1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la G7 lakamilisha mkutano wa kilele

Yusra Buwayhid
26 Agosti 2019

Kundi la mataifa saba yaliyoendelea zaidi kiviwanda G7 limekamilisha mkutano wa kilele Jumatatu baada ya kujadili changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na moto wa msitu wa Amazon na vita vya kibiashara vya Marekani.

G7-Gipfel in Frankreich
Picha: Getty Images/AFP/P. Wojazer

Mkutano huo wa kilele katika mji wa Biarritz kusini magharibi mwa Ufaransa, ghafla ulibadilika muelekeo baada ya kuwasili Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Javad Zarif kuja kujadili mkwamo wa kidiplomasia unaohusu makubaliano ya kinyuklia yaliyoafikiwa mwaka 2015.

Zarif hakuwa akitarajiwa kuhudhuria mkutano huo, lakini alialikwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ambaye anajaribu kutuliza mvutano kati ya Iran na Marekani.

Wanadiplomasia wa Ufaransa wamesema Zarif na Trump hawakuzungumza, lakini uwepo wao katika chumba kimoja angalau umetoa matumaini.

Moto wateketeza Amazon

Katika siku ya pili na ya mwisho ya mkutano huo wa kilele, viongozi wa mataifa hayo saba ambayo ni -- Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan na Marekani -- waligusia pia moto unaoteketeza msitu wa Amazon, ambao viongozi hao wameueleza kama shambulio dhidi ya 'mapafu' ya ulimwengu. Trump kwa upande wake hakuwa na mengi ya kusema juu ya suala hilo.

Soma zaidi: G7 yaingilia kati moto wa Amazon

Suala kubwa zaidi lililodhihirisha mpasuko kati ya Trump na viongozi wengine katika mkutano huo wa G7 ni la biashara, na juhudi za rais huyo wa Marekani za kuwabania masoko hata washirika wa karibu pamoja na kuwapandishia ushuru wa bidhaa.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiwa na Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/AP Photo/I. Langsdon

Trump aliwasili mjini Biarritz baada ya kusisitiza kuwa ataiongezea ushuru China katika wakati ambapo nchi hizo mbili zinavutana kibiashara.

Trump amuahidi biashara Johnson

Katika mkutano huo, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alikuwa mshirika wa hivi karibuni wa kundi la nchi za G7 kumsihi Trump aachane na vita vya biashara ambavyo wakosoaji wanahofia vinaweza kuuporomosha uchumi wa dunia.

Trump ametabiri kuwa Johnson atafanikiwa kuikwamua nchini yake katika mchakato wa Brexit wa Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya. Rais huyo wa Marekani mwenye umri wa miaka 73 amemuahidi Johnson makubaliano makubwa ya kibiashara ambayo hayakuwahi kushuhudiwa.

Halikadhalika, Trump na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe wametangaza kuafikiana juu ya makubaliano ya kibiashara ambayo wanatarajia kuyasaini mwezi ujao.

Mkutano wa pamoja wa viongozi hao na waandishi habari ambao ndiyo utafunga mkutano huo utafanyika baadaye Jumatatu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW