1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSlovakia

Kremlin yadai ndege za kivita hazitaleta mabadiliko Ukraine

17 Machi 2023

Ikulu ya rais ya Urusi, kremlin imeshtumu uamuzi wa Poland na Slovakia wa kupeleka silaha Ukraine pamoja na ndege za kivita za enzi ya Kisovieti na kutaja hatua hiyo kuwa ya uchochezi zaidi.

Russland | Dmitri Peskow
Picha: Valery Sharifulin/TASS/dpa/picture alliance

Msemaji wa ikulu ya rais ya Urusi, Kremlin Dmitry Peskov, amedai kuwa ndege za kivita chapa MiG-29 hazitaleta mabadiliko yoyote katika vita vya Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi lakini zitaleta matatizo zaidi nchini humo. Kulingana na shirika la habari la Interfax, Peskov amesema kuwa huu ni mfano mmoja zaidi wa jinsi mataifa wanachama wa muungano wa NATO yanaongeza ushiriki wao wa moja kwa moja katika mzozo huo.

Slovakia yaidhinisha kupelekwa kwa ndege za kivita Ukraine

Serikali ya Slovakia Ijumaa (17.03.2023) imeidhinisha mpango wa kuipa Ukraine ndege 13 za kivita za enzi ya kisovieti chapa MiG-29 na kuwa taifa la pili mwanachama wa NATO kuzingatia ombi la Ukraine la ndege za kivita kusaidia dhidi ya uvamizi wa Urusi. Akitangaza uamuzi huo wakati wa mkutano na wanahabari, waziri mkuu Eduard Heger, amesema kuwa serikali yake iko katika upande sawa wa historia. Mapema, Heger alituma ujumbe katika mtandao wa twitter akisema kwamba msaada wa kijeshi ni muhimu kuhakikisha kwamba Ukraine inaweza kujitetea na Ulaya yote dhidi ya Urusi.

Poland pia yatangaza msaada wa ndege za kivita kwa Ukraine

Siku ya Alhamisi, Poland ilitangaza kuwa itaipa Ukraine ndege kadhaa chapa MiG-29s, kwa kuanza na nne zinazotarajiwa kupelekwa nchini humo katika siku zijazo. Poland na Slovakia zote zilikuwa zimeashiria awali kwamba ziko tayari kutimiza ombi la Ukraine la ndege za kijeshi lakini kama tu sehemu ya muungano mpana wa kimataifa.

Rais wa Slovakia Zuzana ČaputováPicha: Aureliusz M. Pędziwol

Slovakia kupokea pesa za fidia

Waziri wa ulinzi wa Slovakia Jarolav Nad, amesema nchi hiyo itapokea dola milioni 213 kutoka Umoja wa Ulaya kama fidia na silaha za kiwango kisichojulikana kutoka Marekani za thamani ya dola milioni 745 kubadilishana na upelekaji wa ndege hizo aina ya MiG-29 nchini Ukraine. Mara kwa mara, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ameyaomba mataifa ya Magharibi ndege za kivita lakini mataifa wanachama wa NATO hayajaitikia wito huo na kutaja hatari ya kuchochea zaidi mgogoro huo.

Kwa kujibu tangazo la Poland la siku ya Alhamisi, ikulu ya White House imesema kuwa hatua hiyo ya Poland haitakuwa na ushawishi wowote kwa rais Joe Biden, ambaye amekataa wito wa kupeleka ndege za Marekani chapa F-16 Ukraine .

Umoja wa Ulaya kuunga mkono mpango wa kupeleka makombora milioni 1 Ukraine

Huku hayo yakijiri, wakati wa kongamano la Umoja wa Ulaya wiki ijayo, baraza la Umoja huo, linapanga kuunga mkono mpango wa kupeleka makombora milioni 1 kuisaidia Ukraine kukabiliana na uvamizi wa Urusi nchini humo. Hii ni kulingana na gazeti la Ujerumani la Handelsblatt lililoona rasimu ya makubaliano hayo hii leo. Kulingana na rasimu hiyo, maneno ya kifungu ambacho kinatoa wito wa kutolewa kwa haraka kwa silaha nchini Ukraine ikijumuisha kupitia ununuzi wa pamoja, huenda bado yakabadilika kabla ya kongamano hilo kuanza siku ya Alhamisi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW