1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kucharazwa watoto hadharani kwazua sintofahamu Tanzania

4 Oktoba 2019

Mashirika ya kutetea haki za binadamu na ustawi wa watoto nchini Tanzania yamelaani vikali kitendo cha mkuu wa mkoa wa Mbeya kuwacharaza viboko hadharani wanafunzi wa sekondari kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Videostill AOM Africa on the Move Tansania Schule für Kinder mit Behinderung
Picha: DW/M. Grundlach

Kitendo hicho ambacho bado kimeendelea kuwa gumzo kinatajwa ni kinyume cha sheria ya kanuni ya viboko shuleni inayotamka kuwa, mwenye mamlaka ya kufanya hivyo ni mwalimu mkuu pekee au walimu wengine kwa ruhusa ya mwalimu mkuu.

Kikionekana kuchukizwa na hatua hiyo, kituo cha sheria na haki za binadamu kinaona kuwa tabia ya baadhi ya viongozi wa umma kujichukulia sheria mkononi ni ishara mbaya hasa kwa taifa ambalo limekuwa na miiko ya uongozi na maadili ya kazi.

Mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho, Anna Henga amesema viongozi wa umma hawapaswi kujiona kuwa wako juu ya sheria na kwamba hata kama wanafunzi hao walikuwa na utovu wa nidhamu wa aina gani bado walipaswa kuadhibiwa kwa kufuata kanuni.

Simu za mkononi zawatia wanafunzi matatani

Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Mkuu huyo wa mkoa wa Mbeya Albert Chalamila aliwacharaza bakora wanafunzi wa shule moja mkoani humo katika kile kilichofahamika kuwa walikwenda shuleni hapo na simu za mkononi na kutuhumiwa kuchoma moto moja ya mabweni ya shule hiyo.

Kumekuwa na mjadala mkali unaoendelea hasa kutokana na baadhi ya watendaji wa serikali kutoa matamshi na kushiriki katika matukio yanayodaiwa ni kinyume cha sheria.

Tukio la mkuu huyo wa mkoa ni sehemu ya matukio yanayolalamikiwa na wengi ikiwemo tukio la hivi karibuni la mkuu wa wilaya ya Kigamboni jijini Dar es salaam, Sarah Msafiri, aliyetangaza kuwavunja miguu wanananchi wanaotuhumiwa kwa matukio ya wizi.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakikosoa vikali mienendo hiyo na baadhi yaliahidi kwenda mahakamani kuwabana viongozi wanaokwenda kinyume na sheria.

Chanzo: DW Tanzania 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW