1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa rais wa EU, lipi linamkabili von der Leyen?

15 Julai 2019

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen, aliyeteuliwa kugombea urais wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya, ameahidi kuimarisha utekelezaji wa matarajio wa umoja huo yahusuyo mabadiliko ya tabianchi.

Ursula Von der Leyen
Picha: picture-alliance/AA/D. Aydemir

 

Kura ya bunge inatarajiwa kupigwa majira ya kesho jioni Jumanne.

Waziri huyo wa ulinzi na mshirika wa karibu wa kansela wa Ujerumani Angela Merkel, aliteuliwa na viongozi wa Umoja wa Ulaya mwezi hii, kuchukua nafasi ya rais wa sasa Jean-Claude Junker kuanzia Novemba 1.

Uteuzi wake unatakiwa kuthibitishwa na wingi wa kutosha wa wabunge wa bunge la Umoja wa Ulaya. Hata hivyo, bunge hilo limegawanyika juu ya uteuzi wake, na hivyo hata uthibitisho wake kwa kiasi kikubwa umegubikwa na sintofahamu.

Hata baada ya uteuzi wake wiki iliyopita, bado pande za Wasoshaliti na Maliberali ambao wanashika nafasi ya pili ya tatu ya kuwa na wingi wa wabunge wanaokiunga mkono chama cha siasa kali za mrengo wa kati cha EPP cha Von der Leyen, wanataka ufafanuzi zaidi kutoka kwa mwanamama huyo ya sera.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anampigia upatu pakubwa bi von der LeyenPicha: Reuters/P. van de Wouw

Miongoni mwake ni pamoja na matamshi yake kwamba anataka Umoja wa Ulaya kuwa na matarajio makubwa juu ya suala la mabadiliko ya tabianchi, lakini pia kuwa na mpango wa kuibua malengo ya mwaka 2030 ya kupunguza usambazaji wa gesi chafu.

Amesema atajiuzulu bila kujali matokeo ya kura ya bunge.

Lengo la mwaka 2030 ni kupunguza usambazaji wa gesi chafu kwa asilimia 40, ikilinganishwa na viwango vya mwaka 1990, lakini von der Leyen alizungumzia kuhusu kuwa na matarajio ya kupunguza hadi asilimia 55.

Kwenye barua ya kurasa nane ya wabunge wa Kisoshalisti na Democratic iliyoonwa na shirika la habari la DPA, von der Leyen pia alielezea kuunga mkono kulipa bunge haki ya kutoa maamuzi, kuliruhusu kuwasilisha mapendelezo ya kisheria, itakapoonekana wengi wa wabunge watakuwa wanayaunga mkono.

Von der Leyen atatakiwa kupata kura za wabunge 153 wa Wasoshalisti ili kufikia kiwango cha wingi unaotakiwa wa kura 374 za bunge hilo. Lakini wabunge 16 wameapa kutowaunga mkono washirika wenzao. Kwenye barua hiyo hiyo, kundi la wabunge wa Kiliberali la Renew Europe, lenye wabunge 108, bado halijaamua kuhusiana na uteuzi wa waziri huyo wa ulinzi wa Ujerumani.

Kuhusu Brexit, von der Leyen ameyaambia makundi hayo ya wabunge kwamba ataunga mkono Uingereza kuongezewa muda wa uanachama wa Umoja wa Ulaya, iwapo tu kutatolewa sababu za msingi. Alirudia kusema kwamba makubaliano ya kujiondoa kati ya Umoja huo na Uingereza ni mazuri na yanayowezekana iwapo wanataka kuondoka kwa utaratibu. 

na wakati kura hiyo ikisubiriwa, mnamo siku ya Jumatatu bi von der Leyen aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba atajiuzulu wadhifa wa uwaziri wa ulinzi bila kujali matokeo ya kura hiyo ya Jumanne. 

Alisema, "nitaomba bunge liniamini, lakini nitajiuzulu wadhfa wa waziri wa ulinzi bila ya kuzingatia matokeo ya kura hiyo ifikapo siku ya Jumatano ili niweze kuwatumikia watu wa Ulaya kwa nguvu zangu zote."