1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Kuleba awaambia wakosoaji wa magharibi "kufunga mdomo"

1 Septemba 2023

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dymitro Kuleba ametoa matamshi makali dhidi ya wakosoaji wa mataifa ya magharibi walioonyesha mashaka juu ya mkakati wa mapambano wa Kyiv dhidi ya majeshi ya Urusi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dymtro Kuleba amewataka wakosoaji wa magharibi kuacha mara moja kukosoa mashambulizi yao dhidi ya vikosi vya Urusi.
Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dymtro Kuleba amewataka wakosoaji wa magharibi kuacha mara moja kukosoa mashambulizi yao dhidi ya vikosi vya Urusi.Picha: ISABEL INFANTES/REUTERS

Katika siku za karibuni, maafisa wa mataifa ya magharibi wamekosoa juu ya kasi ndogo ya Kyiv ya kusonga mbele katika mapambano dhidi ya wanajeshi wa Urusi, hatua ambayo Kuleba anasema ni sawa na tusi kwa wanajeshi wao. 

Kuleba ametoa matamshi hayo makali mbele ya waandishi wa habari wakati wa mazungumzo ya mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya katika mji wa Toledo nchini Uhispania, baada ya kuwashukuru mawaziri hao wa Ulaya kwa kuisaidia serikali yake hadi sasa huku akiwaomba kuisaidia Ukraine kwa silaha kali zaidi, makombora ya masafa marefu, magari ya kijeshi na mifumo zaidi ya kujilinda angani.

Soma Pia: Mawaziri wa ulinzi wa EU wajadili msaada wa muda mrefu kwa Ukraine.

Amesema "Kukosoa kasi ndogo ya operesheni ya kujibu mapigo ni sawa na kumtusi mwanajeshi wa Ukraine anayejitolea maisha yake kila siku, akisonga mbele na kukomboa kilomita moja ya ardhi ya Ukraine baada ya nyingine. Ningependekeza wakosoaji wote wafunge midomo yao, waje Ukraine wajaribu kukomboa hata sentimita moja ya mraba wao wenyewe."

Ukraine imekuwa ikitetea kasi yake ya mashambulizi, na kusema hatua za polepole huwa zinalenga kuvuruga mpango wa ulinzi wa Urusi katika maeneo wanayoyakalia nchini humo.

Soma Pia: Ukraine yasema ina uhakika Ujerumani itaipatia makombora ya Taurus

Kuleba aidha ameuzungumzia mkutano ujao wa mwezi Septemba kati ya rais Vladimir Putin wa Urusi na Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki unaolenga kuyafufua makubaliano ya nafaka kupitia Bahari Nyeusi, akisema huenda yakawa fursa ya mwisho kwa Moscow kurejea kwenye makubaliano hayo.

Uturuki inajaribu kuangazia namna inavyoweza kuishawishi Urusi kurejea kwenye makubaliano ya nafaka iliyojitoa.Picha: Murat Cetinmuhurdar/Turkish Presidential Press Office/REUTERS

Aidha amezungumzia juu ya mpango mbadala wa kusafirisha nafaka kupitia pwani ya Bahari Nyeusi ya nchini Romania, lakini akisema mifumo ya kujilinda angani ilikuwa inahitajika ili kuzilinda meli zitakazobeba nafaka kabla ya kuingia kwenye eneo la maji hayo.

Ukraine yaendeleza mashambulizi ya droni dhidi ya Urusi.

Tukiyageukia mashambulizi yenyewe, maafisa wa Urusi wamesema mapema leo kwamba wamezidungua ndege zisizokuwa na rubani zilizokuwa zikielekeea katika mikoa mitatu ya magharibi mwa Urusi. Magavana wa mikoa hiyo wamesema mifumo ya kujilinda angani imezizuia ndege hizo tatu katika mikoa ya Kursk, Belgorod na Moscow. Viwanja vya ndege vya Moscow vilifungwa kwa muda, hii ikiwa ni kulingana na mamlaka za Urusi.

Ukraine imekuwa ikilaumiwa na Urusi kwa msururu wa karibu kila siku wa mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani nchini Urusi wakati vita kati ya mataifa hayo vikiingia mwezi wa 19.

Huku hayo yakiendelea, meya wa Moscow  Sergei Sobyanin amesema anataka kuimarisha mfumo wa kujilinda wa mji huo, katikati ya ongezeko la mashambulizi hayo ya droni ya Ukraine.

Taarifa za vyombo vya habari kutoka Kyiv zimesema, Ukraine imekiri kushambulia eneo la kiwanja cha ndege cha jeshi katika mkoa wa Kursk siku chache zilizopita kwa kutumia aina mpya ya droni. Duru za idara ya ujasusi kwenye jeshi la Ukraine, SBU zimesema jana kwamba walitumia droni hizo mpya Jumamosi usiku.

Katika hatua nyingine, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma pendekezo jipya kwa Urusi ili kuwezesha upatikanaji wa nafaka na mbolea katika soko la ulimwengu, na kwa matumaini ya kuyafufua makubaliano ya nafaka yaliyoruhusu ukraine kusafirisha karibu tani 33,000 za nafaka katikati ya ongezeko la njaa duniani.

Hata hivyo, Moscow imesema mapema wiki hii kupitia waziri wa mambo ya nje Sergei Lavrov kwamba haijaridhishwa na pendekezo hilo na kusema imeipatia Uturuki orodha ya hatua ambayo magharibi inatakiwa kuchukua ili kurejeshwa kwa makubaliano hayo.  

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW