1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kusini yatoa pendekezo rasmi kwa Kaskazini

Admin.WagnerD25 Aprili 2013

Korea kusini imetoa pendekezo la mazungumzo rasmi na Korea Kaskazini kuhusu kufunguliwa kwa kiwanda cha pamoja cha Kaesong na kutishia kujiondoa katika mradi huo wa pamoja iwapo kaskazini itakataa kuitikia wito huo.

Magari yakizuiwa kuingia katika eneo la viwanda la Kaesong.
Magari yakizuiwa kuingia katika eneo la viwanda la Kaesong.Picha: Reuters

Korea kusini imesema inatoa fursa ya kuwepo kwa mazungumzo ili kusuluhisha mzozo uliopo kuhusu kiwanda hicho cha Kaesong ambacho ni kiunganishi muhimu kati ya nchi hizo mbili na kujipata kuathirika kutokana na uhasama ambao umekuwa ukitotokota katika rasi ya Korea.

Mwanajeshi wa Korea Kusini akiweka kizuizi katika daraja linaloziunganisha Korea mbili, baada ya Kusini kufunga eneo la viwanda la Kaesong.Picha: Getty Images

Masharti ya mazungumzo

Ombi hilo la Korea kusini la kutaka mazungumzo hata hivyo limekuja na masharti fulani ambayo haikutaka kuyataja iwapo Kaskazini itakataa kukukabali pendekezo hilo katika kipindi cha saa 24 zijazo.Msemaji wa wizara ya muungano ya Korea kusini Kim Hyung Seok amesema kuwa bado hawajabadili msimamo wao wa kuunga mkono kuboreshwa na kuendelezwa kwa shughuli dhabiti katika kiwanda hicho lakini hawataruhusu kuacha hali iendelee kama ilivyo sasa katika kiwanda hicho.

Kim hakufafanua zaidi kuhusu ni hatua gani Korea kusini itachukua iwapo Kaskazini itakataa kutii pendekezo lao lakini inadokezwa kuwa huenda Kusini inatafakari kujiondoa kabisa kutoka kiwanda hicho ambacho kwa kawaida kinaajiri wafanyakazi elfu 53 katika kampuni 123 zinazomilikiwa na Korea kusini.Mazungumzo hayo yanayopendekezwa yatakuwa kati ya viongozi wa pande zote mbili wa kamati simamizi wa shughuli za kibiashara katika kiwanda hicho.

Pendekezo hilo linawadia siku moja tu baada ya Korea kusini kutangaza kuwa serikali itazisaidia kampuni zilizoathirika katika mzozo huo wa Keosong ili kutatua matatizo za kifedha yaliyosababishwa na hasara ya mali na kufutiliwa mbali kwa maombi ya wateja.

Waandishi wa habari wakiwa wamezuiwa kuingia katika eneo la viwanda la Kaesong.Picha: Jung Yeon-Je/AFP/Getty Images

Kitega uchumi muhimu kwa Kaskazini

Eneo hilo la viwanda lilianzishwa mnamo mwaka 2004 na liko kilomita 10 ndani ya mpaka wa Korea Kaskazini. Kaesong ni kitega uchumi muhimu kwa Korea Kaskazini ambayo inazongwa na umasikini kupitia kodi na ushuru na malipo ya wafanyakazi.Mradi huo ulianzishwa chini ya makubaliano ya amani ya Korea hizo mbili yaliyoongozwa na Rais wa Korea kusini Kim Dae Jung miaka ya 90 na kupelekea mkutano wa kihistoria na kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong II mwaka 2000.

Rasi ya Korea ilikuwa imekumbwa na mzozo uliochochewa na jaribio la kinyuklia la Korea Kaskazini mwezi Februari wakati ilipoamua kuzuia wafanyakazi wa kutoka kusini kuingia katika kiwanda hicho tarehe 3 mwezi huu.Kaskazini ilighadhabishwa na matamshi ya waziri wa ulinzi wa Kusini kuwa kuna mipango ya kijeshi ya dharura ya kuwalinda wafanyakazi wa kusini katika kiwanda hicho na hivyo kuilazimu Kaskazini kukifunga kabisa kiwanda hicho tarehe 9 mwezi huu na kusitisha shughuli zote.

Tangu hapo imedinda maombi kadhaa ya kupelekea wafanyakazi wa kusini walioamua kusalia kiwandani humo vyakula na mahitaji mengine ya kimsingi.Chama cha wawakilishi wa kampuni za korea kusini zimesema zinatumai mazungumzo hayo yataanza haraka iwezekanavyo.

Mwandishi: Caro Robi/afp
Mhariri: Iddi Ssessanga.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW