1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kosovo yangojea kutambuliwa kama taifa jipya

18 Februari 2008

Tangazo la uhuru wa Kosovo lasherehekewa na wakaazi wenye asili ya Kialbania.

Waziri Mkuu wa Kosovo,Hashim Thaci akitangaza uhuru wa Kosovo katika bunge mjini PristinaPicha: AP

Siku ya Jumapili,Kosovo ilijitangazia uhuru wake kutoka Serbia na sasa ndio inangojea kutambuliwa na nchi za magharibi,licha ya upinzani mkali kutoka Serbia na mshirika wake mkuu Urusi.Jumapili hiyo hiyo Urusi iliitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York.Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa,Vitaly Churkin alisema kuwa tangazo la Kosovo halikubadilisha cho chote nchini Serbia.Kwani kwa maoni ya Serbia tume ya Umoja wa Mataifa iliyopo Kosovo kuambatana na Azimio 1244 ndio yenye mamlaka katika jimbo hilo lililojitenga.Azimio hilo la Umoja wa Mataifa lilipitishwa mwishoni mwa vita vya Kosovo katika mwaka 1999 na jimbo hilo likapewa mamlaka ya ndani chini ya usimamizi wa serikali ya Serbia.Vile vile tume ya Umoja wa Mataifa ikisaidiwa na NATO ilipewa mamlaka ya kuliongoza jimbo hilo lenye wakaazi wengi wenye asili ya Kialbania.

Waziri Mkuu wa Kosovo Hashim Thaci akijaribu kutuliza hofu za wakaazi wenye asili ya Kiserbia wapatao 120,000 alisema,Kosovo itakuwa nchi ya wakaazi wake wote.Lakini Waserb wachache wakiongozwa na wenzao wanaoishi hasa kaskazini mwa Kosovo na wakiungwa mkono na serikali ya Belgrade wanapinga kabisa uhuru wa Kosovo.Kwa hivyo kuna kila ishara kuwa ule mgawano wa kikabila ungali ukiiendelea kati ya makabila hayo mawili katika Kosovo.

Kwa upande mwingine takriban nchi zote 27 wanachama katika Umoja wa Ulaya zinatazamiwa kuitambua Kosovo na kuidhinisha kupeleka Kosovo tume ya watu 2,000 kuisimamia nchi hiyo mpya.Lakini kama nchi sita katika umoja huo bado zinasitasita.

Hata hivyo leo hii mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana kulijadili suala la Kosovo.Inatazamiwa kuwa taifa hilo jipya litatambuliwa na Ujerumani Uingereza, Ufaransa,Italia na Marekani.Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Australia Kevin Rudd ameshasema kuwa Australia itatambua uhuru wa Kosovo.Amesema,historia ya huzuni ya watu wa Kosovo humaanisha kuwa wakaazi wake wanapaswa kusaidiwa.Kwa hivyo,serikali ya Australia itaitambua Kosovo kibalozi upesi iwezekanavyo.