Korea Kaskazini yathibitisha mlipuko wa kwanza wa COVID
12 Mei 2022Kituo cha televisheni cha taifa KRT, Jumatano kimerusha picha ya vidio ikimuonyesha kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un akiwa amevaa barakoa wakati akiongoza mkutano wa kamati yenye nguvu ya kisiasa ya chama tawala cha Wafanyakazi kujadili mlipuko wa Covid-19 nchini humo.
Soma pia: Kim Jong Un aombwa kuzungumza na mrithi wake Suk Yeol
Katika picha za siku za nyuma za mikutano kama hiyo au matukio mengine, kila mmoja isipokuwa yeye tu, alivaa barakoa. Kim aliitisha mkutano huo Jumanne kuamuru kuwekwa vizuwizi vikali kote nchini na kuandaa vifaa vya dharura vya tiba baada ya kuthibitishwa kwa mlipuko huo.
Hatua hiyo ya kukiri hadharani juu ya mambukizi ya Covid inamulika uwezekano wa mgogoro mkubwa katika taifa hilo ambalo limekataa msaada wa kimataifa wa chanjo na kuifunga mipaka yake.
Kufikia mwezi Machi, hakukuwa na visa vya Covid-19 vilivyoripotiwa kwa mujibu wa shirika la afya duniani, WHO, na hakuna taarifa zozote rasmi za Wakorea Kaskazini waliochanjwa.
Soma pia: Ni kwa nini Pyongyang ilidanganya kuhusu jaribio la kombora?
Kwa mujibu wa ripoti ya KRT, sampuli zilizochukuliwa Mei kutoka watu wanane mjini Pyongyang, ambao walikuwa wanaugua homa, zilionyesha walikuwa na aina ndogo ya kirusi cha Omricron, kinachojulikana kama BA.2, bila hata hivyo kufafanua idadi ya kesi au chanzo cha maambukizi hayo.
Kamati ya kisiasa iliwakosoa maafisa wa kupambana na janga hilo kwa kukosa ufahamu, uzembe, kutowajibika na kukosa uwezo, lilisema shirika la utangazaji la serikali.
Hakukuwa na maambukizi Korea Kaskazini?
Ingawa Korea Kaskazini haijawahi kuthibitisha hapo kabla maambukizi yoyote ya virusi vya corona nchini humo, maafisa nchini Korea Kusini na Marekani wametilia mashaka kwamba taifa hilo halijakumbwa kabisaa na maradhi hayo, wakati ambapo visa vya kirusi aina ya Omicron vilikuwa vinaripotiwa pakubwa katika taifa jirani la Korea Kusini na pia nchini China.
Taifa hilo lililotengwa limeweka hatua kali za karantini, ikiwemo vizuwizi vya mpakani, tangu kuanza kwa janga la Covid mapema mwaka 2020. Julai mwaka huo, Kim alitangaza dharura na kuweka vizuwizi dhidi ya Kaesong, karibu na mpaka wa Korea mbili kwa muda wa wiki tatu baada ya mwanaume alietorokea Kusini mwaka 2017, kurejea mjini humo akionyesh dalili za virusi vya corona.
Soma pia: China na Urusi zazuia vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini
Kwa mujibu wa data kutoka shirika la afya duniani, WHO, watu 64,207 kati ya raia zaidi ya milioni 24.7 wa Korea Kaskazini ndiyo wamepima covid-19, na wote walikutwa hawana virusi hivyo kufikia Machi 31.
Korea Kaskazini imekataa shehena za chanjo kutoka mpango wa kimataifa wa kugawana chanjo wa COVAX pamoja na chanjo ya Sinovac Biotech kutoka China, hali inayoashiria kuwa huenda hakuna raia hata mmoja aliechanjwa.
Chanzo: Mashirika