia ya uchochezi kuimarisha umoja wake wa ndani na kupinga makubaliano huku mazungumzo ya nyuklia kati ya taifa hilo na Marekani yakikwama.

Kwa mujibu wa taarifa ya ikulu ya Korea Kusini, mkurugenzi wa usalama wa nchi hiyo Chung Eui-yong, aliandaa mkutano wa dharura kwa njia ya video na waziri wa usalama na majenerali wa jeshi kuzungumzia hali ya sasa katika rasi ya Korea na hatua ambazo huenda zikachukuliwa na serikali.

Waangalizi wanasema Kaskazini Korea inahitaji kwa haraka kulegezewa vikwazo, wakati ikikabiliana na janga la corona na vikwazo iliyowekewa na Marekani.Wizara ya umoja ya Korea Kusini inayoshughulikia mahusiano na Korea Kaskazini imesema kuwa nchi hizo mbili zinapaswa kufanya juhudi za kuzingatia makubaliano yaliofanywa. Wizara ya ulinzi nayo ilisema inalifuatilia jeshi la Korea Kaskazini kwa karibu na itaendelea kuliweka jeshi lake katika hali thabiti na ya utayari.

Jana jumamosi, dada wa kiongozi wa Korea Kaskazini mwenye ushawishi mkubwa Kim Yo Jong aliionya Seoul kuwa muda si mrefu itashuhudia janga katika ofisi ya uhusiano baina ya nchi hizo mbili iliyoko Korea Kaskazini ikiwa imebomolewa.

Kim Yo Jong atishia kuliruhusu Jeshi kulipa kisasi

Jong, alisema pia ataliachia jeshi la nchi yake haki ya kuchukua hatua inayofuata ya kulipa kisasi kwa Korea kusini na alitishia pia kuyafuta makubaliano ya mwaka 2019 ambayo yalisababisha mataifa hayo ya Korea kusimamisha ufyatulianaji risasi, kuondoa mitego ya mabomu ya ardhini na vituo vya ulinzi katika maeneo ya mzozo.

Korea Kaskazini ilihusisha mfululizo wa vitisho vyake na kushindwa kwa Korea Kusini kuwazuia wanaharakati kutopeperusha karatasi za propaganda katika eneo la mpaka. Hata hivyo baadhi ya wataalamu wanasema Korea kaskazini imejikuta katika mkanganyiko kwamba Kusini haijafanya juhudi za kutosha katika kuifufua miradi mikubwa ya pamoja ya kiuchumi pamoja na kutopiga hatua katika mazungumzo yake ya nyuklia na Marekani.

Picha ya makombora ya Korea Kaskazini kama ilivyotolewa na shirika la habari lanchi hiyoPicha: picture-alliance/dpaEPK/KCNA

Mazungumzo hayo yamepiga hatua kidogo tangu mkutano wa pili kati ya Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na Rais wa Marekani Donald Trump ulipokwama mwanzoni mwa mwaka 2019 kutokana na mzozo juu ya kiasi kinachopaswa kuondolewa ili Kim aachane na mpango wake wa nyuklia. Baadaye Kim aliapa kuongeza silaha zake za nyukli, na kuanzisha silaha mpya za kimkakati na kuachana na Marekani inayoongozwa na vikwazo.

Baadhi ya waangalizi katika mgogoro huu wanasema makubaliano ya mwaka 2018 yangeiruhusu Korea Kaskazini kutuma meli katika eneo la  mpaka la bahari lenye mgogoro.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW