1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ireland inaitegemea kiasi gani Uingereza kibiashara?

7 Februari 2019

Suala la mpaka limetawala mawazo ya jamhuri ya Ireland katika kizungumkuti cha Uingereza kuondoka kwenye Umoja wa Ulaya maaruf Brexit.

Grenze Irland - Nordirland
Picha: Getty Images/AFP/P. Faith

Kutokana mivutano ya kisiasa waingereza kadhaa wametoa wito wa kutumiwa utegemezi wa kibiahsara wa jamhuri ya Ireland kwa Uingereza kama karata muhimu kwenye majadiliano kuhusu mpaka.

Mahojiano ya hivi karibuni kwenye kituo cha radio cha shirika la utangazaji la Uingereza BBC kati ya waziri wa masuala ya ulaya wa jamhuri ya Ireland na mtangazaji mkongwe John Humphyrs yalitoa picha kamili ya kwanini kizungumkuti cha Brexit  taratibu kinageuka kuwa hasira mjini Dublin huko Ireland.

Nadharia kutoka kwa mtangazaji wa BBC kwamba Uingireza ni muhimu mno kwa uchumi wa jamhuri ya Ireland na kwamba nchi hiyo itafaidi zaidi ikiwa Uingireza itapata mwisho mwema baada ya Brexit imezusha taharuki na hasira baada ya mahojiano hayo kuwafikia watazamaji wa Jamhuri ya Ireland.

Maswali na data nyingine za mtangazaji wa BBC kwa waziri wa Ireland ilikuwa ni sawa na kuwauliza wanasiasa wa nchi huru kuwa kwanini hawarejei kuwa makoloni ya watawala wao wa zamani. Mara zote hilo si swali la kuvutia kwa wanasiasa na huzusha ghadhabu.

Kile kilichoibuka kwenye mahojiano hayo ni kutiwa chumvi kulikopitiliza kwa baadhi ya takwimu za uchumi hasa kuhusu kiwango cha bidhaa kinachosafirishwa na Jamhuri ya Ireland kwenda Uingereza.

Mwandishi wa BBC alijaribu kutaka kuonesha kuwa Ireland husafirisha hadi asilimia 50 ya mauzo yake yote ya nje kwenda Uingereza jambo ambalo lilisahihishwa mara moja na waziri wa masuala ya ulaya wa Jamhuri ya Ireland.

Lakini msingi wa fikra hiyo kuwa Ireland inaitegemea sana Uingreza imekuwa maarufu sana katika mijadala nchini Uingereza kuhusu Brexit na patashika za hatma ya mpaka wa Ireland na Ireland ya Kaskazini.

Nadharia hiyo inakwenda mbali na kuamini kuwa kwa sababu  Ireland ina utegemezi mkubwa kiuchumi kwa Uingereza basi mwishowe itasalimu amri na  kuondoa madai yake kuhusu mpaka kwa sababu ikiwa Uingereza itajiondoa kutoka Umoja wa Ulaya bila mkataba hilo litakuwa jambo hatari zaidi kwa Ireland kuliko Uingereza.

Ireland ni tegemezi kibiashara kwa Uingereza?

Lakini ukweli ni kwamba madai kwamba Uingereza ndiyo mnunuzi wa asilimia 50 ya mauzo ya nje ya Jamhuri ya Ireland ni uongo mtupu.

Mwaka 2016 soko la Uingereza lilipokea asilimia 11 pekee ya mauzo ya nje kutoka Ireland na mwaka 2017 mauzo hayo yalifikia asilimia 12.

Licha ya ukweli kwamba takwimu hizo zinaonesha kuna kuimarika kwa biashara baina ya pande hizo mbili lakini hakuna dalali yoyote kukaribia mauzo ya nje ya asilimia 50 ya Ireland kwenda Uingereza.

Mwaka 2002 mauzo ya nje ya Ireland kwa Uingereza yalidorora zaidi ikilinganishwa na na miaka ya karibuni. Kulingana na data ambazo DW imezipata mwaka huo ni asilimia 23.9 pekee ya mauzo ya nje ya Ireland yalikwenda Uingereza ikilinganisha na asilimia 40 ya mauzo yaliyolifikia soko la Umoja wa Ulaya na 16 asilimia ya mauzo yalikwenda Marekani.

Kuimarika kwa utengamano katika kanda ya sarafu ya Euro kumesaidia zaidi mabadiliko hayo katika mauzo ya Ireland.

Takwimu za mwaka uliopita zinaonesha mauzo ya nje ya Ireland kwenda uingereza yalikuwa asilimia 11 pekee  ukilinganisha na asilimia 39 yaliyopelekwa katika mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya.

Sekta kadhaa za Ireland bado zina soko kubwa Uingereza

Picha: picture-alliance/robertharding

Licha ya ukweli kwamba masoko ya mauzo ya nje ya Ireland yametandaa katika miongo miwili iliyopita katika baadhi ya sekta utegemezi wa soko la nchini uingereza bado ni kubwa.

Sekta mojawapo ni ya chakula na vinjwaji. Mathalan kiasi asilimia 82 ya  bidhaa za mawazia ya Ireland iliuzwa nchini Uingereza na hilo linaweza kuelezea ni kwanini suala la mpaka wa Ireland limekuwa jambo la mjadala mkali kwa wamiliki wa viwanda wakihofia athari za Brexit kwa sekta hiyo ya kilimo nchini mwao.

Mbali ya mauzo nje liko suala pia la kuagiza biadhaa. Ireland inaingiza zaidi bidhaa kutoka Uingereza kuliko kutoka nchi nyingine yoyote duniani. Zaidi ya asilimia 24 ya bidhaa zinazoingizwa Ireland zinatoka Uingereza.

Hata hivyo ikiwa uingereza itaondoka Umoja wa uUaya bila mkataba mahsusi hilo litasababisha changamoto kadhaa kwa Ireland katika eneo la mauzo ya bidhaa zake nje ya nchi ambazo zitahitaji kutafutiwa ufumbuzi haraka.

Ireland na njia muhimu ya kusafirishia bidhaa zake

Picha: Getty Images/AFP/P. Faith

Lakini jambo linaloingia akilini kuhusiana na hatma ya Ireland kibiashara baada ya Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya ni njia ya kusafirisha bidhaa na umuhimu wa Uingereza kama ujia nafuu na wa kimkakati kibiashara na si hoja nyingine.

Kwa kutumia bandari za Uingereza wafanyabiashara wa Ireland wamekuwa wakinufaika zaidi kuyafikia masoko ya Ulaya kwa haraka na unafuu.

Vikwazo vyovyote kwenye njia hiyo ya jadi baada ya Brexit ikiwemo uchelewashwaji katika vituo vya forodha au ongezeko lolote la gharama vitazingatiwa kuwa vizingiti vikubwa kwa wafanyabiashara wa Ireland kuyafikia masoko ya Ulaya.

Juhudi zinajaribu kuchukuliwa kuondoa vikwazo hivyo.

Kwa hiyo wakati ni wazi kuwa Uingereza ni mshirika muhimu wa kibiashara kwa Ireland, umuhimu wake umekuwa ukiporomoka siku hadi siku kutokana na kuimarika kwa utengamano wa soko la Ulaya kupitia Umoja wa Ulaya.

Hata hivyo eneo ambalo Ireland inahitaji mpango mbadala ni katika sekta ya uchukuzi na njia za usafirishaji bidhaa zake kupitia Uingereza baada ya Brexit.

Na suluhisho lake ndiyo litaamua ikiwa Ireland itakuwa salama kiuchumi baada ya Brexit au kitisho cha Uingereza na nadharia chungu nzima kuhusu utegemezi wake kitakuwa dhahiri.

 Mwandishi: Rashid Chilumba/DW Engl

Mhariri: Iddi Ssessanga