Umaarufu wa chama cha SPD wazidi kushuka Ujerumani
18 Januari 2018Imani ya wananchi kwa chama cha SPD imeporomoka na kusalia asilimia 18.5 tu kufuatia uchunguzi wa maoni uliofanywa wiki iliyopita, na taasisi ya Insa mara baada ya Martin Schulz na viongozi wenzake wa vyama vya kihafidhina vya CDU/CSU kukamilisha mazungumzo ya kutathmini uwezekano wa kuunda serikali ya muungano wa vyama vikuu-GroKo.
SPD wameporomoka kutoka asili mia 20.5 walizojipatia uchaguzi mkuu ulipoitishwa Septemba 24 iliyopita, matokeo yaliyotajwa kuwa pigo kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa katika chama hicho tangu mwaka 1949.
Kuchapishwa matokeo ya utafiti wa maoni wa taasisi ya Insa kumesadifu mnamo wakati ambapo Martin Schulz anakutana na wakuu wa chama cha SPD katika jimbo la magharibi la North Rhine Westphalia ili kuwatanabahisha waunge mkono mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano pamoja na kansela Angela Merkel, mkutano mkuu wa chama chao utakapoitishwa siku ya Jumapili (21.01.2018) mjini Bonn.
Madhara makubwa mkutano mkuu ukipinga
Sauti zinapazwa kuonya dhidi ya kishindo kitakachoibuka pindi mkutano mkuu wa SPD ukipinga mpango wa kuanzishwa mazungumzo amoja na CDU/CSU. Kundi la mrengo wa kulia ndani ya chama cha SPD linalojulikana kama kundi la "Seeheimer" linahofia madhara makubwa pindi wawaakilishi watapiga kura ya la Jumapili inayokuja mjini Bonn.
"Pindi SPD wakipinga fikra ya kuundwa serikali ya muungano wa GroKo, basi kuna hatari kubwa ya kuzidi kupoteza kura uchaguzi mpya utakapoitishwa. Kundi hilo linakadiria SPD wataporomoka na kufikia asili mia 15 hadi 16 ya kura.
Msemaji wa kundi hilo la Seeheimer Edgar Franke anasema itakuwa shida sana kwa SPD kujiinua pindi wakiporomoka. Onyo kama hilo limetolewa pia na waziri wa zamani wa afya Ulla Schmidt anaesema "uchaguzi mkuu mwengine utamaanisha Ujerumani itabidi kusubiri hadi mwisho wa mwaka 2018 kujipatia serikali mpya, ingawa mizani ya kisiasa haitobadilika sana.
Katibu Mkuu SPD apuuza hofu
Katibu mkuu wa SPD, Lars Klingbeil anasema anazielewa hofu zilizoko kuelekea vyama ndugu vya CDU/CSU hata hivyo anashauri watu wasitaharuki na kuhoji kwa kuwa kansela Merkel anapinga kuongoza serikali ya wachache, kitakachobakia ni ama uchaguzi mpya au kupata ridhaa ya kuunda serikali ya muungano wa vyama vikuu.
Hofu zimeenea pindi mkutano mkuu wa SPD ukiamua kutounga mkono fikra ya kuendelezwa mazungumzo ya kuundwa serikali ya muungano wa vyama vikuu, uongozi wa chama hicho utalazimika kujiuzulu.
Katibu mkuu wa SPD Lars Klingbeil amejaribu kutuliza hofu hizo akisema hazina msingi."Ni makosa kufungamanisha masuala ya kimsingi na yale ya uongozi".
Akizungumza na waandishi habari anasema ikiwa hilo lilikuwa likitokea zamani, basi lilikuwa kosa. Anasaema Januari 21 mada itakayoamuliwa ni kama wana SPD wanataka au la kuanzisha mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano pamoja na CDU/CSU na sio zaidi.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu