1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kujiuzulu kwa Hamdok kwatishia uongozi mbaya Sudan

3 Januari 2022

Wachambuzi Sudan wamesema kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa taifa hilo kunalipa jeshi mamlaka kamili ya uongozi na kutishia kurejea kwa sera za ukandamizaji zilizokuwepo wakati wa utawala wa Omar al Bashir.

Sudan Premierminister Abdalla Hamdok
Picha: AFP

Baada ya miezi kadhaa ya maandamano na kamata kamata dhidi ya waandamanaji, iliyosababisha vifo vya watu 57, wachambuzi wanahofia umwagikaji damu zaidi baada ya Waziri Mkuu Abdalla Hamdok kujiuzulu nafasi yake hiyo siku ya Jumapili (02.01.2021)

Katika hotuba yake aliyoitoa kupitia televisheni ya kitaifa, Hamdok alisema amejaribu kuizuwiya Sudan kutumbukia katika mgogoro zaidi lakini kwa sasa imefikia hatua hatari iliyo njia panda inayotishia mustakabali wa taifa hilo.

Magdi al-Gizouli wa taasisi moja ya utafiti, amesema kujiuzulu kwa Hamdok kumeliacha jeshi kuwa na mamlaka kamili ya kuamrisha, huku akiongeza kuwa waandamanaji wataendelea kuandamana na itabidi wakabiliane na vurungu zaidi.

soma zaidi: Sudan: Waziri mkuu Abdalla Hamdok ajiuzulu

Mjumbe wa Umoja wa mataifa anayeshughulikia masuala ya Sudan Volker Perthes, amesema anajutia hatua ya Hamdok na kuelezea hofu ya kutanuka kwa mgogoro wa kisiasa na kuchelewesha hatua iliyopigwa tangu kufanyika  mabadiliko mwezi Desemaba.

kwa upande wake Marekani imewataka viongozi wa Sudan kuweka kando tofauti zao na kupata suluhu ya pamoja, kuhakikisha kuendelea kuwepo kwa utawala wa kiraia. Taasisi ya masuala ya Afrika nchini humo imesema, Waziri Mkuu wa Sudan pamoja na Baraza la Mawaziri wanapaswa kuteuliwa chini ya makubaliano ya katiba ili kutimiza matakwa ya wananchi ya ´kupatikana kwa uhuru, amani na haki.

Wanaharakati waitisha maandamano dhidi ya utawala wa jeshi

Maandamano ya kupinga utawala wa jeshi mjini Khartoum, SudanPicha: AFP/Getty Images

Hata hivyo wanaharakati wameendelea kutoa wito wa maandamano zaidi ya kupinga utawala wa kijeshi kuanzia siku ya Jumanne (04.01.2022) kuwataka waandamanaji kupiga kambi katika ikulu ya rais hadi ushindi utakapopatikana.

Jeshi kwa upande wake limejipa madaraka ya kusitisha upinzani. Burhan mwezi uliopita alipitisha sheria kuwaruhusu maafisa wa usalama kuwakamata watu kwa uhalifu unaohusiana na hali ya dharura ambayo inapiga marufuku maandamano ya barabarani.

soma zaidi: Marekani yahimiza utawala wa kiraia baada ya Hamdok kujiuzulu

Magdi al-Gizouli anasema mambo yalioko hatarini sasa ni makubwa huku akisisitiza kuwa Hamdok ndio aliyokuwa mpatanishi wa pande zote. Amesema vuta nikuvute ipo kati ya wanajeshi na mfumo wa zamani bila ya kumuhusisha Omar al Bashir na mavuguvugu yasiokuwa na viongozi mitaani inayowajumuisha vijana.

Aidha John Prendergast, wa taasisi nyengine ya utafiti amesema mataifa ya kigeni yalio na nguvu hayapaswi kuangalia tu mambo yanavyoendelea Sudan. Ameongeza kuwa Marekani na Umoja wa Ulaya zikisubiri muda mrefu bila ya kuchukua hatua, utawala uliopo utaendelea kutumia nguvu ya kiuchumi na kisiasa kuleta madhara makubwa kwa watu wa Sudan.

Watu 57 wapoteza maisha tangu maandamano ya Oktoba 25

Waandamanji wakibeba picha za wenzao waliouwawa tangu kuanza kwa maandamano Oktoba 25Picha: AFP/Getty Images

Tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Uingereza na Misri mwaka 1956, Sudan ambayo ni miongoni mwa mataifa masikini duniani imekuwa mara nyingi chini ya utawala wa kijeshi kukiwa na nafasi chache za uongozi wa kidemokrasia. Imekuwa ikijaribu kupita katika kipindi kigumu cha mpito kuelekea utawala kamili wa kiraia tangu mwezi Aprili mwaka 2019 baada ya Omar al Bashiri kuondolewa madarakani kufuatia maandamano makubwa dhidi yake.

Bashir, anaetakikana na Mahakam ya Kimataifa ya uhalifu ICC kujibu mashitaka ya uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur aliwekwa kizuizini wakati Sudan ikipiga hatua kujiunga tena na jamii ya kimataifa ili kusamehewa madeni yake na msaada wa uwekezaji wa kigeni.

Sudan: Vikosi vya usalama vyatumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji

Lakini kipindi cha mpito kilichoyumba kilicheleweshwa kufuatia mapinduzi yaliyofanywa na jeshi Oktoba 25 wakati kiongozi mpya wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah al Burhan alipoipindua serikali na kumzuwiya waziri Mkuu Abdalla Hamdok pamoja na baraza lake la mawaziri.

Hatua hiyo ilikosolewa vikali kimataifa na kusababisha maandamano makubwa nchini Sudan kupinga mapinduzi hayo, watu 57 waliuwawa huku mamia wengine wakijeruhiwa na wanawake 13 wakiripotiwa kubakwa katika vurugu zilizosababishwa na maandamano hayo.

Chanzo: afp

    

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW