1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJamhuri ya Kongo

Kuelekea upigaji kura Kongo, vijana watamani ajira

Hawa Bihoga | Iddi Ssessanga
14 Desemba 2023

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo inajiandaa na uchaguzi mkuu wa Desemba 20, lakini vijana wengi wanasema suala la msingi kwao ni amani na ajira, kwa ajili ya mustakabali wa taifa lao.

Kongo | Vijana wakiwa na vipeperushi na picha za wagombea wanaouwaunga mkono
Vijana wakiwa na vipeperushi vya wagombea wanaouwaunga mkono wakati huu wa kampeni.Picha: Paul Lorgerie/DW

Gedeon, 22, akiendesha bajaji yake katika mitaa yenye shughuli nyingi ya mji mkuu wa DR Kongo, Kinshasa, anasema hakuwahi kufikiria kwamba angeishia kufanya kazi anayofanya.

Kama ilivyo kwa vijana wengi katika taifa hilo lenye umaskini mkubwa la Afrika ya Kati, alisema ana matumaini makubwa kuwa seŕikali inaweza kuleta mustakabali mwema.

"Nataka kurudi shuleni," alisema Gedeon, ambaye amefanya kazi kama dereva wa bajaji kwa miaka mitano.

Anataka kuwa mhandisi wa umeme, alielezea, lakini umaskini ulimzuia kwenda chuo kikuu.

Wapiga kura wanatarajiwa kupiga kura mnamo Desemba 20 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Rais Felix Tshisekedi, 60, anawania muhula wa pili.

Vijana, ambao wengi wao wanakabiliwa na ukosefu sugu wa ajira -- wanaunda kundi muhimu la wapiga kura. Zaidi ya asilimia 60 ya wakaazi wa taifa hilo lenye watu milioni 100 wana umri wa chini ya miaka 20.

Soma pia:Uchochezi wa vita, ukabila vyatawala kwenye kampeni Kongo

Shirika la habari la Ufaransa, AFP liliwahoji vijana kadhaa wa Kongo kuelekea kura hiyo, ambapo wengi wao wameleezea shauku ya kurejea kwa amani katika nchi hiyo iliyokumbwa na migogoro -- na ajira.

Raphael Rubangiza, 18, anahusisha kura ijayo na matumaini ya soko bora la ajira. Alisema kuchagua "watu wenye uwezo" kutamaanisha "tutapata fursa, tutakuwa na kazi".

Lakini Rubangiza, ambaye anasomea uhandisi wa ujenzi huko Kinshasa, haoni matumaini makuwa. Wahitimu wengi "huishia kuuza vifurushi vya simu," alisema.

Ahadi za wagombea vinara

Kongo ni mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, licha ya utajiri mkubwa wa madini. Takriban theluthi mbili ya watu wanaishi kwa chini ya dola 2.15 kwa siku, kulingana na Benki ya Dunia.

Wagombea wakuu wa uchaguzi wa urais wote wameahidi kutoa nafasi zaidi za kazi. Tshisekedi ameahidi kuunda nafasi mpya za kazi milioni 6.4 iwapo atashinda muhula wa pili.

Wagombea vinara wa nafasi ya urais katika uchaguzi wa Desemba nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: AFP/Getty Images, picture alliance, G. Kusema, DW

Takwimu sahihi ni ngumu kupatikana, lakini ukosefu wa ajira unaaminika kuwa mwingi. Valery Madianga, mtafiti katika taasisi yenye makao yake mjini Kinshasa, alikadiria kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana kuwa takriban asilimia 70.

Maelfu ya watu huhitimu kila mwaka ili tu kuingia kwenye soko la ajira na fursa chache zinazotoweka, iwe katika sekta ya kibinafsi au ya umma.

Prisca Musangi, 27, alisomea sheria mjini Kinshasa lakini hakuweza kupata kazi.

"Sisi, vijana waliohitimu, tunataka kujiunga na kuwa na taaluma katika taasisi za umma bila kupendekezwa," alisema, akimaanisha upendeleo ambao mara nyingi hutawala nani anayeajiriwa.

Soma pia:  Katumbi asitisha kampeni zake baada ya vurugu Kongo

Alfred Bopando, mwenye umri wa miaka 29, mkuu wa kampuni ya fedha na mawasiliano, vile vile alisema anataka rais ajaye "kuwapa kazi vijana". Amechoshwa na ahadi hewa: "Hatuwezi tena kuvumilia ahadi," Bopando alisema.

Floribert Anzuluni, mmoja wa wagombea wadogo zaidi wanaowania nafasi ya urais aneshiriki katika uchaguzi huo, ambaye anataka kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana, alikubaliana.

"Hali hii haiwezi kutatuliwa kupitia ahadi," kijana huyo mwenye umri wa miaka 40 alisema. "Ili kutengeneza nafasi za ajira, unahitaji kuunda makampuni."

Kukomesha mzozo mashariki mwa Kongo

Kumaliza mzozo nchini Kongo pia ni ajenda kuu ya wapiga kura wengi vijana. Beni Mingi, 25, mfanyakazi wa posta huko Kwilu magharibi mwa nchi, alisema anataka mabadiliko makubwa. 

"Waliopewa madaraka hawajafanya lolote,” alisema. "Katika suala la usalama, daima kuna vita."

Eneo la masharikilinakabiliwa na makundi yenye silaha, ambayo ni urithi wa vita vya kikanda vilivyopamba moto katika miaka ya 1990 na 2000. Kundi mojowapo, M23, limeteka maeneo mengi katika eneo hilo tangu lianzishe mashambulizi mwishoni mwa 2021.

Wapiga kura wataka mabadiliko Kongo

02:54

This browser does not support the video element.

Soma pia: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inatarajia kufanya uchaguzi Disemba 20, huku kukiwa na wasiwasi wa kiusalama

Katika mji wa mashariki wa Goma, ambao unakaribia kuzungukwa na M23 -- mwanafunzi wa sheria Brave Kafumbiri alisema kuwa kurejesha utulivu ni jambo la kipaumbele. 

Viongozi wa siku zijazo lazima "wakomeshe M23, ama kijeshi au kidiplomasia," kijana huyo wa miaka 25 alisema.

"Tunamaliza masomo yetu, hatuna kazi, kuna ukosefu wa usalama katika eneo lote la mashariki mwa nchi, idadi ya watu wanaishi chini ya dola 2 kwa siku," alisema, akitoa muhtasari wa matatizo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW