Korea Kaskazini yawatimua wachunguzi wa shirika la IAEA
15 Aprili 2009Korea Kaskazini imewaamuru wachunguzi wa shirika la kimataifa la kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia, IAEA, kuondoka nchini humo. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya utawala wa Pyongyang kuamua kuanzisha tena mpango wake wa silaha za nyuklia na kutangaza kujiondoa kwenye mazungumzo ya mataifa sita kufuatia kauli kali ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu jaribio lake la kombora la masafa marefu siku 10 zilizopita.
Huku ikiadhimisha siku ya kuzaliwa ya baba wa taifa, Kim Il-Sung, hii leo, Korea Kaskazini imeisifu hatua yake ya kurusha roketi angani ikiitaja kuwa ushindi wa kihistoria.
Saa chache baada ya Korea Kaskazini kutangaza kujiondoa kwenye meza ya mazungumzo ya mataifa sita kuhusu mpango wake wa nyuklia, shirika la kimataifa la kuzuia utapakazaji wa silaha za nyuklia, IAEA, limesema wachunguzi wake wametakiwa waondoke nchini humo haraka iwezekanavyo.
Msemaji wa shirika hilo, Marc Vidricaire, amewaambia waandishi wa habari kwamba Korea Kaskazini imewaamuru maafisa wa shirika hilo waondoe vifaa vyao vyote vya uchunguzi katika kinu cha nyuklia cha Yongbyon na baadaye hawatoruhusiwa tena kuingia katika kinu hicho.
Wachunguzi hao walikuwa wakisimamia kazi ya kukiharibu kinu cha Yongbyon kama sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa mnamo mwezi Februari mwaka 2007 na mataifa sita yanayoshiriki kwenye mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini. Mazungumzo hayo ambayo yamekuwa yakiendelea tangu mwaka 2003 yanazijumulisha Korea Kaskazini, Korea Kusini, Marekani, China, Urusi na Japan.
Ukosoaji
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Hilary Clinton, ameieleza hatua ya Korea Kaskazini kuwafukuza wachunguzi wa shirika la IAEA kuwa isiyo na umuhimu wowote kwa taarifa halali ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa iliyolaani hatua ya Korea Kaskazini kurusha roketi lake angani mnamo Aprili 4.
"Tunaiona hatua hii kuwa isiyo na maana kwa taarifa halali ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Bila shaka tuna matumaini kutakuwa na nafasi ya kulijadili swala hili sio tu pamoja na washirika wetu, bali pia hatimaye na Korea Kaskazini."
Katika hatua ambayo huenda izushe hali ya wasiwasi, Korea Kusini imesema itatangaza kujiunga na juhudi za Marekani kukamata meli za Korea Kaskazini zinazoshukiwa kubeba silaha za maangamizi makubwa. Utawala wa Pyongyang umesema hatua hiyo itachukuliwa kama tangazo la vita.
Korea Kusini inasema Korea Kaskazini inavitimiza vitisho vyake na imeitaka Marekani kuishawishi tena nchi hiyo kurejea kwenye mazungumzo ya mataifa sita.
Robert Gibbs, msemaji wa rais wa Marekani, Barack Obama, amesema Korea Kaskazini inafanya kosa kubwa. Ameitaka iachane na vitendo vyake vya uchokozi na iheshimu utashi wa jumuiya ya kimataifa na kutimiza ahadi zake. Tangazo la Korea Kaskazini kujiondoa kwenye mazungumzo ya mataifa sita ni mtihani wa kwanza mkubwa kwa sera za kigeni za utawala wa rais Obama. Watalaam wa Marekani wanasema rais Obama atatafuta njia za kuanzisha tena mazungumzo hayo.
Uingereza imeilaani hatua ya Korea Kaskazini kusitisha ushirikiano na shirika la kimataifa la kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia, IAEA, ikisema haina uhalali wowote na kuitaka irejee kwenye mazungumzo.
Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Uingereza amesema Korea Kaskazini ina njia moja tu ya kufuata, nayo ni kuchukua nafasi yake kama mwanachama kamili wa jumuiya ya kimataifa. Lazima Korea Kaskazini itimize ahadi zake na hasa kushirikiana na shirika la IAEA katika kumaliza mpango wake wa nyuklia. Uingereza imesema itaendelea kuishawishi Korea Kaskazini irejee kwenye mazungumzo ya mataifa sita kuhusu mpango wake wa nyuklia.
China imezitolea mwito pande zote zinazoshiriki katika mazungumzo ya mataifa sita ziwe na utulivu na zijizuie huku ikiwa na matumaini kwamba mazungumzo hayo inayoyaandaa mjini Beijing yataanza tena.
Mwandishi: Charo, Josephat/RTRE/AFPE
Mhariri: Thelma Mwadzaya