1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UtamaduniTanzania

Kumbukumbu ya miaka 124 ya kunyongwa kwa Mangi Meli

Veronica Natalis
4 Machi 2024

Maadhimisho hayo ya miaka 124 sasa, yamefanyika katika eneo la Old Moshi Mkoani Kilimanjaro na kuwashirikisha viongozi wa serikali ya Ujerumani na Tanzania.

Kiongozi wa Wachaga Mangi Meli aliyeuliwa kwa kunyongwa na kisha kukatwa kichwa na wajerumani katika kipindi cha ukoloni
Kiongozi wa Wachaga, Mangi Meli aliyeuliwa kwa kunyongwa na kisha kukatwa kichwa na wajerumani katika kipindi cha ukoloniPicha: DW

Katika hotuba yake wakati wa maadhimisho hayo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Katja Keul, amebainisha kuwa ni muhimu nchi ya Ujerumani ikaukabili ukweli kuhusu mabaya yaliyofanywa enzi za utawala wa kikoloni na kwamba utawala huo wa kijerumani nchini Tanzania ulikuwa wa kinyama na wa kikatili.

''Hatuwezi kuyafuta makosa ya nyuma''

Katja Keul aliambia hadhara iliyohudhuria maadhimisho hayo pia kunaushahidi mwingi uliowekwa katika kumbukumbu unaodhihirisha matendo ya kikatili ikiwapo Wajerumani kuwaua kwa kuwanyonga viongozi wa kimila wa Tanganyika.

"Kama Mjerumani, nina aibu kwa yale ambayo mababu zetu walifanya nina omba msahama, nina toa heshima zangu kwa Mangi Meli na machifu wengine 18  tunaowakumbuka leo na waathiriwa wote wa utawala wa kikoloni nchini Tanzania.'', alisema Keul. 

Kabla ya kuongeza kusema : ''Ninaomba radhi ya dhati kwa mateso ambayo wakoloni walisababisha, kama mwakilishi wa serikali ya Ujerumani nina sema hatuwezi kuyafuta makosa ya nyuma lakini tunaweza kujadiliana nini tunaweza kufanya ili kusaidia angalau kuponya maumivu yenu. Kama Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alivyosema huko Songea tutafanya kila liwezekanalo kurudisha mafuvu ya ndugu zenu.''

Mabaki kurejeshwa nyumbani ?

Mkuu wa wilaya ya Moshi, Kisare Makori, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, akimkabidhi zawadi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Katja KeulPicha: Veronica Natalis/DW

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, mkuu wa wilaya ya Moshi  Kisare Makori amesema hatua ya Ujerumani kuomba radhi na kutaka kurudisha mafuvu ni ya heshima na ya kihistoria na serikali ya Tanzania inataka familia za viongozi hao walionyongwa enzi za ukoloni wapate fursa ya kuzika kwa heshima mabaki ya miili ya mababu zao.

Tanzania imekuwa ikiiwekea shinikizo serikali ya Ujerumani, iwajibike kutokana na ukatili wa enzi za ukoloni Afrika Mashariki. Mafuvu yaliyopelekwa Ujerumani kama nyara za kivita wakati wa ukoloni yalihifadhiwa Berlin kwa zaidi ya miaka 100.

Chifu Mangi Meli, alikuwa kiongozi wa Wachaga wa Kilimanjaro, ambaye alinyongwa na wanajeshi wa Kijerumani pamoja na watu wengine 18, wakiwemo maakida na machifu mnamo karne ya 19.

Ujerumani iliomba msamaha kwa maovu ya ukoloni wake

Mangi Meli alinyongwa pamoja na watu wengine 18, wakiwemo maakida na machifu mnamo karne ya kumi na tisaPicha: Konradin Kunze

Mnamo ziara yake nchini Tanzania November 2023, rais wa Shirikisho la Ujerumani Frank-Walter Steinmeier aliomba rasmi msamaha kwa mauaji ya kikatili kukandamiza vuguvugu la kupinga ukoloni kusini mwa Tanzania ya leo, katika vita vya Maji maji.

Watu wapatao 300,000 katika maeneo ya Songea walikufa katika uasi huo dhidi ya ukoloni wa Ujerumani kati ya mwaka 1905 na 1907. Pamoja na zana nzito za kijeshi, Wakoloni wa kijerumani pia waliharibu mazao ili kuwadhoofisha wapiganaji wa kiafrika kwa njaa.

Historia ya vita vya majimaji inayofundishwa katika shule za msingi na sekondari katika nchi za Afrika inaeleza madhara ya vita hivyo vya kikoloni, na jinsi viongozi wa sasa wa mataifa ya Afrika wanavyoweza kujifunza uzalendo wa kiuongozi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW