Korea Kusini yaongeza kasi ya juhudi za raia wao kuachiwa na Taleban
23 Julai 2007Ni katika eneo hilo ndiko kulikoanzishwa kundi la Taleban. Korea Kusini ina takriban majeshi 200 nchini humo ambayo kundi la Taleban inataka yaondoke huku likishinikiza serikali kuwaachiwa wafungwa wake 10.
Wapiganaji wa Taleban wamewapa Korea Kusini hadi jioni ya leo ili kuondoa majeshi yake nchini Afghanistan vilevile kuwaachia wafungwa wake 23 . Wengi wao ni manesi na waalimu wa lugha ya Kiingereza walio na umri wa miaka 20 hadi 30.
Hata hivyo inaripotiwa kuwa majadiliano ya kujaribu kuwashawishi kundi la Taleban kuwaachia mateka hao yanaripotiwa kutoendelea vizuri.Kwa mujibu wa msemaji wa kundi hilo Yusuf Ahmadi aliyezungumza na shirika la habari la AFP huenda wakatimiza vitisho vyao vya kuwaua ifikapo jioni.
Kulingana na kiongozi huyo ujumbe wa serikali ya Afghanistan katika mazungumzo hayo hauna madaraka kamili ya kuwaachia wafungwa wa Taleban.
Wakati mazungumzo ya kutafuta suluhu yanaendelea wapiganaji wa Taleban wanaripotiwa kuzingira kundi la mateka hao 70 kwenye eneo la Qarabagh mkoani Ghazni.
Ujumbe wa maafisa wanane wa serikali ya Korea kusini wakiwemo naibu waziri wa mambo ya nje na mshauri wa rais wanashiriki katika mazungumzo hayo. Kulingana na vyombo vya habari vya Korea kasisi wa kanisa la Saemmul lililopeleka watu hao 23 anatangaza kusimamisha shughuli nchini Afghanistan na kuomba radhi kwa jamii zao.
Kwa upande mwingine kamanda wa majeshi ya usalama wa kimataifa ISAF katika kikosi cha NATO nchini Afghanistan Jenerali Dan McNeill anasisitiza kuwa sharti wamalize kazi yao nchini Afghanistan
''Tusipoenda Afghanistan kudumisha amani basi matatizo ya huko yatatufata katika mataifa yetu.Hayo yameshatokea na huenda yakajirudia tusipomaliza kazi yetu nchini humo.Naamini huenda tukahatarisha usalama katika mataifa yetu.''
Mwili wa raia mmoja wa Ujerumani ulipatikana mwishoni mwa wiki ukiwa na majeraha ya risasi.Kwa mujibu wa taarifa mhandisi huyo alikuwa na umri wa miaka 44 na kuumwa kisukari. Bunge la Ujerumani linapanga kupigia kura mpango wa majeshi ya Ujerumani kubakia nchini Afghanistan kwa madhumuni ya ukarabati.Mpaka sasa Ujerumani ina majeshi alfu 3 nchini humo.Kansela wa ujerumani Bi Angela Merkel anasisitiza umuhimu ya vikosi hivyo
''Kwangu mimi ni muhimu sana kwa serikali ya Ujerumani kueleza bayana juhudi za kijeshi vilevile ujenzi wa Afghanistan.Ujenzi bila usalama hautawezekana.Kuna nchi nyingi ambazo zinashiriki katika ujenzi huo na kuhakikisha kuwa usalama unadumishwa katika juhudi za kukarabati Afghanistan.Sote tunajukumu la pamoja katika suala hilo.''
Ujerumani inajiandaa kufanya uchunguzi wa mwili wa mhandisi huyo aliyeuawa ili kujua chanzo cha kifo.Wakati huohuo Korea Kusini inatangaza hatua mpya za vikwazo vya usafiri kwa raia wake kuzuru Afghanistan.Nchi hiyo imeorodhesha Somalia na Iraq katika ratiba ya nchi inazopiga marufuku raia wake kuzuru.
Kwa mujibu wa afisa mmoja wa wizara ya mambo ya ya Korea Kusini Han Hye-jin wanaokiuka agizo hilo huenda wakaadhibiwa kifungo cha mwaka mmoja jela au kutozwa faini ya dola 3200.Sheria hiyo inaanza kutekelezwa hapo kesho.