1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

020511 NATO EU Bin Laden

3 Mei 2011

Jumuiya ya kujihami ya NATO pamoja na Umoja wa Ulaya zimiupongeza hatua ya kuuawa kwa kiongozi wa Al Qaeda, Osama Bin Laden. Hata hivyo swali bado limebakia iwapo tukio hilo ni hatua katika usalama dhidi ya ugaidi

Osama Bin LadenPicha: AP


Katibu Mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen amempongeza Rais wa Marekani, Barack Obama kutokana na kufanikiwa kwa operesheni hiyo ya kuuawa Bin Laden huko Pakistan ambapo amesema ni mafanikio katika usalama wa mataifa wanachama wa NATO.

Aidha Katibu Mkuu huyo wa NATO ameahidi kuendelea kwa ushiriki wa vikosi vya washirika wa jumuiya hiyo huko Afghanistan ili kuhakikisha nchi hiyo haiwezi kurejea tena kuwa pepo ya watu wenye kufuata itikadi kali za kidini.

Amesema wataendelea na harakati za kurejesha na kuimarisha nchini humo, uhuru, demokrasia na ubinaadamu vitu ambavyo amesema Osama Bin Laden alitaka kuvikandamiza.

Naye Mkuu wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso pamoja na Rais wa Baraza la umoja huo Herman Van Rompuy walitoa taarifa yao ya pamoja kupitia kwa msemaji wa kamisheni ya umoja huo Pia Ahrenkilde.

"Osama bin Laden alikuwa ni muhalifu ambaye anawajibika na mashambulio ya kutisha ya kigaidi yaliyogharimu maelfu ya maisha ya watu wasio na hatia. Kifo chake kinafanya dunia kuwa sehemu salama, na kuonesha kuwa uhalifu wa namna hiyo hauwezi kuendelea kuwepo bila ya kuadhibiwa. Na haya ni mafanikio makubwa katika juhudi zetu za kuinasua dunia na vitendo vya kigaidi. Umoja wa Ulaya utaendelea kuwa bega kwa bega na Marekani pamoja na washirika wetu wa kimataifa kwenye ulimwengu wa mataifa ya kiislam, katika mapambano dhidi ya ugaidi na kuifanya dunia kuwa salama, yenye amani na mustakhbali mzuri kwa watu wote´´

Herman Van Rompuy(kulia) na Jose Manuel Barroso (kushoto)Picha: dapd

Hata hivyo msemaji huyo wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya wakati akiwasilisha taarifa hiyo kwa waandishi wa habari mjini Brussels alikumbana na maswali ya waandishi wa habari wakihoji mazingira ya kifo hicho cha Bin Laden, lakini hata hivyo alipinga kuwa mauaji hayo yalikuwa ni ya kudhamiria kitu ambacho ni kinyume na mtizamo wa Ulaya.

Naye Guy Verhofstadt, ambaye ni mbunge kutoka chama cha kiliberali katika bunge la Umoja wa Ulaya alisema anasikitika kwamba Osama ameuawa na hakufikishwa mbele ya sheria katika mahakama ya kimataifa.

Kwa upande wake mratibu wa kitengo cha kupambana na ugaidi katika Umoja wa Ulaya ,Gilles de Kerchove, ametetea kitendo cha kuawa kwa Bin Laden, akisema kuwa lilikuwa ni jambo ambalo lisingeweza kuepukika.

´´Naipongeza operesheni hii ngumu iliyofanywa na kikosi maalumu cha wanajeshi wa Marekani, ambayo lengo lake lilikuwa ni kumkamata Bin Laden na kumfikisha mbele ya sheria. Mazingira hasa ya operesheni hii yalikuwa magumu na hayakuruhusu kuweza kumchukua akiwa hai, hivyo ikalazimika auawe. Hiyo ni hatua muhimu katika juhudi zetu za pamoja katika kuzuia na kupambana na ugaidi na hasa hiyo ndiyo sababu inayonifanya nikipongeze kitendo hicho´´

Hata Rais wa Bunge la Umoja wa Ulaya Jerzy Buzek hakuwa na tatizo katika kitendo cha kuawa Bin Laden ambapo alisema.

"Vitendo vya Bin Laden vimesababisha watu kutaabika kote duniani na vifo, Marekani, Ulaya, Afghanistan na sehemu nyingine. Watu wote wanaoamini na kutaka kuishi kwa amani leo wanaweza kuhisi kuwa wako salama.´´

Hata hivyo, Martin Schulz, ambaye ni kiongozi wa Social Democrats na wasoshalisti katika bunge la Ulaya, katika mahojiano na Radio ya Ujerumani ameonya uwezekano wa Al Qaeda kulipiza kisasi.
´´Ni lazima tujua kuwa mtandao wa al Qaida utajaribu kulipiza kisasi. Kwa hivyo naamini, kwamba katika wiki na siku zijazo ni muhimu kuzidisha umakini kwa sababu mashambulizi ya kigaidi au majaribio ya mashambulizi ya kigaidi yanategemewa kutokea hususan Marekani lakini pia yanaweza kutokea Ulaya.´´

Na mratibu wa kupambana na ugaidi katika Umoja wa Ulaya Gilles de Kerchove ameonya kuwa umuhimu wa Bin Laden kama nembo ya hamasa huenda ukayafanya makundi yanayomuunga mkono pamoja na watu binafsi kulipiza kisasi, hivyo ni muhimu kuwa makini.

Mwandishi: Liongo, Aboubakar Jumaa/Hasselbach, Christoph

Mhariri: Nyiro Charo, Josephat

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW