1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuanzia tarehe 1-Januari, sheria mpya ya uhamiaji nchini Ujerumani

RM28 Desemba 2004

Baada ya majadiliano magumu na ya muda mrefu, wanasiana kutoka vyama tawala na vyama vya upinzani, kwa pamoja mwaka huu walifanya marekebisho kwenye sheria ya kuruhusu wageni kuingia nchini. Mageuzi haya yatarahisisha vipengee vingi kwa wahamiaji, yatatoa nafasi mpya kwa wageni kuhamia nchini Ujerumani na hapohapo kuwajumuisha vizuri zaidi kwenye maisha ya kila siku. Sheria mpya itaboresha pia hadhi ya wakimbizi.

Mfano wa wahamiaji nchini Ujerumani; mwanamke kavaa mtandio na baibui
Mfano wa wahamiaji nchini Ujerumani; mwanamke kavaa mtandio na baibuiPicha: AP

Kilichochokonoa mambo nchini Ujerumani mpaka kuwalazimisha wanasiasa kukaa pamoja na kujadiliana juu ya sheria mpya ya uhamiaji, ni matokeo ya utafiti wa muda mrefu kuwa, bila ya kuruhusu vijana wa kigeni kuingia nchini, uchumi wa Ujerumani utakwama siku moja kwa vile wajerumani hawazai watoto vya kutosha. Hata hivyo sheria mpya haitafungua nafasi za kazi kwa wageni kwa kiwango kikubwa. Wanasiasa bado wana wasiwasi na idadi kubwa ya wananchi wasio na ajira, ingawaje kwa upande mwingine wenye viwanda hawapendezwi na msimamo wa wanasiasa kwa upande huu.

Kama ilivyokuwa miaka iliyopita, wageni wanaotoka nje ya nchi wanachama kwenye umoja wa Ulaya, hawaruhusiwi kufanya kazi ndogondogo. Wanaweza kufanya kazi hizo kwa kutumia mikataba maalumu kati ya nchi na nchi, kwa mfano kwenye mashamba au hospitalini. Hata wananchi wanaotoka kwenye nchi mpya za Umoja wa Ulaya, hawaruhusiwi kutafuta kazi nchini Ujerumani – wao wanatakiwa kungojea miaka 7 kwanza.

Wasomi wa hali ya juu, kutoka nchi yeyote duniani, ndiyo wana nafasi nzuri. Mpaka hivi sasa wasomi wa kigeni walikuwa na nafasi ya kufanya kazi nchini Ujerumani kwa kutumia GREEN CARD kwa muda wa miaka mitano tu, sasa wana nafasi ya kufanya kazi bila kikomo.

Pia wanafunzi wa kigeni wanaomaliza masomo yao kwenye vyuo vikuu vya Ujerumani, wanaopenda kuendelea kuishi hapa nchini, watakuwa na nafasi ya kufanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja.

Wageni wengine wanaokaribishwa ni wafanyabiashara wa kujitegemea walio na mtaji wa zaidi ya Euro milioni 1 na walio tayari kutoa ajira kwa zaidi ya watu 10.

Urasimu umepunguzwa kwa watu wanaotaka kufanya kazi nchini Ujerumani: Kuanzia tarehe 1-Januari, watakuwa wanapatiwa viza na kibali cha kufanya kazi kwenye ofisi moja, kwa mfano kwenye ubalozi wa Ujerumani.

Sheria mpya ya uhamiaji, itarekebisha pia hitilafu zilizokuwepo, kwa mfano kwenye upande wa kuwajumuisha wageni takribani milioni 7.3 kwenye maisha ya kila siku hapa nchini.

Wageni watakaohamia Ujerumani hivi sasa, watakuwa na haki ya kupewa nafasi ya kujifunza lugha, pia kutambulishwa sheria, utamaduni na historia ya Ujerumani. Serikali imetenga kiasi cha Euro milioni 200 kwa ajili ya kazi hii.
Wageni wanaoishi hapa nchini, watu 50-elfu kila mwaka, wanaweza kulazimishwa na taasisi za serikali kushiriki kwenye kozi hizo. Anayekataa, hataongezewa viza na anaweza kupunguziwa misaada ya serikali. Mpaka hivi sasa, kozi hizi zilikuwa zinatolewa kwa wajerumani wanaohamia hapa nchini kutoka nchi nyingine, hasa za Ulaya mashariki kama vile Russia. Kwa mujibu wa sheria mpya, hata ndugu za wahamiaji, kama nao wanataka kuhamia Ujerumani, lazima wawe wanakimanya Kijerumani.

Sheria mpya ya uhamiaji itakayoanza kufanya kazi hapo tarehe 1-Januari, itaboresha pia hali ya wakimbizi. Hata watu wasiokimbia kunyanyaswa na utawala fulani, kwa mfano wanawake wanaokwepa kukeketwa, wanaweza kupewa sasa kinga ya ukimbizi, kama nchi yake haiwezi kumkinga.

Kipengee kilichopigiwa sana kelele na jumuiya za wakimbizi, kuitaka Ujerumani itoe viza ya kudumu kwa wageni wote waliokataliwa hifadhi ya kisiasa, hakikupitishwa. Wageni hawa ambao idadi yao ni takribani watu 200,000, huenda wakarudishwa makwao. Wachache tu kati yao, wale walioishi hapa nchini kwa zaidi ya miaka 5 ambao maisha yao yatakuwa hatarini wakirudi makwao, ndiyo watapewa kibali cha kuendelea kuishi Ujerumani kwa muda wa miezi 6.

Sheria mpya inanuia pia kuziba mwanya wa magaidi kuhamia nchini Ujerumani. Kabla ya wageni kupatiwa kibali cha kuhamia Ujerumani, watakuwa wanakaguliwa na taasisi maalumu ya kulinda katiba.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW