Kremlin: Ripoti za vijana kuondoka Urusi sio kweli
22 Septemba 2022Takriban watu sita wameuawa karibu na soko katika eneo la mashariki mwa Ukraine la Donetsk linalodhibitiwa na Urusi baada ya kutokea shambulio la risasi.
Meya wa mji wa Donetsk Alexei Kulemzin ameandika kwenye mtandao wake wa Telegram akithibitisha kutokea kwa mauaji hayo. Meya huyo mwenye umri wa miaka 48 amelilaumu jeshi la Ukraine kwa shambulio hilo lililogharimu maisha ya watu sita na kuwajeruhi wengine sita.
Mara kwa mara Ukraine imekuwa ikipuzilia mbali shutma za kuhusika na mashambulizi hayo ikidai yanafanywa na wapiganaji wanayoiunga mkono Moscow.
Soma pia: Maoni: Putin ametangaza vita
Hata hivyo taarifa hizo hazikuweza kuthibitishwa na vyombo huru vya kujitegemea.
Sehemu za mikoa ya mashariki mwa Ukraine za Donetsk na Luhansk zimekuwa mikononi mwa makundi ya wapiganaji watiifu kwa Urusi tangu mwaka 2014.
Mnamo mwezi Februari, Urusi ilitambua uhuru wa maeneo hayo mawili, alafu baadaye ikaivamia Ukraine kwa kisingizio kuwa inafanya hivyo ili kuyalinda maeneo hayo.
Ikulu ya Kremlin leo kwa mara nyengine, imesisitiza kuwa inauchukulia uvamizi wake nchini Ukraine kama "oparesheni maalum ya kijeshi," siku moja tu baada ya rais Vladimir Putin kutangaza uhamasishaji wa vijana 300,000 kujiunga na kikosi cha jeshi.
Tangazo hilo limezua maandamano kote nchini Urusi huku kukiwa na wasiwasi kuwa nchi hiyo imejitosa kikamilifu katika vita na Ukraine.
Tangazo la Rais Vladimir Putin limezua maandamano kote nchini Urusi
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amekanusha vikali ripoti kwamba idadi kubwa ya vijana wenye vigezo vya kujiunga na jeshi wanajaribu kuikimbia nchi hiyo na kwenda Uturuki na mataifa mengine.
Kwa mfano, shirika la ndege la Uturuki limeripoti kuongezeka kwa wasafiri wanaotafuta tiketi ya kutoka Urusi kuelekea Uturuki baada ya tangazo la Putin, wakati Finland nayo ikirekodi idadi kubwa ya watu waliofurika kwenye mpaka wake na Urusi wakijaribu kuingia nchini humo.
Soma pia: Urusi yaonyesha utayari wa mazungumzo
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wameripoti kuwa baadhi ya watu waliopokea maagizo ya kujiunga na jeshi la Urusi walikuwa wamezuiliwa wakati wa maandamano ya kupinga vita hivyo yaliyoibuka katika miji 38 nchini Urusi jana jioni.
Kwa mujibu wa kundi huru linalofuatilia matukio nchini Urusi la OVD-Info, ni kuwa zaidi ya waandamanaji 1,300 waliwekwa kizuizini huku baadhi wakiamrishwa kujiunga na jeshi.
Katika mji mkuu wa Moscow pekee, waandamanaji 530 walikamatwa huku wengine 480 wakiwekwa kizuizini katika mji wa St. Petersburg. Hata hivyo, hakukuwa na taarifa zozote kutoka mamlaka za Urusi kuhusu maandamano hayo.
Orban: EU inafaa kuiondolea Urusi vikwazo
Wakati hayo yanaripotiwa, Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban ameutaka Umoja wa Ulaya kuondoa vikwazo dhidi ya Urusi kufikia mwisho wa mwaka huu. Hayo ni kwa mujibu wa gazeti la kila siku linaloiunga mkono serikali.
Gazeti hilo la Magyar Nemzet limeripoti kuwa, bwana Orban aliwatolea wito wanachama katika chama chake cha Fidesz kwenye mkutano wa faragha uliofanyika jana jioni, kufanya kila wawezalo kushinikiza vikwazo hivyo viondolewe.
Orban ambaye amekuwa na uhusiano wa karibu na Rais wa Urusi Vladimir Putin katika miaka ya hivi karibuni, mara kwa mara amekuwa akipinga vikwazo hivyo akihoji kuwa vinaiumiza zaidi Ulaya hata kuliko Urusi.