Kubadilishana wafungwa na kufufuliwa mazungumzo ya amani
19 Oktoba 2011Maelfu walipiga vigelele na kusherehekea,huku wakipepea bendera kubwa kubwa za Israel na kumwaga mauwa meupe na ya mawardi magari yaliyomshindikiza Shalit na wazee wake yalipowasili katika kijiji alikozaliwa cha Mitzpe Hila,kaskazini mwa Israel hapo jana.
Shangwe na sherehe zilihanikiza pia katika maeneo ya ukingo wa magharibi na Gaza kufuatia kuachiwa huru wafungwa 477,kundi la mwanzo la jumla ya wafungwa 1027 watakaoachiwa huru kuambatana na makubaliano ya kubadilishana wafungwa yaliyofikiwa kati ya Israel na Hamas.
Maelfu pia walikumbatiana na walio wao machozi yakiwatiririka,wengine hawakuwaona watoto au waume zao kwa kaidi ya miaka chungu nzima.
"Furaha iliyoje kupokewa namna hii.Nadhani miaka 30 ya usumbufu jela,imemalizika sasa."Amessema Allan Bazian.
Miongni mwa wafungwa hao, mia kadhaa walihukumiwa kifungo cha maisha kwa kukutikana na hatia ya kuhusika na mashambulio yaliyoangamiza maisha nchini Israel.
Kuna wengine wasiopungua 40 ambao Israel haikutaka warejee makwao na badala yake wamehamishiwa Uturuki,Qatar,Jordan na Syria.
"Ni hatua ya kihistoria,ingawa unakuwa na kinyongo moyoni unapokatazwa kurudi nyumbani,lakini tunaziangalia nchi zote za kiarabu kuwa ni sawa na nyumbani." amesema Mohammed Wael alipowasili Doha nchini Qatar hii leo.
Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani, serikali ya Marekani imeiarifu Israel wasiwasi wake kuhusu baadhi ya wafungwa walioachiwa huru.
"Tumewachunguza baadhi yao na tumeielezea serikali ya Israel msimamo wetu" amesema msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje Mark Toner na kuongeza" hawezi kufafanua zaidi."
Katika wakati ambapo serikali nyingi za dunia zimeelezea matumaini kuona makubaliana haya ya kubadilishana wafungwa yatafungua njia ya kufufuliwa mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina,msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani anahisi ni shida kuashiria jambo hilo.
Lakini waziri mkuu wa Uengereza David Cameron amezungumzia matumaini ya kujongelea amani kufuatia makubaliano hayo ya kubadilishana wafungwa.
Hata rais wa Marekani Barack Obama amewasihi waisrael na wapalestina waitumie fursa hiyo na kurejea katika meza ya mazungumzo.
Nae waziri mkuu wa Misri Essam Charaf amesema kubadilishana wafungwa kati ya Israel na Palestina ni sehemu ya juhudi za nchi yake ya kuimarisha utulivu na usalama katika eneo la mashariki ya kati.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFPE/dpa
Mhariri Yusuf Saumu