1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kremlin: Putin yuko tayari makubaliano ya amani Ukraine

20 Julai 2025

Urusi imesema rais wa nchi hiyo Vladimir Putin yupo tayari kufikia makubaliano ya amani na Ukraine lakini dhamira ya utawala mjini Moscow ni kutimiza malengo yake ya vita.

Rais Vladimir Putin wa Urusi
Rais Vladimir Putin wa Urusi.Picha: Sefa Karacan/Anadolu/picture alliance

Hayo yamesemwa na msemaji wa Ikulu ya Urusi, Kremlin alipozungumza na kituo cha televisheni cha nchi hiyo. Sehemu ya mahojiano hayo yamechapishwa siku ya Jumapili.

"Rais Putin amerejea kusema mara kadhaa juu ya shauku yake ya kufikisha mwisho mzozo wa Ukraine kwa njia ya amani haraka iwezekanavyo. Huo ni mchakato mrefu na unahitaji juhudi mahsusi na siyo kitu rahisi," amesema Peskov kwenye mahojiano hayo na mtangazaji wa televisheni ya taifa Pavel Zarubin.

"Kitu muhimu kwetu ni kutimiza malengo yetu. Malengo yetu yako wazi kabisa," ameongeza Peskov.

Peskov pia amezungumzia matamshi ya wiki za karibuni yaliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani kuelekea Urusi akisema ulimwengu hivi sasa umeanza kuzoea tabia hiyo ya Trump ya kurusha maneno ambayo wakati mwingine ni "makali".

Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Dmitry Peskov.Picha: Pavel Bednyakov/Pool/REUTERS

Amesema pamoja na hayo, Trump ameonesha bado ana nia ya kuendelea na jitihada za kusaka amani.

Kiongozi huyo wa Marekani amerejea mara kadhaa matamshi yake ya kutaka kuumaliza mzozo wa Ukraine haraka lakini amesema amevunjwa moyo na tabia isiyotabirika ya rais Putin.

Jumatatu ya wiki hii, Trump alitangaza nia ya kuchukua msimamo mzito dhidi ya Urusi, akiahidi msaada mkubwa zaidi wa kijeshi kwa Ukraine, ikiwemo kuipatia mifumo mamboleo ya ulinzi chapa Patriot. Vilevile aliipatia Urusi muda wa mwisho wa siku 50 kufikia makubaliano ya kusitisha vita au ikabiliwe na vikwazo.

Mwanazouni wa kijeshi Ulaya asema matumaini ni madogo kwa vita vya Ukraine kumalizika 

Katika hatua nyingine nchi washirika wa Ukraine hasa za Ulaya zina matumaini madogo na mkakati anaoutumia Trump kuvimaliza vita vinavyoendelea.

Mtizamo huo umo pia miongoni mwa wanazuoni wa nchi za Ulaya. Mtaalamu mmoja wa kijeshi nchini Ujerumani amesema siku ya Jumapili kuwa uwezekano wa kumalizika kwa vita vya Ukraine kwa mazingira ya sasa ni mdogo, na hata kifo cha Rais Vladimir Putin hakitobadili chochote.

"Putin ni mmoja tu kati ya wawakilishi wengi wa utawala wa kiimla, kijeshi na unaopendelea sera za kizalendo," amesema Marcus Matthias Keupp, mwanazuoni wa kijeshi anayefundisha katika shule ya jeshi ya ETH mjini Vienna.

Mfumo wa ulinzi wa anga chapa Patriot. Picha: U.S. Army/ABACAPRESS/picture alliance

Amesema shinikizo likiendelea dhidi ya Urusi, bado Moscow itatumia mbinu cha chini chini kuihujumu Ukraine. "Kutakuwa na umwagaji damu usio na kikomo," amesmea Keupp.

Ametabiri kuwa Moscow itaendelea na jitihada za kuyaingilia mataifa ya Ulaya. Amejenga hoja kuwa Putin tayari anao washirika ndani ya Ulaya ambao ni viongozi wa Hungary na Slovakia na analenga pia kupata viongozi wa aina hiyo nchini Austria na Ujerumani.

"Atajaribu kwa kila hali kuchochea siasa zitazoviingiza madarakani vyama vya mrengo mkali wa kulia ama kushoto vinavyowakilisha mtizamo wake na ajenda yake. amesema Keupp.

Huko kwenye uwanja wa vita, Urusi imedai kuwa vikosi vyake vimechukua udhibiti wa kijiji cha Bila Hora kilichopo kwenye mkoa wa mashariki mwa Ukraine wa Donetsk. Hayo yameripitiwa na shirika la habari la nchi hiyo RIA likiinukuu wizara ya ulinzi ya Urusi.

Madai hayo lakini hayajaweza kuthibitishwa na vyanzo huru vya habari.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW