Krismasi: Papa Francis atoa wito wa amani na kumaliza vita
25 Desemba 2024Ujumbe wa Kiongozi huyo unaofahamika kama "Urbi et Orbi" uliotolewa kwa ajili ya mji wa Vatican na ulimwengu kwa ujumla huelezea kwa muhtasari masaibu yanayoikabili dunia mwaka huu. Ikiwa sherehe za Krismasi zimeambatana na kuanza kwa sherehe ya Mwaka Mtakatifu wa 2025, Papa Francis ametoa wito wa "matumaini na upatanishi" hata na maadui zetu.
Akiwatubia umati wa watu mjini Vatican: " Ninamualika kila mtu na watu wote wa mataifa yote kuwa mahujaji wa matumaini na kunyamazisha sauti za silaha na kuishinda migawanyiko,'' aliwaambia Papa Francis akiwa kwenye roshani ya Kanisa la Mtakatifu Petro.
Katika mkesha wa Krismasi, Papa Francis aliufungua Mlango Mtakatifu wa Kanisa hilo ili kuzindua wiki ya kusherehekea mwaka mpya wa 2025, katika matarajio ya kupata rehema ya Mungu, aliyosema "inafungua kila fundo; inabomoa kila ukuta wa mgawanyiko; huku ikiondoa chuki na roho ya kisasi."
Soma pia: Wakristo duniani kote washerehekea sikukuu ya Krismasi
Baba mtakatifu amehimiza pia kusaka amani katika migogoro ya nchini Lebanon, Syria, Mali, Msumbiji, Haiti, Venezuela, Sudan, Myanmar, Nicaragua na katika Ukanda wa Gaza ambako amesema hali ya misaada ya kibinaadamu ni mbaya sana.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki ametoa pia wito wa kuachiliwa kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na kundi la Hamas huku akuelezea pia mlipuko mbaya wa ugonjwa wa surua nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wito wa kuvimaliza vita vya Ukraine
Wakati wa ujumbe huo wa kuadhimisha sikukuu ya Krismasi, Papa Francis ametoa wito wa kufanyika mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine ili kuvimaliza vita vilivyodumu kwa karibu miaka mitatu.
Katika ujumbe huo, Papa Francis alivitaja vita vya Ukraine moja kwa moja na ametaka uwepo ujasiri utakaowezesha kuufungua mlango wa kufanyika mazungumzo.
Akizungumza kutokea kwenye roshani ya kanisa la mtakatifu Peter, kuwahutubia maalfu ya waumini, kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani, amesisitiza kuwa milio ya silaha inapasa kunyamaza nchini Ukraine. Pia ametoa wito wa kuoneshwa ishara za mazungumzo ili kuleta amani ya haki na ya kudumu.
(Vyanzo: DPAE, APE)