1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIraq

Kumbukumbu ya miaka 20 tangu mwanzo wa vita vya Iraq

20 Machi 2023

Imetimia miaka 20 tangu kuanza kwa uvamizi ulioongozwa na Marekani na kuuangusha utawala wa aliyekuwa rais dikteta wa Iraq Saddam Husein. Hata hivyo hakuna sherehe ambazo zimepangwa kufanyika.

Sturz Saddam-Statue
Picha: Patrick Baz/dpa/picture alliance

Taifa hilo lenye utajiri wa mafuta limesalia likizongwa na kiwewe cha miaka mingi ya vita, uvamizi, misukosuko na machafuko ya kidini yaliyotokana na operesheni iliyoanzishwa Machi 20, 2003.

Mfano wa utulivu ndio umerejea, lakini Iraq ingali inakabiliwa na misururu ya changamoto, ikiwemo ukosefu wa utulivu wa kisiasa, umaskini na ufisadi uliokithiri.

Leo, raia wa Iraq wana maoni yanayokinzana kuhusu hali ya nchi yao, Mohammed Abbas ni mhandisi na anahisi mambo yanazidi kwenda kombo. "Tunaona ufisadi kwenye sekta ya afya na huduma za kiraia. Ndiyo tunashuhudia. Hali inazidi kuwa mbaya zaidi."

Pentagon yaahidi kuendelea kuisaidia Iraq kupambana na IS

Lakini Abu Ali, ambaye ni mfanyabiashara anayemiliki mkahawa anaridhika na hali iliyoko. "Maoni yangu ni kwamba mfumo kwa sasa ni mzuri. Angalau tuna kiasi cha demokrasia na uhuru. Mambo yamebadilika na hali pia imebadilika".

Miaka 20 tangu kuanza kwa vita nchini Iraq, nchi hiyo ingali inakumbwa na kiwewe kutokana na vita hivyo vilivyosababisha kuangushwa kwa utawala wa rais dikteta Saddam Hussein na mwishowe kunyongwa kufuatia hukumu ya kifo.Picha: Karim Sahib/dpa/picture-alliance

Ushawishi wa Iran nchini Iraq

Iran, nchi yenye nguvu kubwa ya Kishia lakini adui wa Marekani, kwa sasa ina ushawishi mkubwa Iraq, ambayo Washia wake wengi waliachiliwa kutoka ukandamizaji wa Saddam aliyekuwa Msunni.

Waziri Mkuu Mohamed Shia al-Sudani, anayeungwa mkono na muungano unaouunga mkono Iran, hajasema lolote kuhusu uvamizi wa Marekani, isipokuwa kuanguka kwa utawala wa kidikteta wake Saddam, ambaye baadaye alinyongwa kufuatia hukumu ya kifo dhidi yake.

Mnamo mkesha wa kumbukumbu ya leo, Sudani alisema: "Tunakumbuka machungu na mateso ya watu wetu katika miaka hiyo iliyotawaliwa na vita visivyokuwa na maana pamoja na hujuma za kimfumo”.

Vita vya Iraq vilichochewa na nini?

Rais Bush akiwa kwenye manuwari ya kivita ya Marekani alitangaza kuwa ‘Lengo Limetimizwa' baada ya wanajeshi wake kudhibiti mji mkuu Baghdad, wiki tatu tu baada ya vita kuanza.Picha: Stephen Jaffe/AFP/Getty Images

Vita vya Marekani nchini Iraq, vilianza wakati wa utawala wa rais wa zamani wa Marekani George W. Bush na vilishika kasi baada ya mashambulizi ya mtandao wa Al-Qaeda wake Osama Bin Laden dhidi ya Marekani mnamo Septemba 11, 2001.

Bush aliyeungwa mkono na Waziri Mkuu wa Uingereza wa wakati huo Tony Blair, alihoji kuwa Saddam Hussein alikuwa kitisho kwa ulimwengu na kwamba alikuwa akitengeneza silaha za maangamizi makubwa. Hata hivyo hakuna silaha za aina hiyo ziliwahi kupatikana.

Operesheni iliyoitwa Uhuru wa Iraq, ilianzishwa na wanajeshi 150,000 wa Marekani pamoja na wanajeshi 40,000 wa Uingereza na mashambulizi makali ya angani dhidi ya vituo vya kimkakati.

Miaka 10 baada ya Saddam Hussein

Baada ya wiki tatu, utawala wa Saddam ulianguka na ilipofikia Aprili 9, wanajeshi waliovamia nchi hiyo wakawa wanadhibiti mji mkuu Baghdad.

Kanda ya video iliyotangazwa ulimwenguni ilionyesha wanajeshi wa Marekani wakiangusha sanamu kubwa ya Saddam.

Changamoto zilizotokana na vita hivyo

Juhudi za Marekani kuleta demokrasia ya kiliberali nchini Iraq zililemazwa na vita na machafuko ya kidini, huku wapiganaji wa Kishia wakipambana na makundi ya Kisunni.Picha: Karim Sahib/dpa/picture-alliance

Lakini uvamizi huo ulichochea uporaji na hali kubwa ya uvunjifu wa sheria. Machafuko yaliongezeka kufuatia uamuzi wa Marekani kukivunja chama tawala na vifaa vya kijeshi vya nchi hiyo.

Mnamo wakati wanajeshi wa Marekani walikuwa wakiondoka Iraq mwaka 2011, zaidi ya raia 100,000 wa Iraq walikuwa wameshauawa kufuatia vita hivyo, na Marekani iliwapoteza takriban wanajeshi 4,500. Hayo ni kulingana na shirika la haki za binadamu Body Count Group la Iraq.

Maafa hayo yalichochea kuchipuka kwa Wasunni wenye misimamo mikali ya Kiislamu waliojiita ‘Dola la Kiislamu' IS ambao wapiganaji wake wa kidini walisababisha maafa mapya ya kutisha kote Iraq na Syria, kabla ya wao pia kushindwa na muungano ulioongozwa na Marekani uliorejea kusaidia katika vita dhidi yao.

Maoni: Miaka 20 tangu Marekani ilipoivamia Iraq

This browser does not support the audio element.

Chanzo: AFPE

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW