Korea Kaskazini yatangaza hali ya vita na Kusini
30 Machi 2013Hii ni baada ya kuwekewa vikwazo vya kimataifa kufuatia jaribio lake la silaha za nyuklia.
Shirika la habari la Korea Kaskazini KCNA, limetoa taarifa inayosema kuwa kuanzia sasa, uhusiano wa Kaskazini na Kusini utaingia katika hali ya vita, na kwamba maswala yote yanayojitokeza kati ya Kaskazini na Kusini yatashughulikiwa ipasavyo.
Tangu mwanzoni mwa mwezi huu Korea kaskazini imekuwa ikitishia kila siku kuishambulia Korea kusini pamoja na kambi za kijeshi za Marekani.
Vitisho hivi vinakuja baada ya Marekani na Korea Kusini kuanzisha mazoezi ya kawaida ya kijeshi, na imeyaamrisha majeshi yake kukaa kwa tahadhari na kuwa tayari kushambulia wakati wowote.
Korea kaskazini imetoa kitisho kipya kuishambulia Marekani, baada ya ndege mbili za Marekani chapa B-2 zenye uwezo wa kubeba makombora ya nyuklia kufanya mazoezi nchini Korea ya Kusini.
Wasiwasi juu ya kitisho cha Korea Kaskazini
Kitisho cha Korea Kaskazini cha kuingia vitani na Korea Kusini kumezusha wasiwasi mkubwa katika rasi ya Korea. Taarifa iliotolewa na Pyongyang hii leo imesema itabatilisha makubaliano yote ya kutoshambuliana yaliyofikiwa kati ya Kaskazin na Kusini.
Mapema wiki hii Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un aliamuru jeshi lake kujitayarisha kufuatia hatua ya Marekani na Korea Kusini kukataa kufuta mazoezi ya kijeshi ya kiwango kikubwa yaliopangwa kufanywa kwa pamoja na nchi hizo mbili.
Kiongozi huyo ameonya kuwa nchi yake iko tayari kukabiliana na nchi hizo mbili haswaa baada ya ndege hizo mbili za kijeshi za Marekani kupeleka kundi la majeshi nchini Korea kusini.
Pyongyang inahofiwa kuwa hatua ya nchi hizo mbili - Marekani na Korea Kusini inanuia kufanya uvamizi wa kijeshi ndani ya nchi yake.
Pyongyang inachukua hatua ya kujutia
Hata hivyo tayari wachambuzi nchini humo wanasema ghasia kamili zikiibuka itakuwa ni njia moja ya Pyongyang kujimaliza yenyewe.
Wachambuzi pia wamesema vitisho hivi vinanuia kuishawishi Marekani kuingia katika meza ya mazungumzo, kumhimiza rais mpya wa Seoul kubadilisha sera yake dhidi ya Korea Kaskazini na kujenga umoja ndani ya nchi bila ya kutishia vita vikubwa kati ya Kusini na Kaskazini.
Julai mwaka huu itatimia miaka 60 tangu Korea kaskazini na China zilipotia saini mkataba na Marekani pamoja na Umoja wa Mataifa kumaliza vita vya miaka mitatu vilivyosababisha vifo vya watu wengi.
Wanajeshi wa China waliosaidia jeshi la Korea Kaskazini katika mapigano hayo wameondoka nchini humo, huku takriban wanajeshi 28,500 wa Marekani wakibakia hadi leo Korea kusini na wengine 50,000 wako karibu na Japan.
Ujerumani yatoa maoni yake
Kwa upande wake, mkuu wa shirika la ujasusi wa nje nchini Ujerumani Gerhard Schindler, aliliambia gazeti la Bild am Sonntag kwamba hii si mara ya kwanza Korea Kaskazini kutoa vitisho kama hivi.
Schindler amesema kwa upande wao wanaona kwamba Korea Kaskazini haiko tayari kuingia vitani bali inaona kuwa Marekani inataka kuingilia kutokana na azma yake ya kuwa na silaha za nyuklia kwa kuwa nchi hiyo imeweka bajeti kubwa ya fedha katika idara ya ulinzi, sayansi na teknologia.
Hata hivyo kile Korea kaskazini inachohitaji hasa ni uhalali mbele ya Marekani na pia mkataba wa amani. Pyongyang wanataka majeshi ya Marekani kutoka kabisa katika ardhi ya Korea na vitisho vya mabomu na makombora ndiyo karata ya mwisho waliobakiza, na wanayotumaini itawaleta wamarekani katika meza ya mazungumzo.
Mwandishi Amina Abubakar/AP/dpa
Mhariri Iddi Ssessanga