1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuapishwa kwa Chavez kunaweza kuahirishwa

5 Januari 2013

Kuapishwa rasmi kwa Rais Hugo Chavez wa Venezuela kwa kipindi kengine kipya cha miaka sita madarakani hapo tarehe 10 Januari kunaweza kuahirishwa iwapo kiongozi huyo anayetibiwa Cuba atashindwa kuhudhuria hafla hiyo.

Rais Hugo Chavez
Rais Hugo ChavezPicha: Reuters

Kauli hiyo iliotolewa na Makamo wake wa Rais Nicolas Maduro Ijumaa usiku(04.01.2013) ni dokezo la wazi kuwahi kutolewa kabla kwamba serikali ya Venezuela inapanga kuchelewesha hafla hiyo ya kumuapisha wakati ikijaribu kuepuka kumtangaza mtu wa kuchukuwa nafasi yake au kuitisha uchaguzi mpya katika nchi hiyo ya Amerika ya Kusini mwanachama wa Nchi Zinazosafirisha kwa Wingi Mafuta Duniani(OPEC).Kiongozi huyo wa kisoshalisti mwenye umri wa miaka 58 ambaye amekuwa madarakani tokea mwaka 1999 hajaonekana hadharani kwa zaidi ya wiki tatu sasa. Washirika wake wanasema yuko katika hali mbaya kufuatia operesheni ya nne katika kipindi cha miaka miwili kwa saratani iliyoko kwenye fupa lake la nyonga ambayo aina yake haikutajwa.Upinzani wa kisiasa nchini Venezuela unasema kwamba kuendelea kwa Chavez kuwepo Cuba hapo tarehe 10 mwezi wa Januari ambapo inatajwa kuwa yu mahtuti ni sawa na kujiuzulu kwa rais huyo.

Katiba yaruhusu

Lakini Maduro akiwa na nakala ya katiba wakati wa mahojiano na televisheni ya taifa amesema hakuna tatizo iwapo Chavez atakuja kuapishwa baadae na Mahakama Kuu ya nchi hiyo.

Makamo wa Rais wa Venezuela Nicolas Maduro.Picha: AFP/GettyImages

Amesema tafsiri iliyopo ni kwamba katiba hiyo ya mwaka 2013 hadi 2019 inaanza kutumika tarehe 10 mwezi wa Januari na kwamba katika kesi ya Rais Chavez yeye ni rais aliyechaguliwa tena na anaendelea na madaraka yake.Ameongeza kusema kwamba utaratibu rasmi wa suala hilo la kuapishwa unaweza kutatuliwa katika Mahakama Kuu wakati mahakama hiyo itakapoona unafaa kwa kuliratibu suala hilo na mkuu wa nchi.

Katika uchambuzi wa hali hiyo ya kisiasa isiyo ya kawaida Venezuela ambayo inaweza kutafsiriwa kwa njia mbili ni kwamba Maduro na washirika wengine wanaamini kuwa Chavez hatimaye atapona au kwamba wanapoteza wakati kuimarisha mipango ya urithi wa uongozi kabla ya kuingia katika uchaguzi.Maduro amesema licha ya hali mbaya ya afya ya Chavez hakuna sababu ya kumtangaza kwamba hatoweza tena kurudi madarakani. Tangazo hilo litasababisha kuitishwa kwa uchaguzi mpya katika kipindi kisichozidi siku 30.

Kupona inawezekana

Kwa mujibu wa Maduro, ambaye wiki hii alikwenda Havana kumjulia hali bosi wake huyo, Chavez ana fahamu zake na yuko njiani kupata nafuu.

Wafuasi wa Chavez wamuombea kiongozi wao.Picha: AP

Amesema "Kamanda huyo atapata nafuu tena."Maduro mwenye umri wa miaka 50 ambaye Chavez amemtangaza kuwa mrithi wake iwapo atalazimika kuachia madaraka amesema upinzani nchini Venezuela hauna haki ya kwenda kinyume na matakwa ya wananchi kama walivyoyaeleza katika uchaguzi wa tarehe 7 mwezi wa Oktoba kwa kumchaguwa tena rais huyo.Amesema "Rais huyo hivi sasa ndio rais. Msiwaruge wananchi. Heshimuni demokrasia."

Licha ya kusisitiza kwamba Chavez anaendelea kuw rais na kwamba kuna matumaini ya kupona serikali imekiri juu ya hali yake kuwa mbaya kwa kusema kwamba ana matatizo ya upumuaji kutokana na maambukizo makali ya mapafu.

Uvumi Chavez yu mahtuti

Mitandao ya kijamii ilikuwa imejaa uvumi kwamba kiongozi huyo anaishia kwa kutegemea mashine au anakabiliwa na saratani ya mifupa isiyobitika.Kuondoka kwa ghafla kwa Chavez katika jukwaa la kisiasa kutasababisha fadhaa kubwa kwa Venezuela. Sera yake ya ujamaa inayogharamiwa na mafuta imemfanya awe shujaa kwa maskini wakati wale wanaomkosoa wanasema ni dikteta anayetaka kulazimisha utawala wa kikomunisti wa mtindo wa Cuba kwa wananchi wa Venezuela.Iwapo Chavez itabidi aondoke madarakani uchaguzi mpya yumkini ukawapambanisha Maduro dereva wa basi wa zamani na mwanaharakati wa wafanyakazi dhidi ya kiongozi wa upinzani Herique Capriles gavana wa jimbo la Miranda mwenye umri wa miaka 40.

Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Henrique Capriles.Picha: dapd

Capriles alishindwa na Chavez katika uchaguzi wa mwezi wa Oktoba lakini alijipatia asilimia 44 ya kura. Juu ya kwamba chaguzi zilizopita zilimuonyesha kuwa mashuhuri zaidi kuliko washirika wengine wote wale wa Chavez hali hivi sasa ni tafauti kutokana na kwamba Maduro amepata baraka binafsi za rais jambo ambalo yumkini likawapa shauku wafuasi sugu wa Chavez kumuunga mkono.

Hali ya Chavez inafuatiliwa kwa makini na washirika wake wa Marekani Kusini waliofaidika na msaada wake na wawekezaji wanaovutiwa na deni la biashara lenye faida la nchi hiyo.

Mwandishi:Mohamed Dahman/RTRE

Mhariri: Stumai George

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW