1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuna haja gani kuandaa mikutano ya COP kila mwaka?

1 Desemba 2023

Je ni kwa nini Umoja wa Mataifa huandaa mkutano wa kilele kila mwaka wa COP kuhusu tabia nchi, mwaka huu ukiwa mara ya 28? Je mikutano hiyo ina tija gani?

Watu wakitembea katika eneo lililoko ukumbi wa mkutano wa kilele wa tabia nchi COP28 kule Dubai, katika Umoja wa Falme za Kiarabu
Watu wakitembea katika eneo lililoko ukumbi wa mkutano wa kilele wa tabia nchi COP28 kule Dubai, katika Umoja wa Falme za KiarabuPicha: Thaier Al-Sudani/REUTERS

Lau ungewauliza watu wengi juu ya kinachozungumziwa katika mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabia nchi, huenda jibu litakuwa ni: Eti? Na ukiwauliza wanaofahamu juu ya kinachozungumziwa kwenye mkutano huo wa hali ya hewa. Jibu jingine huenda likawa ni: Kwa nini nijali? Na ndipo kunazuka swali, je ni kwa nini Umoja wa Mataifa uandae mkutano huo wa kilele kila mwaka katika muda wa miaka 28 iliyopita? 

Mazungumzo hayo yaitwayo Mkutano wa Wadau au Vyama (COP) huchukua takriban wiki mbili. Mwaka huu mazungumzo hayo ambayo ni ya 28, ndipo yakaitwa Cop28, yanafanyika Dubai.

Wajumbe hutumia misamiati isiyoeleweka kwa urahisi kwa wote kama vile NDCs, nyuzi joto 1.5, hasara na uharibifu na kadhalika.

Maafikiano yao aghalabu si ya kulazimisha nchi kuyatekeleza. Ina maana, nchi zinaweza kukubaliana kuhusu jambo fulani lakini zisiweze kulitekeleza.

Na wakati maelfu kwa maelfu ya wajumbe wanaposafiri kuhudhuria mkutano huo, gesi chafu nyingi hutolewa, jambo linalokwenda kinyume na dhamira kuu ya mkutano huo.

Vikao vya COP pia hutengeneza mada na kuamua jinsi ya kuzungumzia masuala muhimu.Picha: Amr Alfiky/Reuters

Basi ni kwa nini kujisumbua? Hata baadhi ya wanaharakati wengi wa mazingira wakati mwingine huuliza swali hilo. Isitoshe kuna mjadala unaozidi kuongezeka ikiwa mchakato wa sasa unahitaji mageuzi makubwa.

Lakini ukitizama kwa kutumia darubini na kwa kuzingatia uhalisia wa mambo kwamba maendeleo mara nyingi huja polepole, tofauti na tukio la kushangaza lenye athari mbaya, kuna sababu nyingi ambazo kwa hakika mazungumzo hayo yanaweza kuwa ya manufaa.

Misukumo ya mikutano ya COP kwa Mataifa

Msukumo wa mikutano ya COP ni sehemu muhimu ya maendeleo katika kuangazia michango inayoamuliwa kitaifa ijulikanayo kama NDCs. Hii ni mipango ya kila nchi ya kupunguza matumizi ya mafuta, gesi na makaa ya mawe ambayo hutoa gesi ukaa na kuathiri mazingira. Aidha mipango hiyo huainisha mikakati ya nchi kukabili athari za majanga ya hali ya hewa.

Mikutano ya kimazingira ya COP huweka malengo kuwa wazi, jambo ambalo wakati mwingine baadhi ya mataifa au mashirika hayapendi.

Maelfu kwa maelfu ya wajumbe husafiri kwa ndege kuhudhuria mikutano ya COP. Wakati wa safari hizo gesi chafu nyingi hutolewa, jambo linalokwenda kinyume na dhamira kuu ya mikutano hiyoPicha: Saul Loeb/Pool/AFP

Mkataba wa Paris ulianzisha lengo bainifu ambalo limeongoza majadiliano ya hali ya hewa tangu wakati huo. Ikiwa ni pamoja na utoaji gesi chafu kutokana na uchomaji wa nishati ya visukuku ili kuhakikisha wastani wa hali joto duniani hauzidi 2 katika vipimo vvya Celsius.

Vikao vya COP pia hutengeneza mada na kuamua jinsi ya kuzungumzia masuala muhimu. Kwa mfano mazungumzo ya hali ya hewa ya mwaka jana, COP27 nchini Misri, yalitoa makubaliano muhimu kwa nchi tajiri kuchangia mfuko wa kusaidia mataifa yanayoendelea kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mfuko wa "hasara na uharibifu"

Kwa miongo kadhaa, wanaharakati wa mazingira wamekuwa wakitoa hoja kwamba mfuko wa "hasara na uharibifu" ulikuwa muhimu kwa sababu mataifa tajiri, ambayo yalijiendeleza kiviwanda kwa kutumia nishati chafu, yalichangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya hali ya hewa. Na kwamba wakati nchi hizo zikiendelea, nchi maskini zilikuwa zikiathirika zaidi, kwani hazina raslimali za kutosha kudhibiti mafuriko, mawimbi ya joto, ukame wa muda mrefu na athari nyingine za ongezeko la joto ulimwenguni.

Athari za mafuriko zawaacha wakaazi wa Dar es Salaam wakihangaika. Picha hii ilipigwa Novemba 6, 2023.Picha: Amas Eric/DW

Soma pia: COP28 yazindua mfuko wa hasara na uharibifu wa tabianchi

Bila maamuzi ya lazima au njia za kutekeleza makubaliano, inaweza kuonekana kama njia ya kufeli. Hata hivyo, katika kipindi cha karibu miaka 30 ya mikutano ya kilele ya COP, matokeo yanaweza kutajwa kuwa na mafanikio na yenye matumaini.

Kwa kwa mfano, miaka 10 iliyopita kiwango cha uzalishaji wa gesi chafu kilikuwa kinakaribia kufikia nyuzi joto 4 Celsius,

ambayo wanasayansi wanasema ingeleta hali mbaya sana. Leo, uzalishaji huo duniani unakadiriwa kuwa kati ya nyuzi joto 2 hadi 2.5, vipimo vya Celsius.

Bila shaka hakuna chaguo mbadala. Mazungumzo kwenye mikutano ya COP ndiyo njia pekee kwa ulimwengu kushughulikia athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa pamoja.

Hebu fikiria tu jinsi inavyoweza kuwa vigumu kwa watu wawili kukubaliana chochote. Sembuse nchi 200?

Soma pia: Mzozo wa Israel na Hamas utaathiri vipi mkutano wa COP28?

Biden kutohudhuria Mkutano wa kilele wa COP28

Chanzo: APAE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW