Korea Kaskazini yazidi kuionyesha dunia ubabe
15 Septemba 2017Waziri wa ulinzi wa Japan Istunori Onodera, aliwaambia waandishi habari kuwa umbali wa kombora hilo ungetosha kulifikisha katika kisiwa cha Marekani cha Guam kilichoko katika bahari ya Pacific, na kwamba ufatuaji huo ulilenga kujaribu ufanisi wa kombora hilo jipya na umbali linaloweza kuruka.
Maafisa wa ulinzi wa Japan wanaamini kombora hilo lina uwezo wa kufika umbali wa hadi kilomita 5,000.
Jaribio la Ijumaa limekuja chini ya wiki mbili tangu Korea Kaskazini ilipofanya jaribio lake la sita la kombora la nyuklia ambalo lilielezwa kuwa lenye nguvu zaidi, na siku moja baada ya serikali mjini Pyongyang kutoa vitisho dhidi ya Marekani na washirika wake, ikiwemo Japan.
Baraza la usalama laitisha kikao cha dharura
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha kikao cha dharura siku ya Ijumaa, kilichoombwa na Marekani na Japan.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani jaribio hilo, na katika taarifa aliyoitoa leo, ameutolea wito uongozi wa Korea Kaskazini kukoma kufanya majaribio mengine, kuheshimu maazimio ya Umoja wa Mataifa, na kutoa nafasi ya kuanzisha tena majadiliano ya dhati kuhusu uondoaji wa silaha zake za nyuklia.
Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe, alisema serikali ya Tokyo haiwezi kuvumilia kitendo cha kuudhi kama hicho.
Naye rais wa Korea Kusini Moon Jae in alisema katika taarifa kuwa uchokozi unaojirudia wa Korea Kaskazini ni kitisho kikubwa kwa kwa rasi ya Korea, na kwa amani na usalama wa jumuiya ya kimataifa.
Katibu Mkuu wa jumuiya NATO Jens Stoltenberg alisema alilielezea jaribio hilo kama ukiukaji mwingine wa kizembe wa maazimio ya Umoja wa Mataifa unaohitaji kuitikiwa kimataifa.
China: Alieanzisha mzozo aumalize
Kwa upande wake, China, ambayo ni jirani mwenye uhusiano wa kiuchumi na Korea Kaskazini, ililaani jaribio hilo na kusema linakiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa, lakini ilipinga madai kuwa yenyewe ndiyo inahusika na kushamiri kwa mzozo katika eneo hilo. Hua Chunying ni msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya China.
"Suala la nyuklia la Korea Kaskazini ni la kiusalama zaidi na kiini chake ni tofauti kati ya Korea Kaskazini na Marekani. China siyo mlengwa katika suala hilo na haihusiki na kuongezeka kwa mgogoro huo," alisema Hua Chunying, msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya China na kuongeza kuwa, alieanzisha matatizo ndiye anaepaswa kuyamaliza.
Urusi pia ililaani jaribio hilo, huku msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov akilitaja kama uchokozi utakaosababisha kuongezeka kwa mzozo katika rasi ya Korea. Urusi na China, ambazo zina uhusiano wa karibu na Korea Kaskazini, zote ni wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Baraza liliiwekea Korea Kaskazini vikwazo vipya siku ya Jumatatu, kuhusiana mipango yake ya nyuklia na makombora, hii ikiwa ni juu y avikwazo vingine ilivyowekewa wiki tano zilizopita, ambavyo vilitarajiwa kupunguza karibu dola bilioni moja kutoka mapato ya dola bilioni tatu yatokanayo na mauzo ya nje.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae, rtre, afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman