1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kufikia amani, Taliban yataka rais wa Afghanistan kuondoka

23 Julai 2021

Kundi la Taliban limesema halitaki kuhodhi madaraka lakini linasisitiza hakutakuwa na amani nchini Afghanistan hadi kuwepo na serikali mpya mjini Kabul na Rais Ashraf Ghani aondolewe.

Afghanistan | Taliban
Picha: Danish Siddiqui/REUTERS

Hayo yameainishwa katika mahojiano kati ya shirika la habari la Associated Press na msemaji wa Taliban Suhail Shaheen, ambaye pia ni mwanachama wa timu ya majadiliano ya kundi hilo,ambalo limedai kudhibiti asilimia 90 ya mipaka ya Afghanistan.

Kundi la Taliban limekamata maeneo kadhaa katika wiki za karibuni, kuteka kivuko cha kimkakati cha mpakani, na sasa wanatishia idadi kadhaa ya miji mikuu ya majimbo, mnamo wakati wanajeshi wa mwisho wa Marekani na Jumuiya ya NATO wakiondoka nchini Afghanistan. 

Wiki hii afisa wa juu wa Marekani, Jenrali Mark Milley, aliuambia mkutano wa habari wa wizara ya ulinzi, Pentagon, kwamba Taliban wana msukumo wa kimkakati, na hakuondoa uwezekano wa kundi hilo kuchukua udhibiti kamili wa nchi.

Serikali ya wa Afghanistan wote

Rais Ashraf Ghani wa AfghanistanPicha: Alex Brandon/AP/dpa/picture alliance

Shaheen amesema Taliban wataweka chini silaha zao pale serikali ya muafaka inayokubaliwa na pande zote itakapoingia madarakani mjini Kabula, na serikali ya Ghani ikiwa imeondoka.

"Ni jambo la muhimu kwamba wa Afghani wote wanakuwa na au wanapaswa kukubaliana juu ya serikali mpya, na kwamba serikali hiyo itachukuwa nafasi ya utawala huu wa Kabul, na kwamba serikali hiyo itakubalika kwetu na wa Afghan wengine," alisema Shaheen.

Shaheen ameweka wazi kwamba wao hawaani katika kuhodhi madaraka kwa sababu serikali yoyote iliyotaka kuhodhi madaraka nchini Afghanistan huko nyuma haikufanikiwa, katika matamshi yanayodhirika kuhusisha pia utawala wa miaka mitano wa Taliban katika tathmini hiyo, na kuongeza kuwa hawataki kurudia mfumo sawa.

Lakini alikuwa pia mgumu kuhusu kuendelea kwa utawala wa Ghani, akimuita mchochezi wa vita na kumtuhumu kutumia hotuba yake ya siku kuu ya Eif al-Adha Jumanne, kuahidi mashambulizi dhidi ya Taliban. Shaheen alitupilia mbali haki ya Ghani kuongoza, na kufufua madai ya wizi mkubwa yalioughubika ushindi wa Ghani katika uchaguzi wa 2019.

Ghani amesema mara kwa mara kwamba atasalia madarakani hadi uchaguzi mpya utakapoamua serikali ijayo. Lakini wakosoaji wake, wakiwemo wa nje ya Taliban, wanamtuhumu kwa kutaka kung'ang'ania madaraka, na kusababisha mgawiko miongoni mwa wafuasi wa serikali.

Uhakikisho kwa wanawake

Picha: Abdul Khaliq Achakzai/REUTERS

Shaheen amesema chini ya serikali mpya, wanawake wataruhusiwa kufanya kazi, kwenda shuleni na kushiriki katika siasa, lakini watalaazimika kuvaa hijab au mtandio.

Amesema wanawake hawatahitajika kuambatana na ndugu wa kiume wakati wanatoka majumbani mwao, na kwamba makamanda wa Taliban katika wilaya mpya zilizotekwa na kundi hilo wana maagizo kwamba vyuo vikuu, shule na masoko vifanye kazi kama hapo kabla, ikiwmeo ushiriki wa wanawake na wasichana.

Madai juu ya udhibiti wa mipaka

Wakati huo huo, wizara ya ulinzi ya Afghanistan imekanusha madai ya Taliban kwamba kundi hilo linadhibiti asilimia 90 ya mipaka ya nchi, ikisitiza kuwa vikosi vya serikali ndiyo vinadhibiti mipaka hiyo.

Naibu msemaji wa wizara hiyo Fawad Aman, ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la AFP, siku moja baada ya Taliban kutoa madai hayo.

Madai ya Taliban siku ya Alhamisi yalikuja baada ya kundi hilo kuteka vivuko muhimu vya mpakani na Iran, Tajiskistan, Turkmenistan na Pakistan katika wiki za karibuni, katika mashambulizi makali yalioanzishwa baada ya kuanza kuondoka kwa vikosi vya Marekani nchini Afghanistan.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW