Korea Kusini na Kaskazini zaanza mazungumzo ya ngazi ya juu
9 Januari 2018Korea ya Kaskazini imesema itapeleka ujumbe mzito wa wanariadha na maafisa katika michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi, ambayo itafanyika nchini Korea Kusini mwezi ujao. Suala hilo la wanariadha lilikuwa agenda kuu katika mazungumzo hayo ambayo ni ya kwanza kufanyika katika muda wa miaka miwili.
Marekani, kupitia wizara ya mambo ya nchi za nje imesema mazungumzo ya leo kati ya Korea mbili ni mwanzo mzuri, lakini ikatoa tahadhari kwamba bado ni mapema kujua iwapo yatazaa matunda yoyote zaidi ya ushiriki katika michezo ya Olimpiki. Wizara ya mambo ya nje ya China pia imesema imefurahia kufanyika kwa mazungumzo baina ya Korea mbili.
Watano kila upande
Ujumbe wa Korea Kusini umeoongozwa na waziri wa masuala ya muungano wa Korea mbili Cho Myoung-Gyon, akisindikizwa na maafisa waandamizi wanne. Ujumbe wa Korea Kaskazini vile vile ulikuwa wa watu watano, kiongozi wao akiwa afisa wa ngazi ya juu Ri Son-Gwon.
Ujumbe wa Korea Kusini unaoongozwa na waziri wa masuala ya muungano wa Korea mbili Cho Myoung-Gyon, akisindikizwa na maafisa waandamizi wanne. Msafara wao wa magari kuelekea kijiji cha Panmunjom kilichoko katika ukanda usio na shughuli za kivita kwenye mpaka wa nchi hizo pacha na mahasimu, ulipungiwa mikono na kundi la watu waliofika kuwatakia maafisa hao mafanikio. Ujumbe wa Korea Kaskazini vile vile ulikuwa wa watu watano, kiongozi wao akiwa afisa wa ngazi ya juu Ri Son-Gwon.
''Safari ya wawili hufika mbali''
Viongozi hao wa ujumbe walichukuliwa picha wakishikana mikono mbele ya Jengo la Amani ambako mazungumzo yamefanyika.
Kiongozi wa ujumbe wa Korea Kaskazini, Ri Son-Gwon ambaye kama kawaida ya maafisa wa nchi yake alivaa beji zenye picha ya mwasisi wa Korea Kaskazini Kim Il-Sung na warithi wake, alitaka mazungumzo hayo yawe zawadi njema ya mwaka mpya kwa wakorea wote, akisema, ''Safari ya watu wawili hufika mbali kuliko ya mtu mmoja''.
Mwenzake wa Korea Kusini alisema michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi itakayofanyika katika mji wa Pyeongchang itakuwa michezo ya amani, akiongoza kuwa washiriki kutoka Korea Kaskazini wanasubiriwa kwa hamu kuungana na wenzao kutoka kwingineko ulimwenguni.
''Watu wanayo hamu kubwa kuona Korea Kaskazini na Kusini zikichukua njia ya amani na maridhiano'', amesisitiza Cho Myoung-Gyon.
Picha tofauti
Yalikuwa mazingira tofauti kabisa na kauli za uhasama ambazo zimetawala hivi karibuni, ambapo kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amerushiana vitisho na Rais Donald Trump wa Marekani, kufuatia hatua ya Korea Kaskazini kuyafanyia majaribio makombora yanayoweza kupiga shabaha nchini Marekani.
Korea Kaskazini imejitahidi kuitangaza michezo ya Olimpiki ya Pyeongchang kama michezo ya amani, mji huo ukiwa umbali wa km 80 tu kutoka mpaka baina ya Korea mbili. Hata hivyo, bila kushiriki kwa Korea Kaskazini, mada hiyo ya amani isingekuwa na mashiko.
Ikiwa Korea Kaskazini itaridhia, Korea Kusini inataka wanariadha wa nchi hizo mbili waingie kama kundi moja wakati wa sherehe za ufunguzi na za kuyafunga mashindano hayo, kama ilivyofanyika awali, katika michezo ya Olimpiki ya Sydney mwaka 2000, michezo ya Athens 2004, na ile ya Turin mwaka 2006.
Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, afpe, ape
Mhariri: Grace Kabogo