1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la G7 lakosoa vita vya Sudan

13 Novemba 2025

Mawaziri wa nchi za nje wa mataifa saba yaliyoendelea kiviwanda duniani G7, wamekosoa vurugu za Sudan wakisema mapigano kati ya jeshi la taifa hilo na wanamgambo wa RSF, yamesababisha mgogoro mkubwa wa kibinaadamu.

G7-2025 | Niagara
Kundi la G7 lina wasiwasi kuhusu visa vya unyanyasaji wa kingono katika vita ya Sudan.Picha: Mandel Ngan/AFP

Katika taarifa yao ya pamoja, mawaziri hao kutoka Canada, Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Japan, wamesema wana wasiwasi kuhusu visa vya unyanyasaji wa kingono vinavyoendelea katikati ya vita hivyo vilivyodumu kwa takriban miaka miwili.

Kwengineko Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Marco Rubio ametoa wito wa hatua za kimataifa kuchukuliwa ili kulipokonya silaha kundi hilo la RSF, huku akilinyooshea kidole cha lawama kwa umwagikaji wa damu unaozidi kushuhudiwa Sudan na mateso kwa raia ikiwemo ubakaji.

"Tuna mtazamo sawa kama wengine kuhusu jinsi hali inavyoweza kubadilika na kutoa nafasi kwa makundi ya jihadi na kigaidi kuendesha shughuli zao Sudan. Suluhu ya hilo ni kutoendelea kupigana kutoendelea na vita ambavyo raia wanalengwa kwa kubakwa, kunyanyaswa kingono, na kuuawa. Na hayo ndiyo yanayotokea,” alisema Marco Rubio.

Mgogoro wa Sudan hadi sasa umesababisha mauaji ya maelfu ya watu huku wengine takriban milioni 12, wakiachwa bila makao. Mgogoro huo pia umesababisha janga kubwa la njaa. Pande zote mbili, Jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF, wameshutumiwa kwa kutekeleza ukatili dhidi ya raia katika vita hivyo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW