1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kumbukumbu ya miaka 10 ya kifo cha Nelson Mandela

Admin.WagnerD5 Desemba 2023

Raia wa Afrika Kusini na dunia kwa ujumla wapo katika kumbukumbu ya muongo mmoja tangu kifo mpiganiaji uhuru na rais wa kwanza mweusi baada ya utawala wa ubaguzi wa rangi, Nelson Madiba Mandela.

Nelson Mandela - 10. Todestag
Hayati Nelson Mandela, aliyekuwa rais wa Afrika KusiniPicha: Kim Ludbrook/EPA//picture alliance/dpa

Maadhimisho hayo yanafanyika wakati Afrika Kusini ikipitia kipindi kigumu cha kiuchumi na kisiasa, hasa kutokana na kashfa za rushwa zinazokiandama chama tawala cha ANC. 

Maadhimisho haya ya awamu ya kumi yanafanyika huku wakosoaji wa rais Cyril Ramaphosa, wakimtuhumu kwa kushindwa kuenzi yale aliyoyapigania muasisi huyo ndani ya chama, hasa linapokuja suala la rushwa serikalini pamoja na ukosefu wa ajira hasa kwa vijana weusi.

Mambo mazuri ya Mandela hayazingatiwi

Prince Fekade ni mwenyekiti wa chama cha wapigania uhuru wa kiuchumi EFF katika vyuo vikuu vya Afrika Kusini anasema miongoni mwa yale ambayo Nelson Mandela aliyoyapigania hayazingatiwi kama alivyokusudia.

Hayati Nelson Mandela akiwa na Princes Diana ambae pia ni marehemuPicha: Zieminski/epa/AFP/dpa/picture-alliance

Miaka 29 imekatika tangu watu weusi ambao ni sawa na asilimia 80.5 ya raia wote washike hatamu za uongozi Afrika Kusini. Cha ajabu pamoja na kwamba wao ndio wengi, bado wanamiliki  asilimia 4 tu ya ardhi ya kufanya shughuli za kilimo hapa Afrika Kusini.

Asilimia kubwa ya ardhi Afrika Kusini inamilikiwa na jamii ya wachache

Wazungu ambao ni sawa na asilimia 8 ya raia wote, wao wanamiliki asilimia 72 ya ardhi ya kilimo, wahindi ambao ni sawa na asilimia 2.5 ya raia wa Afrika Kusini, wanamiliki asilimia 5 ya ardhi yote huku raia waliochanganya wazazi, mweusi na mweupe yaani machotara ambao uwingi wao ni sawa na asilimia 9 ya raia wote, wao wanamiliki asilimia 14 ya ardhi.
Ni kwa sababu hiyo Ernest Bongani mkazi wa Pretoria anasema, chini ya utawala wa ANC, haoni cha kujivunia. Wakati chama tawala kikipitia wakati mgumu, uchumi wa taifa hili nao umeendelea kuzorota, huku raia wengi wakilalama kukosa huduma mbalimbali za msingi ikiwemo maji, umeme na mishahara duni isiyoendana na hali halisi ya uchumi wa taifa hili lenye viwanda vingi barani Afrika.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Ndileka Mandela ambaye ni mjukuu wa Nelson Mandela, ni wakati wa kuiga (ubuntu) yaani utu wa babu yake.

Somza zaidi:Askofu Tutu afariki dunia
Mamia ya raia wameshaanza kumiminika kijijini Qunu, alikozaliwa Nelson Mandela na wanatarajia kufanya ibada ya kumkumbuka muasasisi huyo aliyefariki December 5, mwaka 2013, huku Urithi Unaishi Kupitia Wewe ikiwa ndiyo kauli ya maadhimisho ya muongo mmoja tangu kifo cha muasisi huyo wa taifa la Afrika Kusini.

DW: Afrika Kusini

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW