1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Korea Kusini kuongeza ushirikiano wake na Afrika

4 Juni 2024

Rais Yoon Suk Yeol wa Korea Kusini ni mwenyeji wa mkutano wa kilele na viongozi wa kiafrika. Wawakilishi kutoka mataifa 48 ya Afrika, wakiwemo wakuu wa nchi 25, wanahudhuria mkutano huo wa siku mbili.

Ujumbe wa Korea Kusini wakiwa katika mazungumzo na wenzao wa Angola.
Ujumbe wa Korea Kusini wakiwa katika mazungumzo na wenzao wa Angola. Picha: Yonhap/picture alliance

Katika hotuba yake kwenye Mkutano wa Korea Kusini na Afrika, Yoon  amesema nchi yake itazidisha misaada ya maendeleo barani Afrika ifikapo mwaka 2030 na kuongeza ushirikiano wa kina hasa katika sekta muhimu za madini na teknolojia.

Maafisa wa Korea Kusini wanasema kupanua mahusiano katika sekta ya madini na rasilimali kutasaidia kuboresha ustahimilivu wa mnyororo wa ugavi katika sekta muhimu kama za kutengezeneza betri.

Biashara na mataifa ya Afrika kwa sasa inachangia chini ya asilimia 2 ya jumla ya uagizaji na mauzo ya nje ya Korea Kusini.

Soma pia:Korea Kusini kutanua ushirikiano na bara la Afrika

Yoon pia amezitolea wito nchi za Afrika kuchukua hatua madhubuti katika kampeni ya shinikizo la kimataifa dhidi ya Korea Kaskazini.

"Ili kuimarisha ushirikiano na Afrika, Korea Kusini itapanua Msaada Rasmi wa Maendeleo hadi karibu dola bilioni 10 ifikapo mwaka 2030." Alisema

Ameongeza kuwa "ili kuhimiza biashara na uwekezaji wa Korea Kusini katika kanda, Korea Kusini itatoa dola bilioni 14 kwa fedha za mauzo ya nje."

Kauli hii ni baada ya Korea Kaskazini hivi karibuni kuzidisha majaribio yake ya mifumo ya silaha zenye uwezo wa nyuklia na kupeperusha mamia ya maputo ambayo yalimwaga tani za takataka na mbole Korea Kusini wakati uhusiano Korea kusini na Kaskazini ukizidi kuwa mbaya.

"Korea Kaskazini imekuwa ikifanya chokochoko za kipuzi. Lakini pamoja na marafiki zetu barani Afrika, Korea Kusini itatekeleza kikamilifu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kufanya kazi ili kulinda amani kwenye Rasi ya Korea na jumuiya ya kimataifa."

Kuhusu ushirikiano wa biashara na kiuchumi

Rais wa Korea Kusini Yoon Suk YeolPicha: KIM MIN-HEE/Reuters

Katika tamko la pamoja Korea Kusini, Umoja wa Afrika na mataifa wanachama, wameahidi kuongeza kasi kwenye mazungumzo ya mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi na biashara na mifumo ya kukuza uwekezaji.

Aidha viongozi hao wametoa wito wa kuendeleza ushirikiano kwa ajili ya usalama wa chakula barani Afrika na kupata msaada wa teknolojia ya kilimo kutoka kwa wa Korea Kusini.

Soma pia:Mkutano wa Korea-Afrika kuangazia madini na biashara

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Mauritania Mohamed Ould Ghazouani, katika mkutano wa pamoja wa wanahabari na Yoon, amesema nchi za Afrika zinatafuta kujifunza kutokana na uzoefu wa Korea katika kuendeleza rasilimali watu, maendeleo ya viwanda na mabadiliko ya kidijitali.