Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte kuachana na siasa
10 Julai 2023Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte ametangaza hii leo kuwa ataachana na siasa baada ya kuitishwa kwa uchaguzi mkuu kufuatia kujiuzulu kwake kutokana na mzozo kuhusu uhamiaji ambao umeiangusha serikali yake.
Uamuzi huo unamaanisha kumalizika kwa takriban miaka 13 ya utawala wa kiongozi huyo wa kihafidhina, ambao umekuwa ukigubikwa na kashfa katika mihula yote minne alipokuwa akihudumu kama Waziri Mkuu wa Uholanzi.
Rutte kiongozi mwenye umri wa miaka 56 wa chama cha People's Party for Freedom na Demokrasia, au VVD, aliuita kuwa ni uamuzi binafsi na bado hakuna dalili za haraka za kubaini ni nani atachukua nafasi ya kiongozi huyo katika chama chake, ingawa kundi la wabunge wa chama hicho linaongozwa kwa sasa na msaidizi wa zamani wa siasa wa Rutte, Bi Sophie Hermans.
Soma zaidi: Raia wa Uholanzi wapinga hatua za kukaa karantini
Tarehe ya uchaguzi nchini Uholanzi bado haijawekwa wazi ingawa inaelezwa huenda ikawa kabla ya mwezi Oktoba au Novemba. Hiyo ina maana kwamba Rutte atasalia ofisini kama waziri mkuu wa mpito kwa miezi kadhaa na pia bado ataweza kuhudhuria mkutano wa kilele wa NATO unaoanza kesho Jumanne nchini Lithuania.
Katika nchi za Umoja wa Ulaya zenye wanachama 27, ni Waziri Mkuu wa Hungary pekee Viktor Orban ambaye amekuwa madarakani kwa muda mrefu kuliko Mark Rutte ingawa kuna tofauti ya mifumo ya kiutawala ya nchi hizo mbili.
Muungano wa vyama vinne ulioongozwa na Rutte ulijiuzulu siku ya Ijumaa baada ya kushindwa kukubaliana juu ya hatua za kudhibiti uhamiaji za Umoja wa Ulaya, suala ambalo mara nyingi limeleta mgawanyiko ndani ya nchi ya umoja huo.
Rutte anasema uamuzi huo ulifikiwa kulingana na kushindwa kufikiwa kwa makubaliano ndani ya vyama washirika vinavyounda serikali yake.
Soma zaidi: Mark Rutte ashinda uchaguzi mkuu Uholanzi
Rutte alitaka kuweka vikwazo vya kuziunganisha tena familia za wanaotafuta hifadhi, kufuatia kashfa ya mwaka jana kuhusu vituo vya hifadhi vilivyojaa watu.
Mvutano uliibuka wiki hii wakati Rutte alipodai kuungwa mkono kwa pendekezo la kuzuia kuwasili kwa watoto wa wakimbizi wa vita ambao tayari wako Uholanzi.
Pendekezo hilo pia litafanya familia kusubiri angalau miaka miwili kabla ya kuunganishwa tena. Mapendekezo hayo yalipingwa vikali nan washirika wake wa CDCU na mrengo wa kushoto wa D66. Uholanzi tayari ina moja ya sera kali zaidi za uhamiaji barani Ulaya.
Maombi ya hifadhi nchini Uholanzi yameongezeka kwa theluthi moja mwaka jana, na serikali imekadiria kuwa yanaweza juu 70,000 mwaka huu - juu ya kiwango cha juu cha 2015.
Wafuasi na wapinzani nchini Uholanzi wameuita uamuzi huo kuwa ni mwisho wa enzi wakisema kwamba Rutte kwa wakati fulani aliweza kuwapotosha washirika wake wa muungano na wabunge wa upinzani kupitisha baadhi ya sera mpya ambazo ziillitia nchi katika dosari ya kisiasa iliyogharimu mamilioni ya fedha.
Soma zaidi: Viongozi wa EU wakutana kujadili mfuko wa ufufuaji uchumi
Katika Baraza la Wawakilishi la bunge la Uholanzi kuna vyama visivyopungua 20 vinavyowakilishwa, na kwa sasa vyama vya mrengo wa kati ni kama vinapoteza nguvu kwa watu wa mrengo wa kulia na kushoto.
Licha ya Rutte kuachia ngazi lakini bado atakumbukwa kwa namna alivyoingoza Uholanzi kupitia machafuko kuanzia janga la Uviko-19, mafuriko, ajali ya ndege huko Malaysia na ile ya kudondoshwa kwa ndege nchini Ukraine ambayo iliua mamia ya raia wa Uholanzi na viongozi wa upinzani walisifu jinsi kiongozi huyo alivyoyashughulikia matatizo hayo.