1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kaskazini

Korea Kaskazini yavurumisha makombora mengine ya masafa

22 Julai 2023

Korea Kaskazini imefyetua "makombora kadhaa ya masafa marefu" usiku wa kuamkia leo kuelekea Bahari ya Njano inayopatikana kati ya China na rasi ya Korea.

Mvutano kwenye rasi ya Korea
Televisheni za Korea Kusini zikionesha makombora yaliyorushwa na Korea Kaskazini Picha: Ahn Young-joon/AP Photo/picture alliance

Hayo yameripotiwa na Shirika la Habari la Korea Kusini, Yonhap, likinukuu maafisa wa jeshi la nchi hiyo.

Ufyetuaji huo umefanyika ikiwa zimepita siku tatu pekee tangu nchi hiyo ilipofanya majaribio mengine ya makombora mawili ya masafa marefu katika wakati mivutano inaongezeka kwenye eneo la rasi ya Korea.

Mfululizo huo wa mashambulizi yumkini ni jibu la utawala wa Pyongyang kwa safari ya nyambizi ya Marekani yenye uwezo wa nyuklia nchini Korea Kusini.

Nyambizi ya kijeshi ya Marekani ikiwa imetia nanga kwenye mjini Busan huko Korea Kusini Picha: Woohae Cho/AP Photo/picture alliance

Korea Kaskazini imeghadhibishwa na uamuzi wa Washington wa kutuma chombo hicho cha kijeshi ikisema unatishia "kuzusha mzozo wa nyuklia kwenye rasi ya Korea".

Kulingana na Baraza la Wakuu wa Majeshi nchini Korea Kusini, makombora yaliyorushwa yalibainika mnamo saa za alfajiri ya Jumamosi lakini idadi yake kamili haijapatikana.

Baraza hilo limesema Korea Kusini na Marekani zinafuatilia kwa karibu majaribio hayo ya makombora.

Miaka ya karibuni, Korea Kaskazini imekuwa ikijaribu aina mpya kabisa ya makombora ya masafa inayoyatambulisha kuwa ya "kimkakati," ikimaanisha kuwa yana uwezo wa kubeba silaha za nyuklia.

Mataifa ya G7 na washirika wengine kuirai China iizuie Korea Kaskazini kukwepa vikwazo

Wakati hayo yakijiri kundi la mataifa tajiri la G7 na nchi nyingine mbili pamoja na Umoja wa Ulaya zimeandika barua kwenda kwa China ya kuitaka nchi hiyo kusaidia kuizuia Korea Kaskazini kuepeuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa kwa kutumia eneo la bahari la China.

Kundi hilo la mataifa limesema lina mashaka juu ya uwepo kwa meli za mafuta kwenye eneo la bahari la China la Sansha Bay ambazo inaamini zinafanya biashara ya mafuta na Korea Kaskazini na kukwepa vikwazo ilivyoewekewa nchi hiyo na Umoja wa Mataifa.

Barua iliyoandikwa itatumwa kwa Balozi wa China kwenye Umoja wa Mataifa Zhang Jun. Imetiwa saini na wanachama wote wa kundi la G7 yaani Marekani, Canada, Uingereza, Japan, Italia, Ujerumani na Ufaransa pamoja na New Zealand, Korea Kusini na Umoja wa Ulaya.

Nakala itakayotumwa itaambatanisha picha za satelaiti ambazo kwa mujibu wa kundi hilo la mataifa zinaonesha waziwazi jinsi matendo hayo ya kukwepa vikwazo vya Umoja wa Mataifa yanavyoendelea kufanywa ndani ya mipaka ya China kuanzia mwaka 2022 na mwaka huu.

Korea Kaskazini imekuwa chini ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2006 kuhusiana na mradi wake wenye utata wa nyuklia na uundaji wa makombora ya masafa. Hiyo inajumuisha vikwazo vya mwaka 2017 vinavyoweka ukomo wa kiwango cha mafuta ambacho taifa hilo linaweza kuagiza kutoka nje.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW